Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ilikutana tarehe 28 Juni 2012 kujadili na kutathmini hali ya utendaji na utoaji wa huduma hivi sasa katika hospitali.

 

Imebainika kwamba utoaji huduma umeathirika kutokana na mgomo wa baadhi ya madaktari unaoendelea kwa takriban wiki moja sasa tangu ulipoanza Jumamosi ya tarehe 23 Juni 2012.

 

Baada ya tathmini hiyo, Bodi ya Wadhamini imeagiza yafuatayo:

 

(i)Madaktari waliopo kazini waendelee na kazi kama kawaida.

(ii) Madaktari waliogoma warejee kazini kutii amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kwa mujibu wa Kifungu Na. 76 (1) na (2) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004.

(iii) Madaktari waliopo likizo warejee kazini mara moja. Utaratibu wa kufidia likizo na nauli zao umeandaliwa.

(iv) Uongozi wa Hospitali uwachukulie hatua za kinidhamu wafanyakazi wote watakaoendelea kutokuhudhuria kazini na kufanya kazi bila sababu za msingi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za kazi.

(v) Uongozi wa Hospitali ufute mara moja ‘rotations’ za madaktari waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo (interns); na

(vi) Uongozi wa Hospitali uwapange (re-deploy) madaktari na madaktari bingwa waliopo kwenye maeneo yaliyoathirika wakati huu wa mgomo.

 

Aidha, Bodi ya Wadhamini inawashukuru sana madaktari na wafanyakazi wote ambao wameendelea kuwahudumia wagonjwa wetu na wananchi kwa ujumla. Vilevile, Bodi ya Wadhamini inawasihi madaktari na wafanyakazi wote wawe na subira na waheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo pamoja na maadili ya taaluma zao.

 

Dkt. Gabriel Upunda


KAIMU MWENYEKITI

BODI YA WADHAMINI

 

 

By Jamhuri