Naibu Waziri wa TAMISEMI, David Silinde

GEITA

Na Antony Sollo

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Kitengo cha ukusanyaji mapato wamemuomba Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, kuunda tume ya wataalamu kufanya uchunguzi kubaini ukweli kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za umma zilizotolewa dhidi yao na madiwani wa halmashauri hiyo, JAMHURI limeelezwa.

Akizungumza na JAMHURI kwa sharti la kutoandikwa gazetini kwa kuhofia usalama wake, mmoja wa watumishi hao (jina tunalo), ameliambia gazeti hili kuwa kinachoendelea katika halmashauri hiyo ni vita ya kutaka kuwaondoa watumishi hasa wasiokubaliana na masuala fulani yanayopendekezwa na baadhi ya wanasiasa wanaotafuta kura kwa wapiga kura wao kujinufaisha kisiasa.

“Sisi watumishi tuliotuhumiwa katika sakata la upotevu wa mamilioni ya fedha za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe tunamuomba Waziri wa TAMISEMI atende haki kwa kusikiliza pande zote, sisi tumesikitishwa na uamuzi wa Naibu Waziri wa TAMISEMI kushindwa kutoa nafasi ya kufanyika uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, hali hii inaweza kutuvunja mioyo,” anasema mmoja wa watumishi hao.

Aprili 8, mwaka huu, Naibu Waziri wa TAMISEMI, David Silinde, akiongozana na Mbunge wa Mbogwe mkoani Geita, Nicodemas Maganga, alifanya ziara ya kushtukiza kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ili kujionea namna miradi hiyo inavyoendelea.

Katika ziara hiyo, naibu waziri alitembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, ikiwamo Shule ya Sekondari ya Lulembela,  Shule ya Sekondari ya Mbogwe, Shule ya Msingi Kasandalala pamoja na ujenzi wa barabara ya kilomita 1.2, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Aidha, Naibu Waziri Silinde alisikitishwa na uongozi wa Shule ya Sekondari ya Lulembela kushindwa kukamilisha ujenzi huo kwa miaka miwili, ambapo aliagiza viongozi kuandika maelezo na kuyatuma wizarani.

“Ofisa Elimu tatizo nini mpaka ifike miaka miwili bila kukamilishwa ujenzi wa vyumba vya madarasa? Sasa sisi kama serikali tulitaka shule hii ianze kazi ili muweze kupokea wanafunzi, lakini kwa hali hii tutarajie nini? Naagiza muandike maelezo kuja wizarni ili tujue sababu zilizosababisha yatokee haya,” anasema Silinde.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa watumishi ambaye naye aliomba kuhifadhiwa jina lake, anasema Wilaya ya Mbogwe inaonekana kukosekana kwa umoja na mshikamano kati ya viongozi wa chama na serikali, ambapo viongozi wamekuwa na hali ya kukamiana kwa lengo la kukomoana.

Akitolea mfano, mtumishi huyo mkongwe ndani ya serikari anasema Mbogwe kumekuwa na vijiwe vingi vya kahawa kwa ajili ya kujadili watu na kupanga mipango yao michafu na kupandikiza chuki kati ya wananchi, watendaji wa serikali na hata wale wa chama, hali ambayo ikiendelea hivi kupatikana kwa maendeleo ni ndoto. 

“Wapo watu wanatumia muda wao kupeleka malalamiko kwa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemas Maganga na yeye bila kufanya utafiti na kupata ushahidi anayafanyia kazi, hali hii ikiendelea hivi matarajio ya kuiona Mbogwe mpya tusiyatarajie zaidi ya kuona majungu yakishamiri,” anasema mtumishi huyo.

Katika Wilaya ya Mbogwe kumekuwa na sintofahamu kubwa kutokana na kukosekana kwa umoja na mshikamano baina ya viongozi, jambo ambalo linakwenda kuipasua Mbogwe vipande vipande kutokana na majungu yanayotengenezwa na baadhi ya wananchi, ambapo aliwashauri viongozi wa TAMISEMI kutafuta mwarobaini wa matatizo hayo ili kunusuru mpasuko mkubwa unaoweza kujitokeza.

Katika kikao cha majumuisho baada ya ziara ya Naibu Waziri Silinde, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbogwe, Deus Lyankando, alisimama na kuibua tuhuma nzito dhidi ya watumishi kadhaa wa Halmashuri ya Wilaya ya Mbogwe kuhusu upotevu mkubwa wa fedha za umma, huku akimpa nyaraka ambayo alidai kuwa ndiyo msingi wa tuhuma hizo. Hata hivyo alipoombwa nakala na mwandishi wa habari wa gazeti hili hakuwa tayari kumpatia.

“Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza mimi nimeshangazwa na Ripoti ya CAG kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe hati yenye mashaka, sijajua ni nini kilitokea na kusababisha kupewa hati yenye mashaka! Sisi tulistahili hati chafu,” anasema Lyakando. 

Hata hivyo sakata la tuhuma za upotevu wa fedha za umma unaodaiwa kufanywa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe licha ya kutotolewa kwa ushahidi liliungwa mkono na madiwani wengi wakidai kupotea Sh milioni 371 katika mashine za malipo (Pos).

“Fedha nyingi zimeliwa na wataalamu wa halmashauri na nikuambie hawa watumishi si waaminifu, Mheshimiwa Naibu Waziri tusaidieni muwaondoe hapa Mbogwe, kwani pamegeuka sehemu ya kujitafutia kipato kwa watumishi, sasa tunahitaji Mbogwe mpya,” anasema mmoja wa madiwani  hao.

Katika mwendelezo wa tuhuma za sakata la upotevu wa mamilioni ya fedha za umma, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbogwe, Nsika Sizya, anasisitiza kuwapo kwa upotevu wa fadha za mapato huku akilalamikia pia kuharibiwa kwa utaratibu wa vikao vya Kamati ya Fedha ambapo vikao hivyo havifanyiki ndani ya muda.

“Vikao vya Kamati ya Fedha vinatakiwa kukaa kila mwezi, lakini utaratibu wa vikao hivyo umekuwa ukiendeshwa kinyume cha utaratibu, hivyo tunakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri utusaidie kuhusu utaratibu ili vikao hivi viendeshwe kisheria, ili tuweze kwenda na kanuni kwa ustawi wa halmashauri yetu,” anasema Sizya. 

Akitolea ufafanuzi, Silinde ameagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kutokuwa kikwazo cha kufanyika kwa vikao hivyo ndani ya muda.

“Vikao hivi vipo kwa mujibu wa sheria, ninaomba viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kutokuwa kikwazo cha kufanyika kwa vikao hivyo ndani ya muda,” anasema Silinde.

Katika kutafuta ukweli wa tuhuma hizo dhidi ya watumishi wa halmashauri hiyo, JAMHURI liliwatafuta watumishi waliotuhumiwa mbele ya Silinde ili kuzungumzia tuhuma dhidi yao, ambapo walisema kuna chuki kubwa dhidi yao hasa wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao. 

“Kuna chuki kubwa dhidi ya watumishi, hasa tunapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yetu, wapo watu wanatengeneza majungu na kuyapeleka mpaka kwa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Nicodemas Maganga, lengo likiwa ni kutuchonganisha na viongozi wa kisiasa na kutuchafua sisi watumishi,” anasema mtumishi huyo.

Katika maelezo yao  watumishi hao wanasema wamefanya kazi kubwa ya kukusanya mapato ya serikali kama sheria na kanuni zinavyowaelekeza huku akisema tuhuma hizo hazina ukweli na wamesikitishwa na kitendo cha Naibu Waziri wa TAMISEMI kushindwa kutoa maelekezo ya kufanyika uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo ili kubaini ukweli. 

“Tunaomba TAMISEMI wafanyie uchunguzi tuhuma za madiwani hao,” anasema mmoja wa watumishi hao ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini.

Hata hivyo katika uchunguzi wake, JAMHURI lilipata takwimu za mwenendo wa ukusanyaji wa mapato kutoka kwa watendaji wa halmashauri kwa miezi miwili ya hivi karibuni kuonyesha namna watendaji hao walivyokusanya kodi, mrabaha, Service Levy pamoja na ushuru mbalimbali kama vyanzo vya mapato ya halmashauri ili kuonyesha namna madiwani hao walivyotuhumiwa kwa tuhuma ambazo ni za uongo kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.

Kwa mujibu wa taarifa hizo kwa kipindi cha mwezi Machi 2021, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ilikusanya jumla ya Sh 42,237,612.66 na kwa kipindi cha mwezi Aprili 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ilikusanya jumla ya Sh 30,324,872 ambapo fedha hizo zinatokana na mapato kutoka katika migodi iliyoko ndani ya halmashauri hiyo.

Katika madai yao mbele ya Silinde, madiwani hao waliwatuhumu watumishi hao kukusanya jumla ya Sh 7,000,000 kwa mwezi na baada ya kelele za madiwani hao mapato hayo yaliongezeka kufikia jumla ya Sh 14,000,000, ambapo hata hivyo yalikuwa chini. 

Hata hivyo watumishi hao wanasema kuwa tuhuma hizo si za kweli, bali ni chuki binafsi, ambapo mmoja wa watumishi wa halmashauri (jina tunalo), alikumbushia kuwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichokaa na kuhudhuriwa na Maganga na Mbunge  wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita, madiwani hao walimpongeza mkurugenzi wa halmashauri pamoja na timu ya wataalamu kwa kuvuka lengo katika ukusanyaji wa mapato, ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Mei  2021 halmashauri hiyo ilikusanya jumla ya Sh 909,721,407.62.

“Kama kikao kilichokaa kilitoa kauli ya kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na timu ya wataalamu wakiwamo wakusanyaji wa mapato kwa kuvuka lengo katika ukusanyaji wa mapato, kwa kukusanya jumla ya Sh 909,721,407.62 siku hiyo walikuwa wako katika mazingira gani? Au walikuwa wanaongea unafiki?” alihoji mtumishi huyo.

Aidha, watumishi hao wa serikali wamelalamikia kitendo cha kuwahusisha na migogoro yao ya kisiasa na kutafuta kura kwa ‘kuwapakazia’ tuhuma za namna hii, wakamuomba Waziri wa TAMISEMI kutuma tume huru ya wataalamu kufanyia uchunguzi tuhuma mbalimbali, zikiwamo za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za umma zilizotolewa dhidi yao na madiwani wa halmashauri hiyo.

671 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!