Timu ya Taifa ya Tenisi inayoshiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15, imeondoka leo kwenda Nairobi, Kenya kushiriki mashindano ikiwa na matumaini ya kushinda.

Mashindano hayo yatatimua vumbi kuanzia Agosti 8 hadi 15, mwaka huu nchini humo.  Timu hiyo inaundwa na wachezaji wanane kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.  Wachezaji hao ambao wameambatana na Kocha wao, Kiango Kipingu, ni Shadya Kitenge, Jackline Kayunga, Khalfan Peter, Adam Mwambungu, Emanuel Mallya, Omary Sule, Frank Menard na Martina Jonnah.

Kipingu aliwaambia wanahabari Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa vijana hao wamejiandaa vyema, na kuwa wana uhakika wa kufanya vizuri katika mashindano hayo.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi kwa muda mrefu, kwa hiyo vijana wetu wako katika hali nzuri na tayari kabisa kwa mashindano,” alisema Kipingu.

Awali, Chama cha Mchezo wa Tenisi Tanzania (TTA) kiliandaa mashindano ya vijana ili kupata wachezaji wa kuunda timu hiyo. Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Morogoro.

Kwa mujibu wa Kipingu, waliamua kuchagua wachezaji kutoka Dar es Salaam na Arusha kwa vile ndiyo walioonesha viwango vya kuridhisha.

Mashindano ya Tenisi ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana yameandaliwa na Shirikisho la Mchezo wa Tenisi Duniani (ITF), kwa kushirikiana na Shirikisho la Tenisi Afrika Mashariki (CAT). Wachezaji watakaoshiriki katika mashindano hayo wanatoka katika nchi za Ethiopia, Rwanda, Burundi, Sudan, Uganda, Djibouti, Tanzania na wenyeji Kenya.

Wachezaji wataanza kuhesabiwa pointi za ushindi katika hatua ya robo fainali. Washindi watapandishwa viwango na pia watapata nafasi ya kwenda kujifunza mbinu za mchezo wa tenisi kwa kiwango cha kimataifa, katika shule zilizoko sehemu mbalimbali duniani chini ya usimamizi wa ITF.

Historia inaonesha kuwa Tanzania imekuwa ikishiriki mashindano ya tenisi ya kimataifa kwa takriban miaka mitano mfululizo bila mafanikio. Kipingu alisema mashindano hayo ni changamoto kwa uongozi mpya ulioingia madarakani hivi karibuni.

“Hii ni moja ya changamoto tulizonazo sisi kama uongozi mpya, ambao umeingia madarakani hivi karibuni, lakini nina imani kuwa tutafanya vizuri kwa sababu maandalizi tuliyoyafanya yanaridhisha.” alisisitiza.

Hivi karibuni, TTA ilifanya uchaguzi mkuu na kupata viongozi wapya ambapo Mwenyekiti ni Matsusela Mbanjo, Makamu Mwenyekiti ni Fina Mango. Kamati ya utendaji inaundwa na Ismail Omary, Mohamed Hamis, Kiango Kipingu, Majuto Omary, Ismail Hemed na Johua Mazila.

Uongozi ulioondolewa madarakani ulikuwa chini ya Mwenyekiti Denis Makoyi na katibu wake, Inger Njau.


By Jamhuri