Na Frank Christopher
Kwa zaidi ya muongo mmoja, uchumi wa Tanzania umeweza kukua wastani wa asilimia 7 na
kufanikiwa kutajwa kati ya nchi 10 zinazoshuhudia ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi barani Afrika
huku nyingine zikiwa Ethiopia, Ivory Coast, Senegal, Kenya kwa kuzitaja chache (Taarifa ya
Benki ya Dunia, 2017).
Licha ya kuwa na uchumi uliokua kwa wastani wa asilimia 7 pamoja na kuendelea kukua kwa
kiwango cha asilimia 7, 7 na 6.8 kwa miaka ya 2015, 2016 na 2017, Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF) limeionya Tanzania kutokana na mwenendo wake wa ukuaji wa uchumi na
kuishauri ifanye mageuzi haraka ili hali iwe nzuri zaidi kuliko ilivyo sasa.
Ni ukweli usiopingika kwamba moja ya viashiria vinavyotumika kupima mwenendo wa uchumi ni
ukuaji wa Pato Halisi la Taifa. Na, katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopita
(2011/12-2015/16) maoteo ya ukuaji wa uchumi kwa kipindi chote cha mpango ilikuwa ni
shabaha ya asilimia 8 hadi 10 lakini hakukuwa na mwaka ambao tuliweza kufikia lengo hilo.
Kushindwa kufikia lengo kulitokana na kutofanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati
hasa kwenye sekta za nishati, usafirishaji na kilimo na hivyo kutokuwa katika hatua nzuri zaidi
ya kuufikia uchumi wa kati. Na hata kwa mwaka 2016 uchumi ulikua kwa asilimia 7, na kwa
2017, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 6.8 hivyo kushindwa pia kuifikia shabaha ya
ukuaji wa asilimia 8 mpaka 10 inayokadiriwa na mpango wa pili wa miaka mitano wa Maendeleo
wa Taifa (2016/17- 2020/21).
Wasiwasi zaidi ni pale makadirio ya Benki ya Dunia (2017) yanapoonesha kuwa ukuaji wa
uchumi kwa miaka mitatu ijayo yaani 2018, 2019 na 2020 utakuwa asilimia 6.8, 6.8 na 6.9
ukuaji ambao ni chini ya shabaha stahiki za kutupeleka kwa kasi inayoridhisha zaidi katika
uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Na hata jarida la The Economist (2018) kupitia utafiti wake, limekadiria kwamba kama hali
itabaki kama ilivyo sasa, uchumi wa Tanzania utakua kwa wastani wa asilimia 5.8 kwa kipindi
cha miaka minne ijayo yaani 2018-2022 ukuaji ambao utakuwa wa chini zaidi kwa zaidi ya
miongo miwili iliyopita. Makadirio haya yameendelea kuibua maswali mazito kwa wadau na
jamii ni kwa jinsi gani uchumi wa nchi unavyoonekana kupitia kipindi kigumu hasa katika miezi
24 iliyopita.
Kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa takriban miezi 24 iliyopita kulitokana
na mambo yafuatayo:
Mabadiliko ya miundo ya utunzaji wa amana (akiba) za taasisi za Serikali: tangu kuingia kwa
Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali ilifanya uamuzi wa kuzihamishia amana za taasisi zake
Benki Kuu katika robo ya mwisho wa mwaka wa fedha 2015/2016 (Benki Kuu, 2016). Uamuzi
huu ulisababisha kuhamishwa kwa mabilioni ya shilingi na kuyapeleka Benki Kuu hivyo
kupunguza sehemu ya kiasi kikubwa cha fedha katika mabenki ya kibiashara na hatimaye
katika mzunguko wa fedha na kuchangia kupungua kwa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi
katika uchumi (mzunguko wa fedha) kutokana na mabenki kuchukua hatua mbalimbali kutokana
na uamuzi huo wa Serikali, hivyo kuibuka kwa vipindi vya kupungua kwa ukwasi ikilinganishwa
na mahitaji halisi ya uchumi kuliko ilivyotarajiwa, kiasi cha kuifanya Benki Kuu kutumia zana
zake za sera za fedha kama kununua dhamana za Serikali zinazoshikiliwa na mabenki ya
kibiashara na kushusha kiwango cha riba inachoyatoza mabenki yanapokopa Benki Kuu, ili

kukabiliana na hali.
Kupunguza matumizi kulikofanywa na Serikali: ifahamike kwamba, katika nchi yoyote serikali
ndiyo mdau mkuu kwa uchumi wa nchi husika na uamuzi wowote na mabadiliko yoyote ya
kisera yanayofanywa na serikali yana matokeo yake katika uchumi wa nchi husika ambayo
huweza kuwa hasi au chanya. Serikali inapofanya uwekezaji ni wazi itakopa kutoka vyanzo
vyake vya ndani kama Benki Kuu na benki za kibiashara za ndani ya nchi na hata nje na
hatimaye kuongeza mzunguko wa fedha na uzalishaji katika uchumi wa nchi.
Hivyo basi, Serikali inapopunguza matumizi yake ni wazi kwamba uzalishaji na uwekezaji
vitapungua na hatimaye kasi ya uchumi kukua itapungua. Serikali ya Awamu ya Tano
imepunguza kwa ‘kasi sana’ matumizi ya kawaida kiasi cha kuziathiri biashara nyingi
zilizotegemea Serikali kwa kipindi kirefu hasa zilizo katika sekta ya huduma kama mahoteli,
habari, mawasiliano, uhifadhi na usafirishaji huku ikiwa haijafanikiwa kwa kiwango cha
kuridhisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimaendeleo kwa wakati hatua iliyopelekea
kudorora kwa uchumi wa nchi.
Kutokutabirika kwa sera za Serikali kwa sekta binafsi: katika nchi yoyote, sekta binafsi ndiyo
injini ya ukuzaji uchumi wa nchi. Na ili ifanye kazi vizuri katika nyanja zote za kimaendeleo,
haina budi kushirikiana na serikali kwani serikali huandaa mazingira wezeshi kwa ajii ya sekta
binafsi kufanya uwekezaji. Lakini tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano, kumekuwa na
mitazamo tofauti kwa sekta binafsi.
Tumeshuhudia Serikali ikiamua kufanya biashara na taasisi zake yenyewe, jambo linalochagiza
kupunguza kasi na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi. Licha ya hilo,
tumeshuhudia kubadilika kwa sera na miundo ya utunzaji wa amana za Serikali katika taasisi
zilizo chini ya sekta binafsi na kuchagiza kubadilika kwa mtazamo na imani ya wafanyabiashara
na wawekezaji kwa sekta binafsi na hasa mabenki na hatimaye kushusha kiwango cha
ushindani kwa sekta binafsi, kutokana na wengi kuwa na imani na Serikali zaidi kibiashara
kuliko sekta binafsi; na hili laweza kuonekana kwa mabenki zaidi kwani mengi kwa sasa
hupendelea kuikopesha zaidi Serikali kuliko sekta binafsi.
Serikali kutokopa kutoka vyanzo vya nje kutokana na hali ya soko la fedha: kwa mwaka wa
fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukopa shilingi 2.1 trilioni kama mikopo ya kibiashara kwa ajili
ya kugharamia bajeti yake. Lakini katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17 Serikali
haikufanikiwa kukopa kiwango kilichotakiwa kutoka vyanzo vya nje kutokana na soko la fedha la
kimataifa kuwa na riba kubwa ikilinganishwa na ile iliyotegemewa hapo awali.
Kwa mfano, kiwango cha riba kwa ajili ya mikopo katika bara la Ulaya kilipanda kutoka asilimia
6 hadi asilimia 9 kiasi cha kufanya serikali kuahirisha kukopa kwa wakati husika hivyo
kuhamishia utafutaji wa mikopo kwa nchi nyingine kama India, China na Korea Kusini. Hali hii
ilisababisha kukwama kwa miradi mingi ya maendeleo na hatimaye kuchangia kwa kiasi
kikubwa kupunguza mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi.
Fedha nyingi iliyopatikana hasa kutoka katika vyanzo vya nje kama mikopo ya kibiashara na ya
masharti nafuu katika mwaka wa fedha uliopita, ilipatikana hasa katika robo ya tatu na ya nne
ya mwaka wa fedha, kitendo kilichokwamisha utekelezaji bajeti kwa wakati na kwa uhakika
zaidi. Na, kwa upande wa mikopo kutoka vyanzo vya ndani, kwa mwaka wa fedha 2016/17
Serikali ilifanikiwa kukopa asilimia 58 ya lengo katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka
wa fedha, hatua iliyochangia pia utekelezaji hafifu wa miradi kwa wakati husika na hatimaye
kushuka kwa kasi ya kukua kwa uchumi (Wizara ya Fedha, 2016).
Tishio la mikopo chechefu (non-performing loans): ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya fedha
ni injini kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi yoyote ile. Sekta imara ya fedha itajenga
uchumi imara na kadhalika kuyumba kwa sekta ya fedha ni kuyumba pia kwa uchumi wa nchi
kwa maana kwamba wawekezaji hawatapata mitaji ya uwekezaji ya muda mrefu au wakaipata
kwa gharama kubwa kuliko inavyostahili.

Kwa mwaka 2015, mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 24.8 lakini kwa
mwaka 2016 iliporomoka na kuwa asilimia 7.2, jambo lililosababisha kupungua kwa kasi ya
uwekezaji na hatimaye ukuaji wa uchumi. Hali hii ilitokana na tishio la mikopo chechefu (mikopo
iliyo kwenye hatari ya kutolipika) kwenye sekta ya mabenki ambapo mpaka Desemba 2016
ilifikia asilimia 9.53 ambayo ni juu ya kiwango kilichowekwa na Benki Kuu cha asilimia 5. Na
kuondokana na tatizo hili, mabenki yalipunguza kasi ya utoaji mikopo kwa kuongeza riba
(gharama za ukopaji) pamoja na kuongeza ukwasi (akiba) kitendo kilichochangia pia kupungua
kwa mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi licha ya hatua hizo kuongeza uhimilivu katika
sekta ya mabenki.
Na pia, kutokana na tishio hili la mikopo chechefu, benki za kibiashara nchini ziliamua kuongeza
amana zao kwa kupunguza manunuzi ya dhamana za Serikali pamoja na kuuza sehemu ya
dhamana za Serikali (treasury bills) walizokuwa wakizishikilia ili kuongeza ukwasi katika sekta
ya mabenki. Kwa mwaka ulioishia Desemba 2016, dhamana za Serikali zilizoshikiliwa na
mabenki zilipungua kwa asilimia 12.28, kitendo kilichopunguza takriban bilioni 599.7 katika
mzunguko wa fedha (Taarifa ya Benki Kuu, 2016).

Ends

1507 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!