Na Dk. Felician Kilahama

Sehemu ya kwanza, mwandishi wa makala hii, Dk.
Felician Kilahama, alisema amekuwa
akizungumza na viongozi mbalimbali katika vijiji
alivyotembelea, lakini cha kushanganza hakuwahi
kubahatika kukutana na viongozi wa vijiji wenye
upeo mzuri na uelewa wa kutosha juu ya thamani
na umuhimu wa rasilimali ardhi kwenye vijiji vyao.
Ifuatayo ni sehemu ya pili na ya mwisho
inayohusu uharibifu wa mazingira wa ‘kutisha’
katika eneo la Bukwaya, Musoma Vijijini mkoani
Mara. Endelea…

Napata uchungu mkubwa ninapopita sehemu za
vijijini nikakuta misitu mizuri ya asili, iwe ni
kwenye ardhi chepechepe au katika vyanzo vya maji
na mito au sehemu nyinginezo, inafyekwa hovyo

hadi rasilimali miti kuchomwa moto kama ni kitu
kisichokuwa na thamani yoyote.
Hali ya mamna hiyo ni hatari kwa mazingira na
rasilimali miti kuunguzwa hadi majivu bila ya
wanavijiji kunufaika. Hilo si jambo jema. Ukiuliza
inakuwaje miti ya asili iliyokomaa inaangushwa
hovyo na kuunguzwa moto, jibu ni kwamba mhusika
anaandaa shamba kwa ajili ya kilimo.
Unabaki unajiuliza maswali bila majibu: zaidi ya
miaka hamsini ya Uhuru wa nchi yetu bado
Watanzania hatuthamini misitu ya asili na badala
yake tunaiteketeza hovyo kwa kisingizio cha
kulima?
Kwa kusema hivyo haina maana kuwa sitaki watu
walime kwenye maeneo ya misitu ya asili ili kupata
chakula. Ninachomaanisha ni kwamba busara
itumike kwa faida yetu na uhifadhi wa mazingira
utakavyokuwa mzuri kwa matumizi ya vizazi
vitakavyofuata.
Mathalani, iwapo eneo fulani kulingana na matumizi
bora ya ardhi kijijini, limetengwa kwa shughuli za
kilimo, na eneo husika lina miti ya asili, badala ya
kuikata na kuichoma, ni vema kijiji kwa kupitia
ushauri wa kitaalamu, wakulima na wafugaji
wakaitumia miti hiyo kwa kuzalisha bidhaa kama

mbao, nguzo, fito, mkaa, kuni au kuuza magogo na
kijiji kuingiza mapato ambayo yatatumika kwa faida
ya wanakijiji wote.
Baada ya kufanya hivyo wakulima ndipo wagawiwe
maeneo ya kilimo au ufugaji, lakini pia wahusika
waitumie rasilimali ardhi kwa misingi endelevu kwa
kufuata ushauri watakaopewa na wataalamu wa
kilimo, mifugo, misitu na nyuki.

Je, elimu ya mazingira na kilimo na ufugaji bora
wenye tija haitolewi mara kwa mara kwa wakulima
na wafugaji?
Idara za Ugani na Uhamasishaji kwa umma juu ya
umuhimu wa kutunza mazingira hususan kutokata
miti hovyo zifanye kazi ipasavyo ili kuwasaidia na
kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji
wasiendelee kutumia rasilimali ardhi na misitu ya
asili hovyo.
Uharibifu kwa mazingira na athari ya moto kwa
rasilimali miti si kitu kizuri, hivyo tuondokane na
mtazamo kwamba wanatumia moto kuandaa
mashamba au wafugaji kupata nyasi change, bali
tutumie utaalamu wa kilimo cha kisasa na kijani au
ufugaji unaoboresha malisho ya mifugo badala ya
kuchunga hovyo.

Kufyeka misitu ya asili na kuichoma moto ni mbinu
za kilimo zilizopitwa na wakati. Vilevile siyo
mtazamo mzuri kimaendeleo maana ni tabia
inayosababisha sehemu mbalimbali nchini
ziharibiwe kutokana na matumizi ya rasilimali ardhi
na misitu ya asilia yasiyo endelevu.
Kwa maeneo ya Bukwaya, wataalamu wa misitu na
ufugaji nyuki tukishirikiana na wenzetu wa fani za
kilimo na ufugaji na wanamazingira wote; itabidi
tufanye kazi ya ziada ili kuisaidia jamii ya Bukwaya
isiendelee kuharibu mazingira.
Itabidi ushauri wa kitaaluma utolewe hasa juu ya
aina ya miti inayofaa kwenye eneo hilo tukiweka
mkazo kwenye aina za miti ya asili iliyokuwa
ikistawi kwenye eneo hilo miaka ya nyuma.
Baadhi ya aina za miti ziwe zenye uwezo wa
kuboresha ardhi na kurutubisha udongo hivyo
kuwezesha kilimo-miti (agroforestry) kunufaisha
wakulima.
Aina nyingine za miti ziweze kutumika kulisha
mifugo (fodder tree species) na bila kusahau miti ya
matunda na dawa kwa minajiri ya kutaka kuboresha
afya za wana Bukwaya na kuuza ziada kupata fedha
kwa matumizi mbalimbali kwenye familia zao.

Ubora wa mbegu za miti pia utatiliwa mkazo na
matumizi ya kuhifadhi mazingira kupitia utaalamu
wa kijadi (indigenous technical knowledge) kama
“Ngitiri” na viongozi vijijini kujengewa uwezo ili
kusimamia maendeleo endelevu kwenye vijiji vyao
ni baadhi ya masuala muhimu ya kuwekea mkazo.
Matumizi bora ya ardhi ya kijiji iwe ni ajenda ya
kudumu kwenye masuala yatakayokuwa
yanajadiliwa kwenye mikutano ya vijiji na kata.
Kila linalowezekana lifanyike ili kwa pamoja
tuhakikishe uhai wa nchi yetu unarejeshwa kwa
faida yetu na vizazi vijavyo.
Twaweza tujizatiti tusonge mbele: Mazingira bora ni
uhai na kutumia misitu ya asili hovyo ni sawa na
kujichimbia kaburi. Hakuna lisilowezekana- chukua
hatua- panda miti kwa wingi na hifadhi misitu ya
asili.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama
ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa
Misitu Tanzania (TAFORI). Anapatikana kwa
simu: 0756 007 400.

1190 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!