Bukoba wapinga kuanzisha mkoa wa Chato

*Waeleza ilivyojinyofoa Mkoa wa Kagera mwaka 2005

*Wataka Geita ibadilishwe jina iitwe Chato kumaliza kazi

Na Mwandishi Wetu, Bukoba

Wabunge na wazee wa Mkoa wa Kagera wamepinga kuanzishwa Mkoa mpya wa Chato kwa kumega wilaya za Bihalamulo, Ngara na kata tatu za Wilaya ya Muleba kuunda mkoa huo mpya, JAMHURI linathibitisha.

Kwa njia tofauti, wabunge na wazee hao wamepinga utaratibu unaotumika ‘kulazimisha’ kuanzishwa Mkoa wa Chato, wakisema umejaa mbinu chafu, lakini pia wakaongeza kuwa Chato iliikataa Kagera mwaka 2005 ikakimbilia Mwanza, baadaye ikafurukuta ikaumega Mkoa wa Kagera na Mwanza ukaundwa Mkoa wa Geita, ila bahati mbaya, malengo yake ya kupata makao makuu hayakutimia, hivyo hadi leo hawajaridhika.

Katika mkutano wa wazee wa CCM uliofanyika Oktoba 27, 2021 katika Ukumbi wa CCM mkoani Kagera, wazee hao walitoa tamko na kuandika waraka kwenda kwa viongozi mbalimbali wa mkoa na taifa ambao JAMHURI limeuona, wakisema: “Ni ukweli usiopingika kwamba pamoja na maendeleo makubwa yaliyopatikana tangu Uhuru kujenga umoja na mshikamano, Chato haijawahi kuridhika sana na majirani zake.

“Chato ilikuwa tarafa ya Wilaya ya Biharamulo. Mwaka 1995 ikadai na kupewa Jimbo lake la Uchaguzi la Biharamulo Mashariki. Haikuridhika. Ikadai na kupewa Wilaya ya Chato, mwaka 2005. Mwaka 2012, haikuridhika. Ikajitenga na Kagera na kudai mkoa wake. Vigezo vikashindikana makao makuu ya mkoa mpya yakapelekwa Geita. Chato haikufurahi.

“Badala ya kuuendeleza Mkoa mpya wa Geita miundombinu mingi ikajengwa Chato. Sasa Chato inataka kugeuka kutumia ubaguzi huo kuvuta wilaya za Kagera ilizojitenga nazo ilimradi ipewe mkoa wake! Hapa hatuoni nia njema. Kuna athari ya mivutano mipya kuibuka. Historia isije ikajirudia. Mkoa mpya wa Chato nao ukakuta unapewa makao makuu mbali na Chato maana kwa vigezo vya kuwa katikati, Biharamulo au Nyakanazi ni katikati ya Chato na Ngara na Bukombe! Na Kasulu kama hii itamegwa kutoka Kigoma.

“Sisi wazee hatuna budi kutoa tahadhari ya kuibuka kwa mtafaruku wa hata jina la mkoa mpya. Mwaka 2015 kulikuwa na zoezi la kuongelea mkoa mpya wa Muyobozi ambao ungeunganisha Chato, Biharamulo, Ngara na Kakonko kutoka Mkoa wa Kigoma. Tunaamini mkoa hauwezi kujengwa tu kwa ajili ya kuwaridhisha watu wa sehemu moja kwa gharama ya watu wa sehemu nyingine jirani. Inatakiwa kila mtu awe mnufaika, WIN-WIN, eneo linapounganishwa,” inasema sehemu ya waraka huo uliosainiwa na wazee 12 wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mzee Joseph Kamanyi Masabala.

Wengine waliosaini waraka huo unaoeleza historia ndefu ya kuanzishwa kwa Mkoa wa Kagera, athari zitakazotokea kwa uamuzi huu za kijamii na kiuchumi ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Wazee wa Kagera, Oliva Kato Owibingire, Pius Ngeze kutoka Ngara, Prof. Anna Tibaijuka, Haruna Almasi Bigilaenyema, Salvatory Rwiguza Karabamu, Mary Mushumbusi Kassano, Oswald Ignas Makanzu, Hudson Okcran Bagege, Elizabeth Kokwemage Mkimala, Sheikh Nooran Amri na Caritas Pancreas.

Kwa upande wao, wabunge wa Mkoa wa Kagera wamemwandikia barua Mwenyekiti, Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) Mkoa wa Kagera Oktoba 27, 2021  wakisema:

HOJA YA WABUNGE KUPINGA KUMEGA MKOA WA KAGERA

1. UTANGULIZI

Sisi wabunge wa Mkoa wa Kagera kupitia Wilaya ya Muleba na Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mhe Charles John Mwijage wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Dk. Oscar Ishengoma Kikoyo wa Jimbo la Muleba Kusini, na Mhe. Dk. Jasson Samson Rweikiza tumepokea wito wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kagera cha tarehe 29/10/2021 tukiwa tayari tumerudi Dodoma kwa ajili ya vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge.

Barua za wito wa kikao zimeambatanishwa na ajenda za RCC. Ajenda namba 4 ya kikao tajwa inahusu mapendekezo ya wilaya za Biharamulo na Ngara kupelekwa mkoa pendekezwa wa Chato. Hoja ya kuumega Mkoa wa Kagera, inatualika kujadili faida na hasara zake kwa Mkoa wa Kagera kwa kuzingatia masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Tukiongozwa na uzalendo wetu kwa Mkoa wa Kagera na utaifa wetu kwa taifa letu, kwa hali yoyote ile, pendekezo la kumega Mkoa wa Kagera lina athari kubwa sana kuliko faida kwa ustawi wa Mkoa wa Kagera kihistoria, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kwa sababu hizo, na nyingine zitakazotolewa hapa chini, hatukubaliani na hoja ya kuumega Mkoa wa Kagera.

2. CHIMBUKO LA MKOA MPYA WA CHATO

Chimbuko la kuomba Mkoa wa Chato halina mashiko kisiasa, kiuchumi wala kisheria. Chimbuko la Mkoa wa Chato linatokana na mwombolezaji mmoja aitwaye Bigambo wakati wa msiba wa hayati Rais John Magufuli. Mwombolezaji huyo alidai kusikia hayati Magufuli akitaka Chato uwe mkoa, jambo ambalo halina uthibitisho wowote kisiasa.

Vigezo vya kuunda mkoa mpya hutokana na mkoa mama kutokana na ukubwa wake na eneo la jiografia yake kuomba kumegwa ili kusogeza huduma kwa watu wake. 

Kwa ombi hili ni tofauti sana, wilaya ndogo na changa ya Chato iliyoanzishwa mwaka 2005 inaomba kuwa mkoa ili maeneo mengine yamegwe kuisaidia kutimiza azima yake ya kuwa mkoa, jambo ambalo ni kinyume cha dhana na falsafa ya uundwaji wa mikoa katika historia ya taifa hili lililoasisiwa na viongozi wetu mahiri.

Geita, mkoa mama, nao ni mchanga ulioanzishwa mwezi Machi mwaka 2012 ukimegwa kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera. 

Pamoja na uchanga wake, Geita ni moja ya mikoa midogo ikiwa na kilomita za mraba 20,054. Ukichukua ukubwa wa mikoa wa Geita (20,054 Km2) na Kagera (35,686 Km2) kwa pamoja haifikii ukubwa wa Mkoa wa Tabora wenye ukubwa wa kilomita za mraba 76,150 au Morogoro wenye ukubwa wa kilomita za mraba 70,624.

Ipo mikoa mikubwa na mikongwe iliyostahili kuleta ombi kama hili, si Wilaya ya Chato wala Mkoa wa Geita. Kwa ukubwa wa Mkoa wa Kagera na/au Geita kuendelea kuumega, mikoa ya Kagera na Geita itakuwa mikoa midogo sana.

3. FAIDA

Kwa tathmini za kiuchumi, kijamii na kisiasa na kwa kuangalia jiografia ya Mkoa wa Kagera kwa sasa na wilaya zinazolengwa kupelekwa, hakuna faida yoyote kwa Mkoa wa Kagera inayoweza kushawishi wananchi wa Mkoa wa Kagera kuridhia wilaya za Biharamulo na Ngara kupelekwa mkoa pendekezwa.

4. ATHARI

Kwa kutumia vigezo vilivyotajwa hapo juu, athari kwa Mkoa wa Kagera bila wilaya zake hizo mbili na kwa taifa zima la Tanzania ni kubwa sana.

4.1 KIJAMII:

Mkoa wa Kagera ni muunganiko na mshikamano wa wilaya saba (7) za utawala zenye halmashauri nane (8). Pamoja na kuwa na wananchi wanaoweza kuhesabika kuwa makabila yanayojionyesha manne na koo nyingi sana, mapito ya mkoa huu katika historia ya kuwepo kwake yanaufanya mkoa huu kuwa jamii iliyoshikamana na imara kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mkoa wa Kagera kwa kupakana na kuwa karibu na nchi nyingi umekuwa ukifikiwa na wageni wengi wa aina mbalimbali, lakini wakati wote. Wana-Kagera walijiona wamoja na katika umoja huo wameweza kuhimili matokeo yote hasi yaliyoletwa na wageni hao.

Kwa kuomba kuondoa wilaya za Ngara na Biharamulo kutasababisha mgawanyiko katika jamii na kufufua tofauti za kikabila na kikanda na koo zilizokwisha kuzikwa kwa siku nyingi za uhai wa mkoa huu. Pamoja na sababu nyingine, hii inatokana na ukweli kuwa wananchi wa wilaya tano zinazobaki hawakukubaliana na hawatafurahia wilaya za Biharamulo na Ngara kumegwa.

Kwa taifa kuna athari kubwa za kijamii, kisiasa na kiusalama kwani mpangilio wa wilaya tatu (3) zinazopendekezwa kuunda mkoa pendekezwa, zina wingi wa watu wenye nasaba na ushawishi wa mataifa ya jirani ambayo hayajatulia kiusalama. Mshikamano wa Mkoa wa Kagera uliojengeka kwa muda mrefu uliweza kudhibiti na kumaliza nguvu ya athari hiyo.

4.2 KIJIOGRAFIA:

Kuondoa wilaya za Biharamulo na Ngara kunaitenga Kagera inayobaki na kuinyima nafasi ya ‘location advantage’ ya mipaka ya Kabanga na Rusumo. Ustawi wa Mkoa wa Ziwa Magharibi ulitokana na hiyo ‘location advantage’. 

Katika zama hizi ambazo biashara kati ya Mkoa wa Kagera na nchi jirani unaendelea kukua na kuimarika, kuzimega wilaya hizo kutaunyima Mkoa wa Kagera fursa hizo za kibiashara.

Mgawanyo au kumegwa huku kunapunguza eneo la Mkoa wa Kagera. Mkoa wa Kagera una ukubwa wa eneo la mraba 35,686 (KM2 35,686) ikijumuisha nchi kavu na eneo la maji ya Ziwa Victoria. Eneo la maji ni kilomita za mraba 10,173 na eneo la nchi kavu ni kilomita za mraba 25,513. Wilaya ya Biharamulo na Ngara ambazo ni maeneo ya nchi kavu ni kilomita za mraba 9,371.

Hivyo, kumega wilaya hizo mbili, Mkoa wa Kagera utakuwa umebaki na kilomita za mraba 16,142 zinazofaa kwa kilimo na utalii. 

Ikumbukwe, Kagera si mkoa unaotawaliwa na shughuli za huduma (Service Industry) hali ambayo eneo dogo linaweza kuwa na watu wengi na shughuli nyingi za kiuchumi zinazohalalisha.

Huu ni mkoa wa wakulima, wafugaji na wavuvi, hivyo kupunguza eneo lake ni kuudhohofisha kijamii, kihistoria na kiuchumi. 

Katika uhai wa mkoa huu, hasa miaka 15 mpaka leo tumepigana sana kuwa karibu kwa kujenga miundombinu ya barabara. Kwa kazi inayoendelea kwenye ujenzi wa barabara mzunguko wa ndani kwa ndani kwenye mkoa itakuwa si tatizo. Kimsingi suluhisho si kumega wilaya bali kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara, reli, afya, elimu na uchumi.

 4.3 KISIASA:

Kagera bila Ngara na Biharamulo kisiasa si Kagera tunayoiona leo. Kufikia hatua hii ya kuwa na jamii tulivu na inayoelewana yenye mshikamano na mtazamo wa kimaendeleo haikuwa kazi rahisi. Wapo watu walihangaika kwa hadhi na nyadhifa mbalimbali nao kwa kutambua mchango wao kwa Kagera si busara kuumega kila uchao.

Siasa ya Kagera ni zaidi ya mtazamo wa chama cha siasa na chama au vyama vingine. Tunazungumza siasa kama hali au mtazamo wa jamii iliyoshuhudia na kuhimili kuanguka kwa uchumi baada ya kuvunjwa Chama cha Ushirika (BCU), kuanguka kwa bei ya kahawa, jamii ilivyolitangulia taifa katika vita dhidi ya nduli Idd Amin Dada, jamii iliyopokea wimbi la wakimbizi kutoka nchi jirani, lakini pia jamii ambayo ilikuwa ya kwanza kupigwa na janga hatari la ukimwi.

Pia jamii hii iliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi lililoharibu miundombinu na mali za watu, jamii ambayo wajasiriamali wake wengi na raia wengine walizama kwenye Mv Bukoba, ugonjwa wa mnyauko wa migomba kwa kutaja baadhi tu. Kimsingi, tafakuri ya mapigo haya yaliyoipata Kagera, serikali inapaswa kuja na mpango maalumu wa kuikarabati Kagera (Special Economic Rehabilitation Program) ili ipone kwa ujumla wake na si kuumega vipande vipande kama inavyokusudiwa.

Athari nyingine kisiasa ni kufanya uamuzi wa kumega mkoa kwa kufuata kilio cha mwombolezaji wa mkoa mwingine, Bwana Bigambo, alikuwa anaomboleza kama Watanzania wote walivyoumia na kila mtu kusema lake kabla ya kutulizwa.

Kitendo cha kutekeleza matakwa ya Bwana Bigambo na wenzake kwa kuumega mkoa mwingine kinaweza kuchafua taswira ya hayati Magufuli na kumpatia sifa ambazo hakuwa nazo wakati akiwa hai. 

Aidha, kitendo hicho kinaweza kutumiwa na watu wengine kudai vijiji vya marais wote waliopita na wajao vimege mikoa jirani na kuunda mkoa wa kwao na huyo Rais.

Njia rahisi ni RCC ya Mkoa wa Geita iliyokaa kwanza na kupanga mipaka ya Mkoa wa Chato ikae upya na iombe Mkoa wa Geita uitwe Chato au makao makuu ya Mkoa wa Geita yahamishiwe Chato ili kukidhi maombi ya Bwana Bigambo.

4.4 KIUCHUMI:

(1)

Kipekee, Mkoa wa Kagera katika historia yake imepigwa na majanga mengi tofauti na yalitajwa hapo juu kipengele cha (C) (ii). Katika kipindi hiki ambacho Kagera kama mkoa imeanza kuonyesha dalili za kupona ikimegwa itaathirika zaidi, maana eneo lake linalofaa kwa shughuli za kilimo, ufugaji na utalii na sehemu ya rasilimali watu litapelekwa mkoa tarajiwa.

(iii)

Katika maendeleo na ustawi wa Mkoa wa Kagera kwa Serikali ya Awamu ya Sita “mahali tulipo” kama ilivyokuwa kabla ya uhuru patachangia maendeleo ya mkoa huu. Hivyo kumega mipaka ya Kabanga na Rusumo na shughuli za kiuchumi ni kupunguza fursa kwa Mkoa wa Kagera katika kujenga uchumi wake.

(iv)

Katika uhai mkoa huu na majanga yaliyorudisha maendeleo ya wananchi nyuma. Wana-Kagera walikuwa na matumaini makubwa na uendelezaji wa mgodi wa nickel – Kabanga, Ngara. Imani yetu ni kuwa uchimbaji wa nickel ukianza mgodi huo utachangia maendeleo ya Mkoa wa Kagera kama ambavyo madini yanavyochangia maendeleo ya mikoa mingine. Uamuzi wa kumega wilaya zenye migodi ya nickel, dhahabu, tungstain na bati kutaathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya wilaya tano zitakazobaki.

5. USHAURI:

Tunashauri ili kuleta ustawi na maendeleo ya wananchi, nguvu za kiutawala na uongozi zielekezwe kwenye ngazi ya vitongoji, vijiji/mitaa, kata, tarafa na wilaya ambako ndiko wananchi waliko badala ya kuongeza gharama za ki-utawala kwa kuongeza mikoa.

Imetiwa saini hapa DODOMA siku ya 28 mwezi wa Oktoba, mwaka 2021.

Mhe. Charles Jono Mwijage (Mb)

Mhe. Dk. Jasson Samson Rweikiza (Mb)

Mhe. Dk. Oscar Ishengoma Kikoyo (Mb)

Nakala kwa:

1. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mkoa wa Kagera.

2. Katibu Tawala Mkoa, Mkoa wa Kagera.