Mmoja wa wasomaji kindakindaki wa JAMHURI amenipigia simu na kuukosoa msimamo wangu kuhusu wachuuzi (wamachinga), akisema ninavyopendekeza watengewe maeneo maalumu, maana yake ninataka tatizo hilo liendelee kukua.

Kwa mtazamo wake, uwepo wa wamachinga wengi kiasi kinachoonekana sasa katika miji na hata vijiji nchini kote, ni jambo linaloashiria hatari kubwa iliyo mbele yetu.

Anasema kadiri unavyojenga miundombinu ya wamachinga mijini ndivyo unavyozidi kuwavutia wengi zaidi kuingia kwenye shughuli hiyo. 

Matokeo yake siku moja Tanzania yote itakuwa jamhuri ya wamachinga. Kwa mtazamo wake, ambao kimsingi ni mtazamo wa kulipunguza tatizo la ongezeko la wamachinga, ni kuandaa shughuli za uzalishaji mali, hasa kilimo. 

Nami nikawa ninajiuliza, hizi Sh bilioni 500 za mikopo ya shahada zisizo na faida, kwanini nusu yake isingeelekezwa VETA?

Anasema Tanzania kwa utajiri wa ardhi, rasilimali asilia kama madini, bahari, maziwa, mito, misitu na mifugo haipaswi kuwa na vijana wanaojiajiri kwenye umachinga. Bila shaka huu ni mtazamo mzuri ambao watunga sera wataufanyia kazi.

Leo ninapenda nijadili kwa ufupi mambo kadhaa yanayoendelea baada ya kuondoka duniani kwa Rais John Magufuli. 

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye hotuba yake moja aliwashangaa Watanzania kuona wanaacha mazuri, badala yake wanakumbatia mambo yasiyofaa yaliyotendwa na awamu yake. Aliyaita mambo ya hovyo.

Kiongozi mkuu wa Awamu ya Tano hatunaye, lakini bahati nzuri waliokuwa wasaidizi wake wengi wameendelea kuwamo kwenye Awamu ya Sita. 

Rais Magufuli anakosolewa kwa mambo kadhaa, yakiwamo ya haki za binadamu, ubabe, kuwalinda watu kadhaa waovu, kuwabeba waliojipendekeza kupita kiasi na kadhalika. 

Binadamu ndivyo tulivyo. Haiwezekani akawapo binadamu wa kumwagiwa sifa tu na asiguswe upande wa pili wa lawama. 

Hata Baba wa Taifa wapo wanaoamini alifanya mambo yasiyofaa. Huo ni mtazamo wa kibinadamu kulingana na kila mmoja anaguswa vipi na uongozi kwa wakati husika.

Pamoja na udhaifu unaotajwa wa Awamu ya Tano, kitu kimoja kizuri kilichoonekana ni katika kada ya utumishi wa umma – nidhamu ya kazi. 

Sasa kama nidhamu hiyo ilikuwa ya woga au halisi, hilo ni jambo jingine. Lililo muhimu ni kuwa walau ilionekana Watanzania, hasa watumishi wa umma, wanaweza kubadilika kutokana na hofu ya kuwatumikia wananchi. 

Kama nidhamu hiyo ilitokana na hofu tu kuhusu mtawala aliyekuwapo, basi tuangalie ni namna gani hofu hiyo sasa inajengwa ndani ya mifumo yetu ya utumishi wa umma na hata kwenye sekta binafsi ambako walau kuna nafuu.

Tayari tunaanza kuona huduma za kupokea na kuhudumia wagonjwa kwenye hospitali za umma zimeanza kurejea kule kule kwa kawaida. 

Yapo malalamiko mengi ya bayana kwamba utoaji huduma katika zahanati, vituo vya afya na hospitali si mzuri. 

Hili halina budi kumulikwa. Ilipendeza sana kuona watoa huduma za afya kwa wagonjwa wakiwa waungwana kuanzia kuwapokea hadi kuwahudumia.

Tayari kuna malalamiko ya rushwa kwenye taasisi za umma kupitia ukwamishaji mifumo ya ‘control number’. 

Makusanyo ya fedha za umma yaliongezeka mno kutokana na mfumo huu, lakini sasa sehemu kadhaa huduma zinatolewa kwa mfumo wa ‘manual’ kwa kisingizio cha ‘mtandao kuwa chini’. Inajulikana bayana kuwa kwa mfumo wa ‘control number’ ni vigumu sana kuhujumu mapato ya umma, lakini kinyume cha hivyo ni ulaji tu.

Kuna tuhuma za rushwa kwenye maeneo kama bandarini, hasa kwenye kitengo cha ukaguzi wa magari. Ukaguzi unaofanywa ni wa ujanja ujanja tu. 

Kuna malalamiko kuwa mwenye kuhitaji huduma (mawakala) wanachofanya ni kuweka kiasi fulani cha fedha kwenye faili kisha baada ya muda watapelekewa faili lao. 

Kama wahusika watasoma hapa, waangalie ukusanyaji wa mapato yanayotokana na magari yenye dosari ulivyokuwa awali na ulivyo sasa kwa uwiano wa idadi ya magari yanayoingia nchini. Kuna jambo la kulitazama hapo.

Kwa ufupi kuna malalamiko mengi na kwa maeneo mengi kuhusu kuhujumiwa kwa mapato ya serikali. Kama kweli tunaitakia mema Awamu ya Sita ili itekeleze wajibu wake kwa wananchi, hatuna budi kuyasema haya kwa lengo la kutafutiwa ufumbuzi.

Eneo jingine ambalo linasemwa ni la usalama barabarani. Uongozi wa juu wa Awamu ya Sita hauna budi kukemea na kufuta ile kauli ya ‘pesa ya kubrashia viatu’ ili polisi wasijione wana haki ya kukusanya rushwa bila aibu. 

Hata ongezeko la ajali za barabarani, hasa malori na mabasi chanzo kimojawapo kinachotajwa ni rushwa. Wapo matrafiki wasiokagua magari, badala yake hupewa chochote na kuruhusu magari yatembee. Yapo maelezo ya kuvurugwa kwa mfumo wa vidhibiti mwendo hasa nyakati za usiku. Katika hali ya kawaida ni vigumu kuchezea mfumo huo bila ushirikiano wa mamlaka zinazohusika.

Kwa ufupi kuna mambo mengi ambayo Watanzania walianza kuachana nayo, lakini taratibu yanarudi. Swali linaweza kuwa kwanini yanarudi? 

Jibu laweza kuwa kwamba yanarudi kwa sababu hakuna kitu cha umma kinachoweza kudumu kama hakikujengwa katika mifumo. 

Kwa miaka mingi tumeendesha mambo kwa zimamoto na kwa utashi wa aliye na madaraka. Hii ni dosari. Tujenge mifumo ambayo yeyote anayeingia au kutoka ataikuta na kuiacha ikiwa imara.

Mifumo inajengwa namna gani? Hilo nalo ni swali muhimu. Mifumo inajengwa kwa namna ya kuwajibishana kupitia Katiba na sheria zilizo imara. 

Kwa mfano, sioni kwa mfumo wa sasa jaji anaweza vipi kukwepa kupokea maelekezo na mwongozo wa aliyemteua. 

Sioni ni kwa namna gani DC au RC anaweza kuwasikiliza zaidi wananchi badala ya aliyewateua.

Wakati wakosoaji wa awamu zilizopita wakiendelea na kazi hiyo, tusisahau kuendelea kuyaenzi yaliyo mazuri kama ya watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa haki na kwa usawa.

643 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!