Sababu za kupungua nguvu za kiume -3

Homoni ya kiume iitwayo testestorone, ambayo hutolewa na korodani husimamia kazi ya uume kama vile kuleta msisimko, hamu ya tendo la ndoa, kuchelewa kufika kileleni kiasi cha kufurahia tendo la ndoa.

Misuli iitwayo pubococcygeus [kwa kifupi PC muscles] ni misuli iliyokaa kama kitanda cha bembea, ipo kwa wanawake na wanaume, huanzia kwenye mfupa wa kinena hadi kwenye mkia wa mfupa wa uti wa mgongo na husaidia kubeba vitu vilivyo katika nyonga. Misuli hii hudhibiti mkojo na shahawa.

Baada ya kuona namna baadhi ya viungo vya tendo la ndoa na vitu vingine vinavyosaidia, sasa tutazame jinsi uume unavyosimika (unavyosimama).

Tuanze na msisimko wa akili. Licha ya kuwa ni uume ambao husimama, mchakato wa usimamaji wa uume huanza kuratibiwa katika ubongo. Ikoje? Iko hivi: Unapomwona mwanamke kwa matamanio, au kumuwaza, au kumgusa, mishipa ya neva hupeleka habari kwenye ubongo. Aina ya neva hizi zinazopeleka taarifa kwenye ubongo huitwa neva hisishi [sensory nerves]. Hivyo, kusimama kwa uume huanzia kwenye fahamu au msisimko wa akili au vyote viwili.

Taarifa (au habari) hupelekwa kwenye ubongo kwamba baadhi ya aina ya msisimko unatokea na kwamba uume unatakiwa kutanuka.

Neva katika ubongo hupeleka taarifa kwenye eneo la chini ya uti wa mgongo. Neva za uti wa mgongo hupeleka habari kwenye neva zilizo katika eneo la nyonga ambalo hupeleka taarifa kwenda kwenye neva zilizo katika uume. Hapo sasa neva za kwenye uume huziambia mishipa ya damu ambayo husambaza damu kwenye uume ifunguke.

Kemikali muhimu iitwayo “nitric oxide” inayokaa kwenye kuta za damu ndiyo hubeba jukumu hili la kuitanua mishipa ya damu  na hapo damu hutiririka kwenye uume na kujaa kama puto.  Utendaji wa kazi wa vali karibu na sehemu ya awali ya uume huzuia damu kutoka nje tena; walau hadi tendo la ndoa likamilike.

Wakati uume unapopokea taarifa kutoka katika ubongo kama tulivyoona, misuli laini iliyo katika uume huanza kutanuka ili kuruhusu damu kuingia ndani.  Polepole damu huingia na kuijaza corpora cavernosa ikisababisha uume kuwa mgumu, imara na madhubuti. Nimekwishaeleza kuwa Corpora cavernosa ni mirija miwili ya sponji iliyo ndani ya uume ambayo damu huingia ndani yake wakati wa msisimko wa mapenzi ili kufanya uume usimame.

 

Utando uliozunguka Corpora cavernosa unaoitwa kitaalamu Tunica albuginea husaidia kunasa damu ndani ya Corpora cavernosa na kuzuia damu kurudi nje. Hali hii husababisha uume kusimama. Hivyo, kusimama (kusimika) kwa uume hutokea damu inaposukumwa katika uume na kukaa humo uumeni. Damu hiyo hufanya uume kuwa mgumu, imara na madhubuti.

 

Uume unapoanza kujaa damu, na damu inapokuwa inatembea kwenda sehemu mbalimbali za mwili, midomo, chuchu husimama; ndewe na viungo vingine vya uzazi hujaa zaidi na kuwa na hisia zaidi. Mfuko wa korodani pia huanza kunenepa ukizivuta korodani na kuzifanya zikaribiane hadi katika mwili.

Vitu muhimu zaidi vinavyosaidia msisimko wa uume wakati wa kupeana ashki kabla ya tendo la ndoa (foreplay) pia ni hisia iliyo katika ngozi ya uume na kichwa cha uume.

Sehemu hizi kila moja ina hisia yake na kila moja huchangia kwa njia ya msisimko wa tendo la ndoa. Ngozi ya mbele ina tabaka la ndani na nje. Tabaka la nje lina miishilio ambayo huitika mshiko wa taratibu wakati wa mwanzo wa msisimko wa mapenzi.  Neva za ndani na nje ya ngozi ya mbele huchangia msisimko wa uume na ufikaji kileleni.

Wakati msisimko ukiendelea, uume huwa mgumu na imara, unaweza kuwa na rangi nyeusi zaidi na maji ya shahawa huanza kupenya. Katika hali ya kupeana ashki  (kuchezeana) na mwanandoa kwa muda mrefu, uume unaweza kuwa tepetepe (kulegea) na kuwa imara tena. Hii ni hali ya kawaida, siyo tatizo. Hata kama uume utaendelea kusimama kwa uimara kwa muda mrefu, unaweza kulegea kidogo kwa kiwango fulani.

Mfuko wa korodani huendelea kujaa na korodani huwa kubwa. Korodani ya kulia itainuka na itazunguka kwanza kidogo, kisha ya kushoto itafanya hivyo hivyo. Mapigo ya moyo na msukumo wa damu utaongezeka, na kuiva kwa ngozi (kutokana na msisimko) kunaweza kuonekana juu ya kifua, shingo au uso. Upumuaji na mapigo ya moyo huongezeka na kupiga kite au aina nyingine ya sauti inaweza kutokea.

Kama utajiona jinsi na namna kila kiungo cha mwili wako kinavyofanya kazi wakati wa tendo la ndoa, utauona moyo wako unadunda kama nyundo inavyogonga mawe haraka haraka! Utaziona neva zikirukaruka kwenye ngozi mithili ya wanamuziki waliorukwa na akili wanaosakata dansi! Utaziona tezi zinavyofanya kazi kama zimefyatuliwa na umeme! Utaona mwili unavyofanya zoezi la ajabu ambalo hutalipata kwenye ukumbi wa mazoezi yoyote duniani.


Kwa hakika utachoka sana, hii ndiyo maana watu wengi hasa wanaume hulala kabisa usingizi mzito, wanawake wanaweza kuwa macho na kuzungumza.

By Jamhuri