Wiki iliyopita katika maandiko ya Mwalimu tuliona katika kitabu cha “Maendeleo ni Kazi”chama kimetoa maagizo ambayo yanatakiwa kutekelezwa na uongozi. Tuendelee

Elimu ya watu wazima.

Elimu ya watu wazima ni shughuli nyingine ambayo chama kimeshughulikia kutokana na agizo la mkutano Mkuu la kufuta ujinga katika muda wa miaka minne, yaani kwenye mwaka 1975. Chama kimehimiza sana jambo hili kila mahali viongozi wamesaidia kuhakikisha kuwa wananchi wanaitikia wito huu. Na matokeo yake ni mazuri sana. Mahali pengi pana matumaini kabisa ya kufuta ujinga kunako mwaka 1975.

Vijiji vya Ujamaa:

Mkutano Mkuu huu ungewapongeza wananchi wote ambao wamekubali wito wa TANU wa kuishi katika vijiji vya ujamaa. Hasa mikoa ya Mtwara na Lindi ambako asilimia zaidi ya 80 kwa mia ya wanaishi katika vijiji vya ujamaa.

Mkutano Mkuu wa 15 uliagiza Wafanyakazi kwenda vijijini kushirikiana na wanavijiji katika kazi ili kuimarisha uhusiano kati ya wafanyakazi na wakulima.

Agizo linguine lilikuwa ni juu ya wanavijiji kutembeleana wao kwa wao ili kuweza kujifunza kutoka wenyewe kwa wenyewe. Kadhalika iliagizwa kuwa pawe na mipango ya semina za siasa vijijini. Waheshimiwa wajumbe maagizo haya yametimizwa lakini kwa uchache, ipo haja ya kuziendesha semina hizo huko mikoani bila kutegemea makao makuu kwani zinahitajiwa sana.

Hapa pia yafaa kuwapongeza wanafunzi wa vyuo mbali mbali ambao kwa wingi wanakwenda kuishi katika vijiji vya ujamaa na kushiriki kazi na wanavijiji.

Mkutano utafurahi kujua kuwa wanavijiji wanapata mafunzo ya utalaam kutoka vijijini mwao kwa kutembelewa na wataalam mbali mbali ambao huweza kuwafundisha utaalamu  mdogo mdogo kwa mfano juu ya kilimo bora; afya na kadhalika. Pamoja na hayo wanavijiji sasa wanapewa mafunzo kwenye vyuo vya maendeleo vya wilaya ambako hujifunza utaalamu juu ya mambo mbali mbali hasa kilimo; kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa ambako hufunzwa ufundi mbali mbali kama vile Ujenzi, Useremala, Uhunzi, Ufundi mitambo, Ufundi viatu, Ushonaji, n.k. kwenye chuo cha Ushirika Moshi ambako hujifunza utunzaji wa mahesabu na mbinu za Ushirika; na kwenye Mahospitali ambako hufunzwa udresa na huduma ya kwanza. Hata kama utalamu huo unapatikana ni kiasi kidogo mno kwani bado vijiji vingi vinakabiliwa na ukosefu wa uongozi bora, ufundi wa uwekaji wa mahesabu na upangaji mipango.

Mwisho yafaa kusema kuwa vijiji vya Ujamaa vinazidi kuongezeka na sasa vinafikia 5,622 vyenye wakazi wanaokaribia milioni 2 na nusu kwa hesabu ya Machi, 1973 yaani zaidi ya asilimia 14 za Watanzania wote. Vile vile yafaa kukumbushana umuhimu wa viongozi wa TANU kulazimika wawe mfano mzuri kwa wananchi kwa maisha yao na vitendo vyao pia.

Reli ya Uhuru:

Mojawapo ya maagizo ya Mkutano Mkuu wa 15 lilikuwa wito kwa wananchi kuanzisha vijiji vya ujamaa kando kando ya reli ya uhuru. Lakini azimio hili halijawa na mafanikio ya kutosha katika mikoa inayohusika, hata hivyo juhudi inafanywa kulitekeleza kikamilifu.

Hapa inafaa vile vile kuwaarifu wajumbe waheshimiwa Maendeleo ya Ujenzi wa Reli yenyewe. Kazi inakwenda vizuri sana hata imewezekana kufika Tunduma kilomita 950 toka Dar es Salaam miezi kumi na tatu kabla ya wakati uliofikiriwa. Hii imewezekana kwa ajili ya juhudi na ushirikiano mzuri kati ya wafanyakazi wote wa kichama, Wakitanzania, na Wakizambia na Wafanyakazi wa bandarini Dar es Salaam, na kwa ajili ya ushirikiano mzuri wa wananchi ambao reli imepita, ambao bila kusita walisaidia wafanyakazi wa Reli hiyo kwa chakula na mengineyo mengi. Tarehe 27 Agosti, 1973 kulikuwa na sherehe ya kumaliza kazi ya reli upande wa Tanzania nay a kuanza upande wa Zambia.

Ulinzi na Usalama.

Majeshi yetu ni majeshi ya Umma, na yanatumika kwa kuwafunza wananchi wenyewe jinsi ya kujilinda katika sehemu wanazoishi, na kuwa na uwezo wa kutoa habari zinazohusu usalama wa Taifa letu, na kwa ajili hiyo yanaendesha mafunza ya ulinzi wa mgambo kwa nchi nzima ili ulinzi na Usalama uwe mikononi mwa majeshi yetu na watu wenyewe.

Kwa kuwa majeshi yetu ni ya umma, Chama ndicho kinachoona kuwa vijana wote wanaojiunga katika Majeshi yetu ni budi wawe ni wana-TANU au wana-Afro-Shirazi. Na katika Majeshi yenyewe mipango ya mafunzo ya siasa yanatiliwa mkazo sana. Kwa kweli majeshi yetu yote yamekuwa ni vyuo vya siasa yetu ya Ujamaa.

Kuhusu uhusiano wa majeshi hayo na wananchi kwa jumla ni mzuri kwani wanajeshi na wananchi wanasaidiana katika kazi ya kulinda uhuru na nchi yetu, katika kazi za Uchumi, na katika kazi nyinginezo za kujenga nchi.

Majeshi yetu yameendelea kulinda usalama wa Taifa  kwa ujumla na huko mipakani ilipobidi  kutumia silaha basi waliwaadhibu vikali maadui.

 

 

 

Matarajio Yetu:

Taarifa hii ni ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu uliopita wa chama. Tumekwisho ona mafanikio yetu nadhani inafaa tuangalie na matarajio yetu ni nini.

Katika kuangalia matarajio yetu  yafaa kwanza kukukmbuka kwamba maazimio hayo tuliyoyatekeleza yalikuwa ya aina  mbili. Kulikuwa na maazimio ambayo utekelezaji wake ulikuwa ni wa mara moja; ulikuwa ni wa kuendelea, kwa mfano Azimio la kutekeleza fikra za Mwongozo. Kwa ajili hiyo basi matarajio yetu ya kwanza ni kuendelea kuyatekeleza yako maazimio ambayo utekelezaji wake ni wa kuendelea ili kwamba utekelezaji wake ukamilike barabara.

Mojawapo ya fikra zinazotokana na Mwongozo ambazo utekelezaji wake wahitaji vitendo ni siasa ni kilimo na agizo juu ya viwanda vidogo vidogo nchini. Tumekuwa na semina juu ya siasa ni kilimo. Sasa tunatarajia kuendelea na semina hizo ili zaidi katika vitendo. Kadhalika kuhusu viwanda vidogo vidogo tutasisitiza semina zenyewe ziunganishwe na vitendo.

Utamaduni wetu bado kabisa kuimarishwa. Ukweli ulivyo ni kwamba bado hatujajikomboa kiutamaduni. Na kwa sababu tuko katika hila hiyo watoto wetu tunashindwa kuwapa utamaduni unaofaa, mathalani juu ya heshima na adabu, mavazi, michezo na yote mengineyo yahusuyo utamaduni. Tunawaacha wajiokotee utamaduni wowote ule wanaokutana nao.

Kwa hiyo basi tunakusudia kuendeleza kwa nguvu zaidi utekelezaji wa Azimio la Mkutano Mkuu uliopita mpaka limetimizwa kikamilifu na tumejikomboa kweli kiutamaduni pia.

Uimarishwaji wa Chama:

Tunatarajia kuimarisha Chama kwa njia ya Semina; kwani semina husaidia sana kutia uhai katika Chama. Kwanza tunakusudia viongozi wote wa chama hasa matawini wapate mafunzo ya kutosha kuwawezesha  kuielewa  bara bara siasa yetu. Pili tunakusudia kuendelea na mafunzo ya wanachama na wananchi kwa jumla vijijini, maofisini na viwandani.

By Jamhuri