DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Paul Koyi, ametoa wito kwa vijana wanaojishughulisha na biashara kujiunga na chemba hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara yake Makao Makuu ya Kampuni ya Salim Prefarb Housing Limited (SPH) yaliyopo Shekilango, Dar es Salaam, Koyi ameonyesha kufurahishwa na jitihada za maendeleo zinazofanywa na vijana wabunifu wa Kitanzania.

“Mnaonyesha namna mawazo chanya yanavyoweza kutumika kuwainua vijana, na kwa hakika, kijana akisema ‘hakuna kazi’ huo ni uvivu,” anasema Koyi.

Koyi amewasihi SPH kuingia uanachama na TCCIA waweze kupata faida zitakazoikuza kampuni hiyo ambayo ina muda mfupi katika biashara, na kuiongezea thamani.

“Kuwa mwanachama wa TCCIA kuna faida nyingi. Zipo faida za kimtandao na utangazaji za huduma zenu kwa wadau na wateja mbalimbali kupitia chemba hii,” anasema.

Aidha, amedokeza kuwapo mradi mpya ulioidhinishwa hivi karibuni ukilenga kuwajengea uwezo vijana mbalimbali kujifunza stadi na ufundi

Anasema SPH inaweza kuwa mahala sahihi kusimamia mradi huo, ikiwamo kuwajengea uwezo vijana watakaochaguliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Salim Salim, anasema ziara ya Koyi ofisini hapo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano baina ya SPH na TCCIA.

“Kuhusu uanachama, bila shaka tutajiunga mapema sana na mara moja tutaanza kujihusisha na shughuli mbalimbali za TCCIA katika kutanua wigo wa masoko na uwekezaji katika soko la ndani na nje ya nchi,” anasema Salim.

SPH ni kampuni inayoendeshwa na vijana Watanzania waliojikita katika utengenezaji wa ujenzi mbadala wa nyumba kwa ajili ya makazi na ofisi, hususan katika maeneo ya miradi mbalimbali.

By Jamhuri