Wanangu, nianze kwa kuwashukuru kwa kuwa pamoja katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba mpya ya nchi yetu. Naiita katiba mpya kwa kuwa hatujawahi kuifuta tuliyonayo sasa isipokuwa tulikuwa tunaijazia viraka vya hapa na pale ili kufukia mashimo.

Nauita mchakato kwa kuwa tunalazimika kuachana na hii tuliyonayo na kuingia katika ulimwengu mpya wa sheria za nchi, inaweza ikawa bora mpya na wakati huo huo inaweza ikawa bora hii tunayoisigina sasa kwa kutoa mawazo yetu ya kuirekebisha.

 

Yote nakubaliana nayo kwa kuwa anayepinga wengi atakuwa mchawi na mimi sitaki kuwa mchawi, katika hili nimekuwa bendera fuata upepo, litakaloamuriwa na wengi wape ndiyo demokrasia inavyosema na nchi yetu ni ya kidemokrasia.

 

Wiki jana nilitoa mapendekezo yangu juu ya mabadiliko yanayosemwa katika rasimu mpya ya katiba, nilikuwa na maswali machache ambayo nilikuwa najiuliza ikiwa ni pamoja na je, taifa hili maskini linaweza kuhimili kishindo cha kuwahudumia viongozi waandamizi zaidi ya watatu?

 

Hilo lilikuwa ni moja kati ya maswali mengi niliyojiuliza, lakini kama mwananchi mwingine nina haki ya kutoa maoni yangu kwa faida ya taifa langu, na hii inatokana na ukweli kwamba  nchi yetu bado ni maskini, hivyo bado napata mashaka katika kuweza kumudu serikali tatu na viongozi waandamizi wake.

 

Maana kwa uelewa wangu ukiwa na serikali tatu itaambatana na watumishi wa serikali hizo na kutakuwa na mgawanyo wa madaraka, vile vile katika  uamuzi inaweza ikaleta mparaganyiko wa sitoelewa, kwa kuwa kila mmoja atavutia upande wake kwa manufaa ya upande wake, hivyo itakuwa vigumu kutoa uamuzi ulio sahihi.

 

Huo ni mtazamo mmoja na hasi, kama Mzee Zuzu nina mitazamo mingi zaidi ya hiyo ya viongozi, eti nimesikia katika mapendekezo hayo kuwa sasa Muungano tunataka uwe wa ndoa ya mkataba, yaani ndoa zile za talaka rejea.

 

Jambo kubwa lililopo hapa ni hatima ya Muungano ulioasisiwa na viongozi wetu kwa nia nzuri, kila mtu anatoa maoni yake kwa mtazamo wake, mimi nadhani bado hata hao wazee wetu walikuwa na kigugumizi cha kuamua aina ya muungano walioutaka, yawezekana ni kutokana na shinikizo kutoka kwa wananchi.

 

Wakati ule Julius angeniuliza tufanye muungano gani basi ningemwambia uwe muungano wa moja kwa moja, yaani kuwa na taifa moja la Tanzania, Zanzibar ingekufa kifo cha Tanganyika, kusingekuwa na jopo la viongozi Zanzibar kama ilivyokuwa kwa Tanganyika. Tulipaswa kuwa na rais mmoja na viongozi wachache wa mikoa kama ilivyo Tanzania Bara.

 

Kwangu ndoa hii ya muungano siikubali vyovyote, bado ni muungano batili na ndiyo maana kuna kero nyingi za Muungano. Kwa mtazamo wangu naona upendeleo mkubwa unafanywa kwa upande wa pili – Visiwani.

 

Sioni sababu ya msingi kwa Zanzibar kuwa na viongozi kama Tanzania, ikiwa na viongozi na tuseme huo ni muungano, na wala hainijii akilini kwa Zanzibar wadai kuwa na wimbo wao wa taifa, utambuzi wa taifa huru katika mikutano mbalimbali ya kitaifa wakati viongozi wa Tanzania ndiyo walewale wa Zanzibar!

 

Kitendo cha Watanganyika kutolisemea au kulibakia kimya jambo hili ni woga wa kutovunja Muungano, na kitendo cha Wazanzibari kudai viongozi wa Zanzibar wawe na madaraka ya kitaifa kwangu mimi ni makosa katika Muungano. Tulipaswa kutoangalia kiongozi anatoka wapi. Iwe Zanzibar au Tanganyika yote heri ilimradi awe kiongozi wa Tanzania.

 

Katika mabadiliko haya ya katiba ningeomba kuishauri Tume ya Warioba kufutilia mbali wazo la serikali mbili na hilo la serikali tatu, iwe Serikali moja ya Muungano, rais awe mmoja, waziri mkuu awe mmoja, spika awe mmoja, mkuu wa majeshi awe mmoja, mwanasheria mkuu awe mmoja na ikiwezekana hata taasisi nyingine kama za dini kuwa na shehe mkuu mmoja na askofu mmoja, huo ndiyo muungano.

 

Kwa lugha nyingine naomba nipingane hata na wazo la chama tawala la kutaka kuwa na serikali mbili, ni gharama kubwa kuiendesha serikali kubwa, na kimsingi walioko madarakani hawawezi kuziona gharama hizo kwa kuwa ndiyo wanaonufaika na mapato yanayoingizwa na taifa hili maskini.

 

Hili ni wazo la kizamani kidogo kutoka kwa mtu wa zamani, iwapo nimekosea ni suala la demokrasia, mimi siamini kama maendeleo yanaweza kuletwa na utitiri wa viongozi. Wenzetu wa mataifa makubwa kama Marekani wameweza kuunganisha majimbo yao na wakawa na rais mmoja ambaye analeta maendeleo, suala la maendeleo ni dhamira ya viongozi na wananchi si wingi wa viongozi.

 

Hili ni wazo langu tu na ninatoa ushauri kama Mtanzania.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu

Kipatimo

Please follow and like us:
Pin Share