Mkakati maalumu wa kuiua Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) unaohusisha kukodisha reli kwa shirika binafsi umefichuliwa, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini.

Pamoja na kukodisha reli, kiwanda cha kuchakata kokoto cha Kongolo, mali ya mamlaka hiyo kinatafutiwa ‘mnunuzi’.

Uchunguzi wa miezi mitatu wa Gazeti la JAMHURI umebaini kuwa njia ya reli ya TAZARA imekodishwa kwa Kampuni ya Calabash kutoka Afrika Kusini. Kampuni hiyo ndiyo sasa inasafirisha shehena kwa kutumia mabehewa na vichwa vyake (injini).

Tangu Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Bruno Chingandu, ashike madaraka hayo kumekuwepo jitihada za makusudi za kuiua mamlaka hiyo inayozihusisha nchi mbili za Tanzania na Zambia.

Chanzo hicho kimesema kitendo cha kukodisha njia ya reli kwa kampuni binafsi kimelenga kuidhoofisha TAZARA.

“Kimsingi TAZARA inatakiwa kufanya kazi baina ya nchi mbili, treni zibebe shaba kutoka Zambia kuja Bandani ya Dar es Salaam, lakini kiasi kinachosafirishwa ni kidogo sana ukilinganisha na uwezo wa reli yetu. Hapo kuna shida ya uwekezaji baina ya wadau ambao ni Tanzania na Zambia.

“Sasa tumeshangaa kuona treni za Calabash ambazo zinatokea Afrika Kusini zikianza kufanya kazi ambayo kimsingi inatakiwa kufanywa na TAZARA… hapa kuna hujuma kubwa, ninaiomba serikali iingilie kati, tunakwenda kuua kabisa shirika hili kwa kuwanufaisha wageni,” kimesema chanzo chetu.

 Chanzo kingine ndani ya TAZARA kimesema treni za Kampuni ya Calabash zimekuwa zinabeba shaba kutoka Zambia hadi Dar es Salaam na kuondoka na mbolea aina ya sulfur kwenda Zambia.

“Nimesikia hao ‘makaburu’ wanalipa hadi Sh milioni 2 kwa behewa moja kutoka Zambia hadi Dar es Salaam, hapo tatizo si hao makuburu, bali ni mkakati mahususi unaoasisiwa na menejimenti iliyoko chini ya Wazambia wakitaka kuua kabisa TAZARA.

“Kuna maneno hapa kwamba mmoja wa viongozi wa juu wa TAZARA amewahi kufanya kazi katika kampuni moja nchini Afrika Kusini, ana masilahi na Kampuni ya Calabash…hapa tunahitaji serikali ifanye uchunguzi na ikibainika waondolewe.

“Serikali ya Rais Magufuli si ya kuchezewa na hawa ‘vibaraka wa makaburu’, kinachotakiwa hapa ni kuiwezesha TAZARA kufanya kazi yake kwa ufanisi. Tunaweza kufika huko kama wadau watatoa kipaumbele kwenye reli ya TAZARA, Serikali ya Tanzania imekuwa inatoa michango yake, ila Zambia mmhh!” kimesema chanzo chetu.

 Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Bruno Chingandu, ambaye ni raia wa Zambia, amezungumza na JAMHURI na kukiri kuikodosha njia ya reli kwa Kampuni ya Calabash, akidai kwamba uwezo wa TAZARA ni mdogo.

 “TAZARA hatujaikodisha kwa Calabash ila tumewaruhusu kutumia njia yetu, uwezo wa njia yetu ni kubeba tani za ujazo milioni 5 kwa mwaka, lakini uwezo wetu ni tani za ujazo 220,000 kwa mwaka, huku tukiacha ujazo huo mwingine bila kutumika kutokana na uhaba wa mizigo.

 “Wakati reli ya TAZARA ikiwa ‘imechanganya’ mwaka 1977/1978 ilisafirisha tani za ujazo milioni 1.3; kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tena, kwa sisi kumruhusu mtumiaji mwingine tunajaribu kutumia kiwango kile ambacho hakitumiki ili kutengeneza fedha.

 “Hali hiyo inasaidia kuondoa ongezeko la mizigo kwenye barabarani na kuletwa kwenye reli, tunaokoa barabara zetu. Kiuchumi Tanzania inanufaika zaidi kwa mizigo ambayo inapelekwa katika Bandari ya Dar es Salaam,” anasema Chingandu.

Jambo jingine ambalo uchunguzi wa JAMHURI umebaini haliendi sawa ni kutopelekwa kwa michango ya hifadhi ya jamii; hali inayofifisha morali ya wafanyakazi.

 Mamlaka hiyo inadaiwa mabilioni ya shilingi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Mamlaka hiyo inadaiwa takriban Sh bilioni 18 ambazo ni malimbikizo ya miaka 10 kuanzia mwaka 2008. Takwimu zinaonyesha kuwa wamejikongoja na kulipa Sh bilioni 3.9 pekee katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kutokana na usumbufu wa kulipa michango ya NSSF kumekuwapo makubaliano ya TAZARA na NSSF yanayoitaka mamlaka hiyo ilipe Sh milioni 150 kila mwezi hadi deni litakapomalizwa. Endapo malipo yatakuwa ya kasi hiyo, TAZARA itahitaji miaka 13 kumaliza deni hilo.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Chingandu unadaiwa kutoa waraka unaozuia kufanya matengenezo ya vichwa vya treni. Habari za ndani zinasema Serikali ya Tanzania imeingiza zaidi ya Sh bilioni 10 za matengenezo ya vichwa hivyo.

Akijibu madai hayo, Chingandu anasema taarifa kuhusu suala la kutoa mwongozo wa kuzuia ukarabati si za kweli. Anasisitiza kwamba TAZARA wanaendelea kufanya ukarabati kama walivyotakiwa na Serikali ya Tanzania.

 “Taarifa hiyo si kweli, hakuna maelekezo yoyote kutoka ofisini kwangu yanayozuia ukarabati wa vichwa vya treni. Hadi sasa ukarabati unaendelea,” anasema Chingandu.

 Kuhusu suala la kutolipa michango ya hifadhi ya jamii, anakiri kwamba kumekuwapo matatizo kwenye uwasilishaji michango hiyo ya kisheria. Anakiri pia kumewapo kwa makubaliano maalumu kati ya TAZARA na NSSF ya kulipa kiasi fulani cha fedha kila mwezi.

“Changamoto za kifedha ambazo zinaikumba TAZARA zimesababisha taasisi kushindwa kuwasilisha michango yake kama sheria inavyotaka. Tumeshindwa kupeleka NSSF michango ya wafanyakazi, TAZARA haizalishi fedha za kutosha ili kumudu kulipa michango yote ya kisheria.

“Hata hivyo tumeingia makubaliano maalumu na NSSF, tumekuwa tukiwalipa Sh milioni 150 kwa mwezi ili kupunguza deni letu, tumekuwa tukifanya hivyo tangu mwaka 2016 hadi sasa. Kupitia utaratibu huu tumewalipa Sh bilioni 3.9,” anasema Chingandu.

Kuhusu suala la kiwanda cha kuchakata kokoto cha Kongolo kilichoko Mbeya, Mkurugenzi Mtendaji huyo anasema hakijauzwa, isipokuwa wametafuta mwekezaji watashirikiana naye.

“Hatujampatia mwekezaji yeyote mgodi wa kokoto wa Kongolo, isipokuwa tumesaini hati ya makubaliano na mdau mwingine ambaye tutashirikiana naye kuhakikisha tunauendesha mgodi huo vizuri na kwa ufanisi zaidi,” anasema Chingandu.

Waziri azungumza

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe, ameliambia JAMHURI kuwa kitendo cha uongozi wa TAZARA kuingia ubia na mwekezaji katika mgodi wa kokoto wa Kongolo hakikubaliki.

 “Pale Kongolo, ule mgodi una mali ambayo iko tayari kwa matumizi, tena zile kokoto wala huhitaji kutafuta soko maana mteja mkubwa ni TAZARA yenyewe, sitakubali kuona panabinafsishwa kwa namna yoyote ile.

“Nimetembelea eneo hilo hivi karibuni na nikakuta moja ya mashine imeharibika na nikatoa maelekezo kifaa hicho kiagizwe kutoka nchini Italia, naamini maelekezo yangu yatafuatwa, lakini pia hilo jambo la hayo makubaliano siliafiki na nitawataka maelezo TAZARA,” amesema Kamwele.

 Kuhusu TAZARA kukodisha njia ya reli kwa Calabash, amesema jambo hilo amelifuatilia kwa karibu sana na tayari ameshawasiliana na mamlaka za juu.

“Jambo hilo ninalifahamu vizuri, siwezi kusema chochote maana nimeshawasiliana na mamlaka ya juu. Itoshe tu kusema nimesikia wamekodisha,” anasema Mhandisi Kamwelwe.

 Kuhusu TAZARA kwa ujumla wake, Waziri Kamwelwe, anasema kumekuwapo changamoto za muda mrefu, huku akisema kuna masuala ambayo serikali imeyapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuiboresha zaidi mamlaka hiyo.

 “Kuna masuala ambayo yanashughulikiwa na AG (Mwanasheria Mkuu), kwa mfano tangu shirika limeanzishwa mwaka 1975, tangu kuanzishwa kwake wakurugenzi wakuu wamekuwa wakitoka Zambia tu,” amesema.

 Uchunguzi wa JAMHURI umebaini pasi na shaka kuwa wafanyakazi hawalipwi muda wa ziada wa kazi; huku baadhi ya mameneja wakikaimu nafasi hizo. Hata wanapostaafu wanabakizwa kwa mkataba.

 Kilichobainika nyuma ya pazia kuhusu watumishi hao kukaimu na wanapostaafu kubakizwa ofisini, ni kuhakikisha mrija wa ‘kuifyonza’ TAZARA haukomi.

Akijibu hoja hizo, Chingandu anasema TAZARA haijasimamisha malipo ya muda wa kazi wa ziada. Awali ilidaiwa kuwa waliosimamishiwa malipo hayo ni wafanyakazi wa idara ya operesheni, lakini yeye anasema TAZARA imeweka mifumo ya kudhibiti muda wa ziada.

Anasema muda huo wa ziada wa kazi ni lazima upitishwe na msimamizi na upate kibali cha Mkurugenzi Mkuu au Meneja wa Kanda.

Historia ya Reli ya TAZARA

Reli ya TAZARA ambayo pia huitwa Reli ya Uhuru (Uhuru Railway) ilijengwa kati ya mwaka 1970 na 1975 kwa lengo la kuipa nchi ya Zambia iliyokuwa haina pwani ya bahari ‘kiunganisho’ hadi Bandari ya Dar es Salaam kama njia mbadala ya kusafirisha bidhaa zake zilizokuwa zikipitia Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika Kusini na Msumbiji.

Nchi hizo zilikuwa bado chini ya utawala wa kikoloni na/au Wazungu wachache huku mapambano ya kudai uhuru yakiendelea. Kwa upande wa Tanzania, lengo lilikuwa ni kusukuma maendeleo katika maeneo ilimopita reli hiyo.

Hivyo mradi huu tayari ulikuwa na soko kuhusu matumizi yake (turnkey project) na uliwezeshwa na kugharimiwa na fedha kutoka Jamhuri ya Watu wa China. Ujenzi wake uligharimu dola milioni 500 za Marekani kwa wakati huo. Kiasi hicho kiliufanya mradi huo kuwa mradi mkubwa China – nje ya nchi hiyo.

Historia yake ilianza Julai 1, 1965 wakati ambao China ilitoa ahadi madhubuti kwa Serikali za Tanzania na Zambia ya msaada wa pauni milioni 150 kugharimia reli hiyo.

Septemba 6, 1967 makubaliano yalitiwa saini jijini Beijing – yakishirikisha mataifa matatu – China, Tanzania na Zambia. China ilijitolea kujenga reli hiyo katika mkopo usio na riba ambao ulipangwa kulipwa katika muda wa miaka 30.

Ujenzi ulianza mwaka 1970 na usafiri wa reli hiyo ulianza baada ya miaka sita. Reli ilianzia Bandari ya Dar es Salaam na kupitia ardhi ya Tanzania mwelekeo wa kusini-magharibi. Ilipita katika maeneo mengi yasiyokuwa na makazi ya watu, huku milima ikipasuliwa ili kupitisha reli.

Tangu ianze kazi kumekuwapo maendeleo ya viwanda katika maeneo ilikopitia, pamoja na mtambo wa uzalishaji umeme wa Kidatu na Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi (SPM Mgololo).

Reli inapishana na barabara kuu ya kwenda Zambia karibu na mji mdogo wa Makambako na inakwenda sambamba nayo hadi Mbeya hadi Tunduma – mpakani mwa Zambia na inaingia Nakonde, Zambia hadi Kapiri Mposhi. Umbali kutoka Dar es Salaam hadi Kapiri Mposhi ni kilometa 1,860.

3048 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!