*Kaulimbiu ya Simba iliyowafikisha Robo Fainali
DAR ES SALAAM
Na Dk. Ahmad Sovu
Kaulimbiu ni misemo rahisi inayotumiwa zaidi na wanasiasa au asasi fulani kwa lengo la kujenga hamasa yenye madhumuni ya kufikia malengo fulani.
Makala hii madhumuni yake makuu ni kutaka kuonyesha namna Timu ya Simba ya Kariakoo, Dar es Salaam -Tanzania ilivyoweza kufikia hatua ya juu ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika pamoja na mambo mengine, lakini kwa umuhimu wa misemo au kaulimbiu mbalimbali.
Pamoja na kujizatiti kwa maandalizi mengine ya kuimarisha kikosi kama klabu ya mpira wa miguu, Simba pia walitumia kaulimbiu mbalimbali kwa lengo la kujenga morali na kuwatia shime wachezaji, viongozi na mashabiki ili kufikia malengo yao.
Hivyo basi, msingi wa makala hii mwega wake upo kwenye kaulimbiu, ninaweza kuiita kaulimbiu kuu ya ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’.
Uwanja wetu mkuu wa michezo umepewa jina la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa. Kwa hiyo kaulimbiu ya Simba ililenga kuonyesha kuwa mechi zote zitakazochezwa kwenye uwanja wa nyumbani hakuna timu itakayoshinda mchezo ndani ya dimba hilo. Yaani kwa Mkapa hatoki mtu. Wakimaanisha katika uwanja wa nyumbani Tanzania hatutafungwa na timu yoyote ile katika uwanja huo.
Ilianza kama mzaha, lakini hadi jana imethibitika kuwa kwa Mkapa hakutoka mtu.
Sasa Simba imetolewa kwenye mashindano hayo na timu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa ushindi mwembamba wa bao moja. Yaani 4 – 3.
Ufuatao ni uchambuzi wa kaulimbiu au misemo maarufu ya Simba ilivyoichagiza kaulimbiu kuu ya ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’.
Ingawa misemo hii iliyo mingi imebuniwa katika lugha ya Kiingereza rahisi. Kiingereza ambacho Watanzania wengi wanakifahamu maana yake.
Misemo hii ilichagizwa na mbwembwe, madoido, ukabobo, kujishongondoa, kujitanibu na hata kujifaragua kwa mnenaji wa timu hiyo, Haji Manara. Uwasilishaji wa Manara kwa misemo na kaulimbiu hizi ulisaidia sana kutamalaki kwake.
Ukiachilia mazonge au ukayeye wetu wa Usimba na Uyanga, Manara ninaweza kusema aliifanya kazi yake vilivyo. Sasa hebu tuidurusu baadhi ya misemo au kaulimbiu hizo:
Simba Next Level
Msemo huu una maana ya timu ya Simba ni ya kiwango kingine cha juu. Msemo huu ulilenga kuwajenga kisaikolojia wachezaji, viongozi wa Simba na hata mashabiki kuwa timu yao ni ya kiwango cha juu ukilinganisha pengine na timu nyingine za Tanzania.
Haya tuliyashuhudia hata pale ambapo mashabiki wa Simba wakihojiwa walikuwa wakitamba na kujimwambafai kuwa wao ni wa kiwango cha juu. Saikolojia katika msemo huu ulisaidia sana kuifanya timu ya Simba kujiamini na kusonga mbele katika kila hatua. Wachezaji walijiona wao ni timu kubwa na wanastahiki kuchukua ubingwa.
Do or Die
Kaulimbiu au msemo mwingine ulikuwa ni huu wa ‘Do or Die’ ukiwa na maana ya kufa au kupona. Kama kumbukumbu zangu ziko sawa, msemo huu ulichagizwa wakati wa mechi ya marudio baina ya Simba na timu ya AS Vita ya Congo. Kufa au kupona unaweza ukaona ni maneno machache na mepesi, lakini yalisaidia kuijenga saikolojia ya wachezaji wa Simba.
Kufa au kupona, yaani liwalo na liwe, ushindi ni lazima. Hii ni kauli inayoongeza ari ya kujituma kwa hali zote kuhakikisha ushindi unapatikana.
Kaulimbiu hii ilizaa matunda na kuifanya Simba kuendelea kujizolea alama katika hatua ya makundi. Msemo huu pia ulisikika ukitolewa na mashabiki wa Simba kuwa na wao walikuwa wakisema tu ni kufa au kupona leo.
War in Dar (WIDAR)
Msemo huu haukumaanisha vita ya vifaru, bunduki za SMG au AK 47 wala mabomu na kuua watu, la hasha! Ni vita ya kisoka, ni vita pira biriani, pira sambusa.
Msemo huu ulihanikiza mechi ya marudio kati ya Simba na Platinum. Nakumbuka Simba aliibuka na ushindi wa mabao manne katika Uwanja wa Mkapa. Ilikuwa vita kweli, wachezaji walijituma – wakapambana vilivyo na kuishinda vita ya kisoka. Msemo ‘War in Dar’ uliifanya Simba kubakia kileleni mwa kundi lake.
Total war point of no return
Kaulimbiu au msemo mwingine ulikuwa ni ‘Total war point of no return’. Msemo huu ulimaanisha vita kamili, kwa hatua hii hakuna kurudi nyuma.
Ama kwa hakika misemo hii ni muhimu sana, kwani huongeza siha na afya kwa wachezaji na wadau wote wa timu inayohusika.
Kuwaambia wachezaji sasa ni vita kamili na hakuna kurudi nyuma ni jambo linalowapa ukakamavu, uimara na linalotia nguvu kukabiliana na timu pinzani.
Katika hali hiyohiyo tulishuhudia vita kamili na Simba kuendelea kujinyakulia alama muhimu dhidi ya Al Ahly na kuzidi kusogea mbele zaidi katika mashindano hayo, ambapo Simba ilimaliza michezo yake katika hatua za makundi ikiwa kinara wa kundi lao.
Simba iliibuka ikiwa kinara katika kundi lake kwa alama 13 dhidi ya wababe kama Al Ahly ya Misri. Vita kamili waliyoinadi iliwafanya Simba wasirudi nyuma.
0713400079
Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni, Dar es Salaam.