DODOMA

Na Lusungu Helela, WMU

Kampuni ya Kitanzania ya Bushman Hunting Safaris imekuwa ya kwanza kwenye tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini kushinda na kukabidhiwa mkataba wa Uwekezaji Mahiri katika Maeneo ya Wanyamapori (SWICA).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, akikabidhi hati kwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Talal Abood, mwishoni mwa wiki. 

Amesema uwekezaji huo wa kimkakati unalenga kuingizia fedha nyingi serikalini kupitia maeneo ya wanyamapori yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Kampuni ya Bushman Hunting Safaris imepata mkataba unaoiwezesha kuwekeza katika Kitalu cha Uwindaji cha Maswa North baada ya kuzishinda kampuni nyingine kenda.

Uwekezaji huo wa kimkakati unatoa muda mrefu kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya wanyamapori kwa miaka 30, muda ambao unamwezesha mwekezaji kuwekeza bila hofu ya kuondolewa na kukabidhiwa mwingine. Awali, muda wa uwekezaji ulikuwa miaka mitano tu.

Dk. Ndumbaro anasema uwekezaji huo ni mpya na utasaidia katika ustawi wa uhifadhi na kuongeza mapato maradufu serikalini, na umezingatia wawekezaji wa ndani. 

Mwekezaji wa ndani anatakiwa kuwa na mtaji wa kuanzia walau dola milioni 10 za Marekani (Sh bilioni 23). Wawekezaji kutoka nje ya nchi wanatakiwa kuwa na mtaji wa walau dola milioni 50 za Marekani (Sh bilioni 116).

Kampuni za Watanzania zitakazoungana (Joint Venture) zinatakiwa kuwa na mtaji wa chini wa kuanzia dola milioni 20 za Marekani ambazo ni wastani wa Sh bilioni 46.

Mkurugenzi wa Bushman Hunting Safaris, Talal, anasema Agosti 5, mwaka huu inabaki kuwa siku ya kihistoria kwa kampuni hiyo, na kwamba yuko tayari kuwekeza na kutimiza dhamira ya serikali ya kuongeza mapato kupitia SWICA.

Amempongeza Waziri Ndumbaro, TAWA na watendaji ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kuitambua Kampuni ya Bushman na kuipa mkataba baada ya kujiridhisha kuwa imetimiza vigezo vyote vinavyotakiwa kikanuni na kisheria.

Anasema hatua hiyo inapeleka ujumbe kwa wawekezaji wazawa kuwa wizara haina ubaguzi, kwani kumekuwapo dhana potofu kuwa wanapendelewa wawekezaji kutoka nje.

Dk. Ndumbaro amesisitiza kuwa uwekezaji huo ni wa kimkakati unaowapa fursa wawekezaji kufanya uwekezaji unaozingatia uhifadhi, ujenzi wa hoteli za hadhi ya juu, zikiwamo hoteli za nyota tano na aina zozote za uwekezaji ambazo ni rafiki wa uhifadhi.

Aina hiyo ya uwekezaji inatoa fursa kwa wawekezaji kuendesha aina zote za utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.

Anasema aina ya uwekezaji huo ina manufaa kwa mwekezaji na serikali pia. Amehadharisha kuwa pamoja na kufanya biashara, lengo kuu la kwanza kwa wawekezaji katika vitalu watakavyokabidhiwa ni kuhakikisha uhifadhi unapewa kipaumbele.

“Tunawahitaji mno wawekezaji kuwekeza katika maeneo hayo ya wanyamapori, lakini jambo la kwanza ni uhifadhi na jambo la pili ndio uwekezaji,” anasema Dk. Ndumbaro.

Waziri ametoa siku 60 kwa TAWA kuwasilisha majina ya vitalu vya uwindaji wa kitalii ambavyo wamiliki wake wameshindwa kudhibiti ujangili, na walioruhusu mifugo kuchungia maeneo ya hifadhi. Anasema hatasita kufuta leseni za kampuni zote zilizoshindwa kusimamia uhifadhi katika maeneo hayo.

Dk. Ndumbaro ameipongeza TAWA kwa kubuni wazo la Uwekezaji Mahiri na kulitengenezea kanuni. Anasema imekuwa taasisi ya kwanza kati ya taasisi 17 zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na aina hiyo ya uwekezaji.

Kutokana na mafanikio hayo, amezipa siku 25 taasisi nyingine kufanya hivyo. Taasisi hizo ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Ametaka ifikapo Septemba 30, mwaka huu ziwe zimekamilisha kanuni za Uwekezaji Mahiri katika maeneo yao.

Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi, amesema wazo la uwekezaji mahiri walianza kulifanyia kazi mwaka 2018 kwa kulenga kampuni na watu mashuhuri wenye mitaji mikubwa.

Misungwi anasema Kampuni ya Bushman Hunting Safaris ni miongoni mwa kampuni 10 zilizoshindanishwa zikiwania kitalu cha uwindaji cha Maswa North na hatimaye ikashinda. Miongoni mwa kampuni zilizoshindwa ni za Marekani.

By Jamhuri