Majaliwa kauvae u-Sokoine

DAR ES SALAAM

Na Javius Byarushengo

 “Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani kuwa tutawalinda kwa vitendo vyao viovu.” – Sokoine, 26 Machi 1983

“Vijana leo wengi wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi miaka 30 hadi 40. Lakini wanaitaka serikali ndiyo iwaulize mali hiyo wameipata wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanae; ‘mali hii umeipata wapi?’” – Sokoine, 23 Oktoba 1983

“Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha kulinda haki na masilahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau masilahi ya walio wengi” – Sokoine, 1 Februari 1977

Hizo ni baadhi ya nukuu kutoka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Edward Moringe Sokoine, enzi za uhai wake.

Ikiwa imetimia miaka 37 tangu kifo chake Aprili 12, 1984 kutokana na ajali ya gari eneo la Dakawa, Morogoro akitokea Dodoma, kiongozi huyo ameendelea kukumbukwa, kuliliwa sana na Watanzania, hasa pale mambo yanapoonekana kulegalega au kwenda kombo. 

Alikuwa kiongozi asiye na mfano katika vita dhidi ya vitendo viovu, licha ya kuwa aliteuliwa kushika wadhifa huo ambapo nchi ya Tanzania ilikuwa katika kipindi kigumu sana kiuchumi.

Ni waziri mkuu aliyepambana kwa ujasiri mkubwa na kuhakikisha kuwa wahujumu uchumi, walanguzi, wapenda magendo, mafisadi, wala rushwa na watendaji wazembe wa serikili hawapumui kamwe.

Inasemekana katika mapambano hayo ya Sokoine dhidi ya wahujumu uchumi, watu  walificha bidhaa maporini na wengine kuzamisha ziwani, mitoni na baharini huku wakitamani ardhi ipasuke wazikwe wakiwa hai.

Ni kipindi ambacho waovu waliokuwa wakichezea mali za umma katika taifa lenye watu maskini, walijikuta wako magerezani wakijisaidia kwa kutumia mitondoo, kulalia milago huku wakinywa uji bila sukari na kula mlo mmoja.

Mali zote za umma zilizokuwa zimeibwa au kuhujumiwa kama si kutaifishwa, zilirudishwa kwa nguvu mikononi mwa serikali.

Mbali na hayati Sokoine kuanzisha vita dhidi ya uhujumu uchumi, biashara ya ulanguzi na magendo huku akiichukia rushwa kwa vitendo, lakini pia inasemekana alikuwa mtu wa vitendo kwa kila kitu na kamwe hakupenda kuwa mtu wa kulalamikalalamika.

Kutokana na mzalendo huyu kupatwa na mauti, Mwalimu Julius Nyerere alipomaliza tu kutangaza habari ya kifo chake, ilikuwa ni vilio na simanzi nchi nzima, huku Mwalimu akishindwa kujizuia kutoa machozi mbele ya waombelezaji katika siku ya kuuaga mwili wa Sokoine.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Kassim Majaliwa, Mei 28, 2021  ametangaza kuwasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili. 

Akiwa katika kikao kazi na Waziri wa Fedha na Mipango, Katibu Mkuu, manaibu katibu wakuu na watendaji waandamizi wa wizara hiyo mkoani Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salum Hamdun, kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikithibitika si za kweli watuhumiwa watarejeshwa  kazini.

 Tuhuma zilizotajwa na Mtendaji Mkuu huyo wa serikali ni malipo yaliyofanyika  Machi 31, 2021 kupitia vocha 30 ya Sh milioni 251, yakielezwa kuwa ni malipo maalumu, bila kutaja kazi maalumu ambayo haikueleweka ilifanywa na nani.

Fedha nyingine za wanyonge zilizotumika bila huruma ni Sh milioni 198.8 zilizolipwa kwa madai kuwa ni posho tu.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa aliendelea kusema kuwa Aprili 8, 2021 watumishi  27 wa wizara hiyo walilipwa  Sh milioni 44.5 za posho ya kazi maalumu ya wiki nne na Aprili 13, 2021 zililipwa Sh milioni 155.2  kwa watumishi 68, ikiwa ni posho ya kazi maalumu ya wiki tatu.

Pia Aprili 30, 2021 zililipwa Sh milioni 43.9 kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuhifadhi mazingira na siku hiyohiyo zililipwa Sh milioni 14.4 kwa ajili ya Siku ya Wanawake.

 Fedha nyingine Sh milioni 43 zililipwa siku hiyo na kufanya jumla ya malipo yaliyolipwa siku hiyo kuwa Sh milioni 101.8.

Sambamba na hilo, taarifa hiyo ya ubadhirifu ilieleza kuwa Mei Mosi, 2021 zililipwa Sh milioni 184.1  na mchana wa siku hiyo zikalipwa Sh milioni 264 zikiwa ni malipo ya kazi maalumu.

Waziri Mkuu kwa masikitiko makubwa  kutokana na fedha zilizolipwa Siku ya Wafanyakazi Duniani alisema: “Sisi tulikuwa Mwanza tunasherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani, nyinyi hapa ndani mnalipana posho.” 

Fedha nyingine zilizo na utatanishi ni Sh 146.5 zilizolipwa  Mei 3, 2021  kwa  watumishi 125, zikiwa ni malipo ya kuandaa mpango kazi wa manunuzi, kazi ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. Pia siku hiyohiyo zililipwa Sh milioni 171.2 kwa ajili ya kuandaa nyaraka za Bunge, huku Sh milioni 155  ikisemekana zililipwa kwa baadhi ya watumishi zikiwa ni posho ya kuandaa miongozo ya kazi.

Kimsingi ni kosa kisheria kuwaita watuhumiwa kuwa ni wahalifu hadi uchunguzi utakapofanyika na mahakama kuwatia hatiani.

Hata hivyo licha ya kuwa mahakama bado haijachukua mkondo wake, lakini kitendo cha hawa jamaa kutuhumiwa tu, kinatia hali fulani ya uhalali wa kutenda kosa hata kabla ya kutiwa hatiani.

Ni wazi kwamba vitendo hivi vya ubadhirifu wa mamilioni ya fedha vinatia uchungu na huzuni.

Vitendo hivi vinatia huzuni kwani vimefanywa na Watanzania wenzetu ambao wamepewa dhamana, huku wakiamua kudhulumu jasho la wanyonge na wanalipa kodi.

Vitendo hivi vya ubadhirifu vinatia huzuni, kwani vimefanywa na wasomi wa vyuo vikuu ambao wanachezea pesa wapendavyo huku wafanyakazi wa umma na binafsi wakiwa bado hawajapandishiwa mishahara takriban miaka sita.

Vitendo hivi vya ubadhirifu vinatia huzuni, kwani vimefanywa na Watanzania ambao miongoni mwao wanatokea vijijini ambako kuna wakulima wengi wanaoishi kwa maisha ya ‘kubangaiza’.

Je, ni nani anaweza kuondoa maombolezo na kuwafuta machozi wananchi ambao wanaanza kulia baada ya kupokea taarifa  kuwa kuna watu wachache wanaanza kukwapua mali na kuishi kama wako peponi ilhali wao wanaishi maisha ya kishetani?

Anayeweza kufuta machozi haya ni Waziri Mkuu Majaliwa.

Ni Kassim Majaliwa, kwa maana kwamba ndiye aliyemsaidia kwa karibu Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dk. John Magufuli, hivyo serikali hiyo kuonekana ya mfano katika mapambano dhidi ya vitendo viovu ikiwamo, rushwa, ufisadi, kujilimbikizia mali na uzembe.

Ni Kassim Majaliwa kwa maana kwamba kutokana na kuaminiwa na JPM katika kipindi chake cha  kwanza alimteua tena kuendelea na nafasi hiyo ya uwaziri mkuu katika kipindi chake cha  pili.

Ni Kassim Majaliwa ambaye ameaminiwa na Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, kuendelea na uwaziri mkuu.

Kwa watu wanaomjua kwa karibu, Kassim Majaliwa, wanasema kuwa hata katika Serikali ya Awamu Tano iliyopita, ilikuwa ni heri ukutane na Rais Magufuli kuliko Majaliwa, kwani hana simile na watenda uovu, japo ni msikivu mzuri.

Ni ukweli usiopingika kwamba kasi aliyonayo Majaliwa katika kupambana na vitendo viovu,  inawatia matumaimni wananchi, kwani wanaanza kuamini kuwa,  jinsi hayati Sokoine alivyomsaidia Mwalimu Nyerere ndivyo na Majaliwa  atamsaidia mama yetu mpendwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kupambana na wasaliti wetu kiuchumi, kisiasa na kijamii.

[email protected], 0756521119

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa