Kocha Msaidizi wa Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Dar es Salaam, Jumhuri Kiwelu ‘Julio’ amesema kuwa kuwapo kwa Kocha Mkuu mzawa katika timu hiyo, King Abdallah Kibadeni ‘Mputa’,  kutaiwezesha kufanya vizuri katika michuano ijao.

Akizungumza na JAMHURI mwisho mwa wiki, Julio amesema Kibadeni ni kocha mzuri na mwenye uzoefu wa hali ya juu na mpenda mafanikio, hivyo atafanya kazi nzuri Simba.

 

“Sikiliza, hapa tumekaa maprofeshno (professionals)wazawa watupu, ni kama ukichukua moto ukaongeza moto mwingine unapata moto mkubwa, hivyo ndivyo tutakavyofanya kazi na Kibadeni,” amesema Julio.

 

Amesema kukubaliwa kuifundisha Simba ni kutaka kufuta kasumba iliyojaa katika akili ya Watanzania ya kuwaamini mno makocha wa kigeni kuwa ndiyo wanaofaa kufundisha mpira katika timu za hapa nchini.

 

Amekanusha kuwa hilo si jambo la kweli hata kidogo, bali Watanzania wanatakiwa kubadilika na kuwaamini makocha wazawa kuwa ndiyo wanaoweza kufanya maajabu katika soka la Tanzania kwa sasa.

 

Kwa vile King Mputa aliwahi kuifundisha na kuipatia mafanikio makubwa klabu hiyo ya Msimbazi, sasa Simba itarajie kuvuna mafaniko mengine zaidi.

 

“Lazima tubadilike…tusiangalie sheria ya zamani ya kwamba ukiwa penye traffic light (taa za kuongozea magari), ukarudi nyuma ukaligonga kwa nyuma gari lililo nyuma yako, basi wewe uliyogongwa kwa kuwa uko nyuma basi unakuwa na makosa, hii si sawa. Tunatakiwa kubadilika katika soka la Bongo tusiwe kama sheria hii.

 

“Mimi mwenyewe kama mzawa ni mtu wa mafanikio, nimeifunga Yanga zaidi ya mara sita nikiwa na Simba na sasa niko na King Kibadeni tena, ninajisikia furaha na tutafanya vizuri, tutafanya maajabu katika Ligi Kuu ya Vodacom ijayo,” amesema Julio.

 

Akizungumzia kushindwa kwa Simba kutetea taji lake, Julio amesema kuwa Simba haikujipanga vizuri wakati mahasimu wao – Dar es Salaam Young Africans (Yanga) wenye makazi yao mitaa ya Jangwani na Twiga, walijipanga vyema na kumudu kuukwaa mchuma ule.

 

“Kaka kama ni mfuatiliaji mzuri wa michezo hapa nchini, utaona kuwa miaka ya nyuma Timu ya Taifa ya Brazil ilikuwa ni nzuri  sana, na ilishika nafasi ya kwanza katika viwango vya ubora zinavyotambuliwa na Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA), lakini kwa sasa imeshuka na kufika hadi nafasi ya 29 kwa viwango vya Ubora wa Soka Duniani.

 

“Sasa si kwamba viwango vya soka duniani vimeshuka la hasha, bali ni timu nyingine zimejipanga vizuri na kufanya vizuri zaidi ya Brazil, vivyo hivyo nasi Simba tunajipanga kurudisha heshima Msimbazi,” amesema Julio.

 

Kujipanga kunaanzia katika usajili wa wachezaji. Vivyo hivyo, Simba iko katika mkakati wa kusajili wachezaji wazuri wenye nia ya kuichezea Simba katika Kombe la Kagame, iwapo Serikali itaruhusu kushiriki Kombe hilo, kutokana na usalama kuwa hafifu katika eneo ya Darfur kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

 

Kocha Abdallah Kibadeni ana historia ya aina yake, ikiwamo ya kuwamo kikosi bora cha Afrika mwaka 1973, kabla ya kumpisha Maulid Dilunga aliyekuwa mhusika halisi.

 

Kibadeni alikuwamo pia kwenye kikosi cha kihistoria cha Simba kilichoifunga Yanga mabao 6-0, Julai 19, 1977.

 

Katika mechi hiyo, Kibadeni alifunga mabao matatu, katika dakika ya 10, 42 na 89; matatu mengine yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ (mawili – dk. 60 na 73) na Selemani Sanga (dakika ya 20).

Rekodi  hiyo ya Kibadeni ya kuifunga Yanga mabao matatu haijavunjwa wala kufikiwa na mchezaji mwingine yeyote kati ya wachezaji wa timu hizo mbili.

 

Kama vile haitoshi, mwaka 1993 aliiongoza Simba kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast. Hata hivyo, Simba waliangukia pua na kushindwa kuutwaa ubingwa, baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 nyumbani Dar es Salaam huku wakilazimisha sare ya 0-0 mechi ya marudiano.

 

Kibadeni ndiye kocha wa kwanza wa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 almaaruf Serengeti Boys, iliyowahi kupata tiketi ya kucheza fainali za Afrika mwaka 2005 nchini Gambia.

 

Kama si utata wa umri wa mchezaji Nurdin Bakar, Kibadeni angekuwa ameweka rekodi, kwani Tanzania iliikwaa tiketi lakini ilitolewa kutokana na tatizo hilo.

 

Kibadeni pia ni kocha mwenye uwezo mkubwa anayelifahamu vyema soka la Tanzania.

 

Please follow and like us:
Pin Share