Wiki iliyopita Tume ya Marekebisho ya Katiba ilitangaza rasimu ya kwanza. Rasimu hii ina kila sababu ya kusifiwa. Nilipata fursa ya kuwakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kuchambua na kuwasilisha mapendekezo ya tasnia ya habari nchini. Kwa ufupi nasema, asanteni wajumbe wa Tume kwa kusikiliza kilio cha Wanahabari.

Katika mapendekezo yetu kama Jukwaa tuliomba ibara tatu za msingi kwenye Katiba mpya. Tuliomba ibara maalum kwa ajili ya Uhuru wa Kutoa Mawazo. Tukaomba ibara kwa ajili ya Haki ya Kupata Habari na Ibara ya mwisho tukaomba Uhuru wa Vyombo vya Habari.

 

Rasimu hii imetoa Uhuru wa Maoni (Freedom of Expression) chini ya Ibara ya 29 ya Katiba tarajiwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara hii ilikuwapo au ipo kwenye Katiba ya sasa chini ya Ibara ya 18. Hata hivyo, ibara hii ilikuwa na upungufu na wakati nawasilisha maoni ya Jukwaa la Wahariri nilipendekeza iwe na sehemu ya pili ambayo ni kuzuia uchochezi, ubaguzi na mifarakano katika jamii. Nashukuru wameongeza vipengele hivyo na vingine.

 

Ibara ya 30 rasimu inapendekeza isomeke hivi: “Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari.” Hiki ndicho tulichoomba. Naishukuru Tume kwa kusikiliza kilio cha wanahabari  nchini imeandika historia. Haijapata kuwapo tangu nchi hii imepata uhuru Katiba yetu kutambua Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari.

 

Sitanii, mpaka hapo sina ugomvi na Tume, isipokuwa sehemu ndogo ya 4 ya Ibara ya 30 ndio sifurahishwi nayo na naamini wanahabari hawafurahishwi nayo, hivyo kupitia kwenye mabaraza tutapaswa kupendekeza irekebishwe. Kimsingi sheria inapaswa kuweka utaratibu wa jinsi haki inayotolewa na Katiba itakavyopatikana, lakini hapa kwa bahati mbaya, ibara hii inaipa nguvu kubwa sheria itakayotungwa kuliko Katiba.

 

Ibara ndogo ninayoipinga kwenye rasimu inasomeka hivi: 30 (4) “Masharti ya Ibara hii YATALAZIMIKA KUZINGIATIA masharti ya sheria ya nchi itakayotungwa kwa ajili hiyo na kwa madhumuni ya kulinda usalama wa Taifa, amani, maadili ya umma, haki staha na uhuru wa watu wengine.” Hii inaleta ukakasi. Inamaanisha sheria hiyo itakuwana nguvu kuliko Katiba. Nitalijadili kwa kina hili kwenye makala maalum.

 

Leo nasema mimefurahishwa na uamuzi wa rasimu kutangaza ujio wa Serikali ya Tanganyika. Hili lilikuwa wazi, ila kilichokuwa kinasubiriwa ni wakati tu. CCM katika hili nadhani nao watakuwa waungwana na kusoma upepo, kisha wakubali kuwa katika mchezo kuna kushinda na kushindwa.

 

Sitanii, nazifahamu changamoto zinazoambatana na serikali tatu. Na hapa leo nitataja mbili tu za msingi. Moja ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na pili ni suala la Ardhi. Takukuru muda wote wamekuwa chini ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora). Ninaamini wamefanya kazi nzuri. Wameweza kuwafikisha mahakamani watu wazito na wenye uwezo mkubwa.

 

Wamewafikisa  mahakamani wafanyabiashara wenye fedha kama njugu, lakini leo Takukuru inavunjwa na rasimu hii. Rasimu hii inaiweka kazi ya Takukuru chini ya polisi. Eti wanataka polisi wafanye kazi ya chunguza rushwa nchini. Rasimu inawapa madaraka chini ya ibara ya 228 (d) “Kuzuia Rushwa na Ufisadi.” Hapa ndipo walipoihamishia Takukuru.

Sitanii, katika hili napingana na Tume ya Jaji Warioba. Jaji Warioba mwaka 1996 alitoa ripoti iliyotikisa taifa hili kuhusu masuala ya rushwa. Nilitarajia angeipa Takukuru kipaumbele. Siwasemi vibaya, ila polisi wetu wanaongoza kwa kuthumiwa. Wanatuhumiwa kila kona. Tena wengine wanachukua hadi rushwa ya Sh 2,000 kwa tuhuma zilizopo.

 

Leo walau Takukuru kilikuwa chombo pekee kinachowaogopesha polisi na manazi wengine. Kazi ya kuchunguza rushwa kuiweka mikononi mwa polisi ni hatari kuliko kufuga mamba ukalala naye kitanda kimoja. Najua wapo wakubwa wanaofurahia kifo cha Takukuru. Takukuru muda wote wamekuwa na kilio cha kuendesha mashtaka wenyewe.

 

Mara kadhaa wamesema kuwa wanachunguza kesi zenye ushahidi wa wazi zinafia mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP). Leo Takukuru imewakera wakubwa hawa, wanaamua kuizika rasmi. Nasema hili hapana. Takukuru irejeshwe ofisi zake zilizojengwa kila wilaya zifanye kazi. Kuifuta Takukuru kwa sababu yoyote iwayo tutaithibitishia dunia kuwa sisi tuna mapenzi ya wazi ya rushwa.

 

Tanzania imetia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Rushwa wa Mwaka 2004 na ule wa Afrika wa mwaka 2003 uliotiwa saini mjini Maputo, unazitaka Serikali za nchi zote duniani kuwa na chombo cha kitaifa cha kudhibiti rushwa. Zanzibar na Tanganyika hazina mamlaka ya kidola, hivyo rushwa haiwezi kuachwa chini yao. Hili nalo nitaliandikia makala maalum.

 

Sitanii, nafasi inazidi kuwa finyu kwa kiwango kinachonikosesha raha. Ila usihofu si muda tutaongeza kurasa na kuwa kurasa 20, kama si Jumanne ijayo, basi inayofuata. Nitaijadili kwa kina rasimu hii. Nitajadili kwa kurejea kwa Tanganyika. Sitakubali iitwe Tanzania Bara. Tanzania ni muunganiko wa majina Tanganyika na Zanzibar. Kuitwa Tanzania Bara, maana yake nchi hii itakuwa inaitwa Tanganyika-Zanzibar-Bara.

 

Hii haikubaliki. Hatuna sababu ya kuona aibu kuitamka Tanganyika, ila ninalo angalizo. Ardhi ya Tanganyika ilikuwa ikimilikiwa na Wazanzibari kupitia Rais wa Tanganyika aliyekuwa anashikilia nafasi ya Muungano. Hujanielewa namaanisha nini? Rais wa Muungano kwa maana nyingine ndiye aliyekuwa Rais wa Tanganyika.

 

Zanzibar kuna Rais wa Zanzibar ambaye ni mdhamini wa ardhi ya Zanzibar, hivyo Tanganyika sasa itapata Rais wake ambaye atakuwa mdhamini wa ardhi ya Tanganyika. Kwa maana nyingine, itapaswa kutungwa sheria ya ardhi ya Tanganyika kufuta sheria No 4 na 5 za mwaka 1999 zinazoitambua ardhi kama mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sheria ya ardhi ya Zanzibar hairuhusu mtu asiye Mzanzibari kumiliki ardhi Zanzibar, inawezekana hata Sheria ya ardhi ya Tanganyika ikazuia mtu asiye Mtanganyika kumiliki ardhi Tanganyika isipokuwa kwa utaratibu wa kupitia Kituo cha Uwekezaji. Je, Wazanzibari waliojenga Tanganyika na Watanganyika waliojenga Zanzibar itakuwaje? Usiikose Sitaanii katika toleo la Jumanne ijayo.

 

By Jamhuri