Tarime kwawaka

Tarime kwawaka

*Vijana wachachamaa Zakaria kukamatwa usiku

*Namba gari la ‘TISS’, la raia Tarime zafanana

*Shabaha yamwokoa Zakaria, aliwindwa siku 7

*TISS waliojeruhiwa yadaiwa walitoka D’ Salaam

 

TARIME

 

NA MWANDISHI WETU

 

Utata umezidi kuibuka kwenye tukio la mfanyabiashara, Peter Zakaria, kuwapiga risasi maofisa wawili wa Usalama wa Taifa (TISS).

Taarifa zilizosambaa wilayani Tarime zinadai kuwa watu wawili walijeruhiwa, ambapo walitambuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, kuwa ni maafisa Usalama wa Taifa waliotoka Dar es Salaam kwenda kumkamata Zakaria.

Vijana wengi wa Tarime wamechachamaa wakitaka kupata taarifa sahihi juu ya nini kilitokea hadi Zakaria akamatwe usiku.

Pia namba za usajili za gari lililotumiwa na maofisa hao kwenye tukio hilo la kwanza na la aina yake lililotokea Tarime, mkoani Mara mwishoni mwa wiki, zinafanana na namba za usajili za mfanyabiashara mwingine wa mjini humo.

Picha za tukio hilo zinaonyesha gari lililotumiwa na TISS ni Toyota Land Cruiser, T 245 CTW lenye kibao cha njano. Hata hivyo, namba hizo hizo T 245 CTW pia zinatumika kwenye gari aina ya Nissan Morano, la mfanyabiashara Ndesi Mbusiro.

Tovuti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA) inaonyesha kuwa bima ya gari lenye namba hiyo ilikatwa Novemba 9, mwaka jana kwa Kampuni ya Maxinsure. Bima hiyo ya daraja la ‘Third Party’ ni ya gari binafsi.

TISS ipo chini ya Ofisi ya Rais, na magari yake ni ya serikali ambayo kwa kawaida hayakatiwi bima, kwa kuwa hakuna sera ya kuwezesha kuwapo kwa utaratibu huo. Magari ya mashirika ya umma hukatiwa bima ambazo aina yake hutokana na uamuzi wa bodi za shirika husika.

Mfanyabiashara Mbusiro anayedai kumiliki gari lenye namba hizo amezungumza na JAMHURI na kueleza mshangao wake wa kufanana kwa namba hiyo kwa magari mawili tofauti.

“Kudanganya ni kwa hawa wasiojulikana, lakini kwa Mungu huwezi kudanganya kitu. Hizi namba ziko kwenye gari langu ambalo nilinunua mwaka 2016. Kwa kweli Mungu anatenda mambo makuu, maana kama Zakaria angetekwa na kuuawa ina maana ningeingia kwenye matatizo. Wangesema gari langu ndilo limehusika,” amesema.

Mbusiro anasema yeye na Zakaria hawaelewani, na hata sasa wameshitakiana katika kesi iliyoko Mahakama ya Rufaa. “Alichukua nyumba yangu, mama yangu aliyekuwa akiishi humo alifariki dunia kwa mshituko, lakini pamoja na hilo nasema hili tukio lililopangwa la kumteka na pengine kumuua si la kiungwana kabisa,” amesema.

Vyanzo vyetu vinasema maofisa hao walitoka nje ya Mkoa wa Mara kwenda kutekeleza tukio la ‘kumkamata’ Zakaria kwa shauri ambalo halijafahamika.

“Hata polisi walipofika kwenye tukio hawakuwatambua, walichofanya ni kujitambulisha wakisema ‘sisi ni wenzenu’. Wakati huo Zakaria alishawajeruhi wawili na wengine wanaodhaniwa kuwa watatu wakiwa ndani ya gari,” kimesema chanzo chetu.

Sheria ya mwaka 1970 iliyoanzisha Usalama wa Taifa na kufanyiwa marekebisho mwaka 1996 inatamka bayana majukumu ya chombo hicho; na haiwapi maafisa mamlaka ya kukamata watuhumiwa, isipokuwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vilivyopewa dhima hiyo kisheria. Sehemu ya sheria tumeiambatanisha kwenye habari hii.

Tukio la Tarime limezidi kuibua mjadala wa muda mrefu nchini wa watu mbalimbali kutekwa na genge la ‘watu wasiojulikana’. Mara kadhaa vyombo vya usalama vimehusishwa kwenye matukio hayo, lakini Serikali imekuwa ikikanusha.

Licha ya kuwapo watu wanaotekwa na baadaye kupatikana wakiwa wamejeruhiwa, wapo waliopotea na hadi sasa hawajaonekana, akiwamo Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda. Lawama zimekuwa zikielekezwa kwa vyombo vya dola.

Baadhi ya waliotekwa na kuumizwa hapa nchini ni Dk. Stephen Ulimboka, Absalom Kibanda na mwanamuziki, Ibrahim Mussa (Roma Mkatoliki). Wengine waliotekwa, wakashambuliwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo; na tukio la karibuni ni la mfanyabiashara wa mabasi wilayani Simiyu, Samson Josiah.

Tukio lililotawala ndani na nje ya nchi ni la Septemba 7, mwaka jana ambako ‘watu wasiojulikana’ walimvizia na kumshambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema). Siku chache kabla ya tukio hilo, Lissu alizungumza na waandishi wa habari na kusema kwamba alikuwa akifuatiliwa na watu aliodai kuwa ni wa kutoka vyombo vya usalama. Tangu wakati huo Lissu anaendelea kupata matibabu nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Zakaria ambaye ni miongoni mwa makada na wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliwajeruhi kwa risasi maofisa hao wa TISS walipokwenda kumkamata kwenye ofisi zake zilizoko Tarime.

“Kilichomwokoa Zakaria ni shabaha yake kwenye matumizi ya silaha na wananchi waliojitokeza kwa wingi sana kumsaidia. Hali ilikuwa mbaya kama mlivyomsikia Mkuu wa Mkoa wa Mara akisema. Watu wamechoka kuonewa,” kimesema chanzo chetu.

Kuna taarifa kuwa asubuhi ya siku ya tukio hilo, Zakaria alinusurika kutekwa na watu wasiojulikana wakati akienda Utegi wilayani Rorya.

Kiongozi wa ukoo wa Zakaria, Samuel Chomete (65), amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo alipozungumza na JAMHURI. Amesema ndugu yake alivamiwa wakati akiwa na Sh. milioni 16 zilizotokana na biashara zake za siku hiyo.

“Tukio lilikuwa usiku saa 4 kasoro hivi. Kama watu wasingejitokeza kwa wingi, ndugu yetu angeuawa maana walishamkamata na kumwingiza kwenye gari ili waondoke naye,” amesema Chomete.

Ameelekeza lawama kwa serikali akisema kama kuna mpango wa kumkamata mtuhumiwa ni vizuri taratibu za kisheria zikafuatwa.

Amesema endapo asingejiokoa, angeuawa, akitoa mfano wa mfanyabiashara mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah, aliyetoweka kwa wiki mbili na baadaye mwili wake kuokotwa mtoni wakati gari alilotumia likikutwa limeteketezwa kwa moto ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Chomete amesema kinachosikitisha ni kuona wanaotuhumiwa kwenye matukio haya aliyoyaita ya mauaji ni watoto wa Watanzania, na kusema yakiachwa yatavuruga amani ya nchi.

Meneja na Msimamizi Mkuu wa mabasi na vituo vya mafuta – mali za Zakaria, Samuel Athumani, anasema: “Bosi Zakaria siku hiyo alikuwa akitoka ofisini kwa ajili ya kwenda nyumbani kwake, ghafla alivamiwa na watu ambao hakuwajua. Hata mimi sikuwajua. Baada ya hapo mzee (Zakaria) akaanza kupiga kelele akisema ‘Samuel nisaidie, nisaidie hawa watu wanataka kuniua, wanataka kunichukua’.

“Mimi nilipomfuata kumsaidia wakanionyeshea bunduki wakanilaza chini, wakaanza kumvuta mzee kumwingiza ndani ya gari, na muda tu nikasikia mlio wa bunduki. Kuna basi letu likawa linaingia mimi nikiwa nipo chini. Baada ya kuona ule mwanga mkali wa gari wakaniacha, wakawa wanachungulia basi. Nami nikapata njia ya kutoroka na kukimbia kwenda kuita polisi,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Starehe lilipotokea tukio hilo, Bashir Abdallah, anasema Zakaria alikuwa akifuatiliwa kwa muda wa wiki moja. Abdallah pia ni Diwani wa Nyamisangura.

Mashuhuda wengine waliozungumza na JAMHURI wanasema maofisa hao wa TISS walifika na kuegesha gari lao katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Zakaria. Wakalizuia gari la mfanyabiashara huyo. Wakafungua boneti wakitaka iaminike kwamba walikuwa kwenye matengenezo ya gari lao.

Mmoja wa mashuhuda ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa, anasema Zakaria alipotaka kwenda kwenye gari lake ndipo alipotekwa na akaanza kupambana nao wakiwa wanajitahidi kumfunga pingu.

Anasema kwa haraka haraka ilionekana kuwa watu watano walikuwa kwenye gari hilo aina ya Land Cruiser, na baada ya mvutano ndipo walipoanza kurusha risasi.

“Wakamnyang’anya bastola yake moja, hawakujua kama ana nyingine, alipoona wameanza kurusha risasi akaichomoa kujihami. Mfanyakazi mmoja akapiga simu polisi wakaja na kuwakuta majeruhi wawili na wenzao.

“Wakati huo vijana walijaa kwa wingi sana wakiwa tayari kwa lolote, ilibidi polisi wafanye kazi ya ziada kuwatawanya kwenye tukio hadi hospitalini walikopelekwa kutibiwa. Kinachoshangaza ni kuona hata polisi walipofika wakawa hawafahamu ila wao wakawa wanajitambulisha kwa kusema ‘sisi ni wenzenu’,” amesema shuhuda huyo.

Viongozi mbalimbali Tarime na Mkoa wa Mara wamelaani tukio hilo, wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kupata ukweli.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Tarime, Godfrey Francis, ameitwa polisi kuhojiwa kuhusu kauli yake baada ya tukio la kupigwa risasi maofisa wa TISS.

Muda mfupi baada ya taarifa za vurugu hizo kutokea, Francis, aliandika kwenye ukurasa wake akishutumu waliotenda tukio hilo, na kushukuru kuona Zakaria ameendelea kuwa hai.

Wiki iliyopita viongozi wa CCM Wilaya ya Tarime – Mwenyekiti wa Wilaya, Daud Ngicho; Mwenyekiti wa Vijana Wilaya, Francis na Katibu Mwenezi Kata ya Sabasaba Mjini Tarime, Charles Andrea, wamesema walihojiwa kwenye Kamati ya Ulinzi ya Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, wakituhumiwa kula njama za kutaka kumdhuru DC huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amezungumza na JAMHURI na kusema, “Bado uchunguzi unaendelea. Mambo mengine yatajulikana mahakamani.”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe, amejiweka kando kwenye tukio hilo, akisema lipo kwa Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa.

Wilaya ya Tarime imekuwa na migogoro mingi ya uongozi, kiasi cha viongozi wa CCM kupendekeza kwenye mamlaka ya uteuzi kumwondoa Luoga.

Kuna mvutano wa matumizi ya Sh. milioni 214 zilizotolewa na mgodi wa Acacia North Mara kwa ajili ya kuandaa mashamba ya miwa. Pia kuna sintofahamu inayohusu Sh. milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kituo cha Afya Nyamwaga. Fedha hizo zinadaiwa kuingizwa kwenye akaunti zisizohusika, huku lawama zikielekezwa kwa DC.

“Hatuna hakika juu ya uhusiano wa mvutano huu na kutekana kunakoanza kujitokeza, lakini Tarime kuna matatizo. Tunasikia Rais Magufuli anakuja, huenda akasaidia kumaliza tofauti hizi,” kimesema chanzo chetu.

Mkuu wa Mkoa Malima amefafanua hivi: “Kulikuwa na watumishi wa Serikali wa Idara ya Usalama wa Taifa. Wamesimama pale, kwenye kituo chake kutia mafuta na baadaye ikaonekana kwamba watu wawili walishuka kwenye gari.

“Bwana Zakaria alitokea pale kwake na ikatokea milio yenye sauti ya bunduki, na ikatokea pale, kwamba maafisa wa Usalama wamepigwa risasi, na kwenye gari kulikuwa na maafisa wengine wa Usalama wa Taifa na kwa sababu walikuwa kwenye biashara halali, walikuwa kwenye ratiba za kikazi, walitoka kwenye gari na wakamdhibiti yule Bwana Zakaria.

“Lakini tayari wakati huo maafisa wawili tayari walikuwa wamekwishapigwa risasi wakamkamata yule bwana, wakampeleka polisi.”

Amesema askari wawili waliopigwa risasi mmoja amejeruhiwa vibaya na wote wawili wamelazwa hospitalini kwa matibabu. Ameongeza kuwa ametoa kauli hiyo baada ya kubaini kuwa kulikuwapo jaribio la baadhi ya vijana kufanya fujo pale Tarime.

Amehitimisha kwa kusema kuwa Zakaria yupo mikononi mwa polisi, huku taratibu za matibabu zaidi kwa askari hao wa Usalama wa Taifa zikiwa zinaendelea na mambo mengine yatajulikana mahakamani.

Taarifa zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilionyesha kuwa Zakaria angefikishwa mahakamani muda wowote kuanzia jana.

 

.atamati…