Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani Kagera, Johnny Kalupale, anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha pamoja na unyanyasaji wa watumishi walioko chini yake mkoani humo.

Meneja huyu anatuhumiwa kuweka sawa vitabu vya hesabu kabla ya kufanyiwa ukaguzi wa matumizi ya fedha na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa  Hesabu wa Serikali (CAG). Anatuhumiwa kuwapeleka wakaguzi mpakani mwa Uganda na Tanzania (Mutukula) kuwafanyia ununuzi ya vitu mbalimbali.

 

Shutuma nyingine ni kuwa kiongozi huyu anafanya kazi na mke wake katika ofisi yake, ambapo mke wake ni mtunza fedha (cashier), na kwamba amekuwa akishirikiana kwa karibu kufanya uamuzi mkubwa bila kushirikisha vikao halali.

Pia Kalupale anadaiwa kubadili taratibu katika kitengo cha ununuzi, ambapo wakuu wa Kitengo cha Mipango wamegeuka wasimamizi wa miradi kwa manufaa yake.

“Hawa wanafanya haya yote kwa manufaa ya Meneja. Wamegeuka kama watoza ushuru wa asilimia 5 yaani wapokea rushwa za Meneja. Mtu anayepaswa kusimamia miradi ni Engineer au Head of Engineering. Huyu Meneja anafanya kinyume cha mfumo wa utumishi uliowekwa na TANROADS (Marginalization of hierarchy),” anatuhumu mtoa habari.


Tuhuma nyingine ni mgawanyo wa majukumu ya kazi ambayo inadaiwa kuwa hayafanyiki kulingana na mkataba wa mfanyakazi husika, na kwamba watu hawafanyi kazi kama timu.


Baada ya tuhuma hizi, JAMHURI kwa nia ya kupata uchambuzi wa kina, imewasiliana na Kalupale kupata neno lake. Kalupale amepangua shutuma moja baada ya nyingine kwa kuzingatia vipengele kadhaa vya mikataba ya wafanyakazi. Ametaka wafanyakazi wenye malalamiko kufuata taratibu za kuwasilisha matatizo kama hayo, wanapoona wanaonewa na viongozi wao mahala pa kazi.

Majibu ya Kalupale

Kalupale anasema yeye kama kiongozi anayefuata maadili ya kazi, haoni haja ya kumnyanyasa mfanyakazi ambaye yuko chini yake zaidi ya kutimiza wajibu wake.


“Wanaolalamika kunyanyswa ni wale tu ambao hawataki kukosolewa na hasa pale wanaposhindwa kutimiza  wajibu wao, ikiwa ni pamoja na kukumbushana kuwahi kazini, kuzuiwa kusafiri nje ya kituo bila idhini ya Meneja na kuwakemea ile tabia ya utumiaji wa kofia ya Meneja kwa faida na nia binafsi.” anasema Kalupale.


“Hakuna  wizi wowote wa fedha, ni uzushi, kama  wana ushahidi wanaweza kuutoa. Kwa mfumo wa upokeaji na matumizi ya fedha, uhakiki na ukaguzi sioni namna wizi huo unavyoweza kutokea bila kugundulika,” anasema.


Anasisitiza kuwa hayo ni majungu kwa nia ya kuchafua jina la ofisi na uongozi uliopo kwa sababu wanazozielewa watoa habari. Amekuwa na utaratibu wa kuwabana, kuhoji taarifa mbalimbali za usimamizi wa kazi na vipimo vya utekelezaji, hivyo kuna kundi linaloona hatua hiyo ni kero kwao kufikia hatua ya kuupaka tope uongozi bila sababu za msingi.


Anasema kuingiza kwenye majungu ofisi ya CAG ni mbinu mgando za kuuondoa uongozi ulio makini na shughuli zake.  Anasema  wakaguzi wa nje wanafanya kazi kwa weledi na umakini mkubwa na kuongeza kuwa wakaguzi huhudumiwa vizuri na ofisi yao na mafao yao pia yameboreka.


“Kusema kwamba wanapewa vishawishi vya kufanya shopping Mutukula na Kampala  si kweli. Wakaguzi hupitia nyaraka za miradi, stoo na fedha, kisha huenda katika maeneo ya kazi (site) ili kuwianisha na nyaraka.


“Pia hupitia taratibu zote za manunuzi. Huhitaji ufafanuzi na kuibua hoja mbalimbali kwa kuhitaji vielelezo kwa ajili ya kuhakiki majibu. Hutoa maelekezo na maoni ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi zetu na matumizi ya fedha za umma zinazotolewa.


“Aidha, kwa mtazamo huo wangekuwa wanapewa hongo wangeibua hoja kweli? Hata kama wanasema mafaili yamewekwa sawa, je, kule katika maeneo ya kazi (site) wanakolazimika kuwianisha na nyaraka inakuwaje?” anahoji Kalupale


Kwa mujibu wa Kalupale, Kitengo cha uhasibu kina Mhasibu ambaye ni Mkuu wa Kitengo, chini yake kuna Mhasibu Msaidizi, ambaye pia ndiye Cashier na huyo si mke wake.


Alifafanua kuwa mke wake ni Karani wa hesabu na kuongezea kuwa hayuko katika nafasi yoyote ya kufanya uamuzi. Kwa mujibu wa Kalupale nafasi aliyonayo mke wake ya ukarani wa hesabu, haiwezi kumpa nafasi ya kuwa Kaimu wa Meneja.

 

“Huko nyuma Waziri wa Nchi Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara, walishawahi kulitolea ufafanuzi  suala hili.  Meneja kufanya kazi katika idara moja na mke wake sioni kama lina shida na hasa kama taratibu za kazi zinafuatwa na kuzingatiwa pale ambapo mmoja wao hayuko katika nafasi ya maamuzi,” anafafanua.

Anasema mkuu wa kitengo cha Mipango ni Mhandisi. Kwa hiyo kuwa msimamizi wa baadhi ya miradi ya matengenezo  ni jambo la kawaida na ni sahihi kama ilivyo kwa Mhandisi yeyote kwenye ofisi ya TANROADS.

“Haya yameoneshwa  kwenye kabrasha la mkataba wa kandarasi husika kwa uwazi, ili kuwa na usimamizi wa kutosha kuleta tija na ufanisi kwa manufaa ya Taifa na si vinginevyo,” anafafanua.

Anasema suala la kusema mtu anayestahili kusimamia miradi ni Mhandisi wa Matengenezo na Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo, zimeibuliwa na mtu ambaye aidha hajui TANROADS inafanyaje kazi zake, na kama anajua basi analalamika kwa makusudi kutetea Kitengo cha Matengenezo kwa ajili ya kupotosha kwa makusudi ukweli kwa maslahi binafsi, au kikundi kisichokuwa na nia njema na Wakala ili kutaka kufanya kazi kwa mazoea.


Mfumo wa utumishi wa TANROADS Mkoa  uko wazi, haujakiukwa na hakuna ambaye yuko juu ya Meneja wa Mkoa, chini ya Meneja kuna wakuu wa vitengo vinne ambao wote wanawajibika kwa Meneja wa Mkoa, vitengo hivyo ni: Kitengo cha Uhasibu na Utawala, Kitengo cha Matengenezo, Kitengo cha Mipango na Kitengo cha Manunuzi, anasema.


“Hawa walalamikaji wanaojidai kufahamu jinsi TANROADS Mkoa  inavyostahili kutenda kazi zake, basi hawajui hata chembe. Ni upotoshaji wa hali ya juu mfumo wa utumishi uko wazi na ndiyo unaofuatwa na siyo kama wao wasemavyo,” analisema.


“Kwenye maelezo hayo hayo kuna kipengele kinachosema kuwa pamoja na mtiririko wa majukumu yao  makuu bado watapangiwa kazi nyingine na Meneja wa Mkoa kadiri atakavyoona inafaa kwa ajili ya kuleta tija na ufanisi,” anafafanua.


Tatizo kubwa analoliona ni kwamba kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wamefanya kazi mkoani hapo kwa zaidi ya miaka 10, na kuongezea kwamba wamekuwa kama kikwazo pale wanapoona uongozi unafanya kazi kwa kuzingatia haki na kuziba mianya ya uzembe kazini.

“Nafikiri nahitaji kukaa na mkuu wangu wa kazi kumshauri juu ya kuangalia namna ya kutatua tatizo hili, na hasa ninachokiona hapa ni kwamba watu wamefanya kazi muda mrefu na sasa utendaji wao umekuwa wa mazoea. Nafikiri wanahitaji kufanyiwa taratibu nyingine ili kuboresha utendaji wao wa kazi utakaowasaidia kuachana na majungu,” anasema.

0783 106 700


1841 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!