NA MICHAEL SARUNGI

Kufanya vyema kwa timu za taifa za vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes, na ile ya chini ya miaka 17 Serengeti Boys katika michezo yao ni mwendelezo wa matokeo mazuri kwa timu za taifa za vijana barani Afrika.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wadau wa mchezo huo nchini wamesema matokeo hayo ni mwendelezo wa kile ambacho kimekuwa kikifanywa na vijana wengine kutoka mataifa mbalimbali barani humu.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu ya Singida United, Yussufu Mwambani, amesema mara nyingi timu za vijana hapa nchini ndizo zimekuwa zikiwafariji Watanzania linapokuja suala la michezo ya kimataifa.

Amesema changamoto kubwa inayozikumba timu hizo ni wengi wa wachezaji hao kupotelea kusikojulikana mara wanapomaliza majukumu yao katika timu za taifa hali ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwa TFF na wadau wengine.

Amesema hii ni changamoto kubwa inayohitaji kufanyiwa kazi kwa ushirikiano wa pamoja kati ya wadau wote wa michezo hapa nchini, Shirikisho la Mpira nchini Tanzania (TFF) na Serikali.

Amesema tatizo hili limekuwa likiigharimu TFF kwa kuingia katika gharama zingine za kutafuta vipaji vingine wakati mashindano mengine ya kimataifa yanapokaribia, hali inayohitaji kufanyiwa kazi kwa uangalifu.

Amesema vijana wengi wa Afrika wanatoka katika familia maskini hivyo kushindwa kumudu gharama mbalimbali za kujikimu ili wafike mbali katika kuendeleza vipaji vyao hali inayohitaji kufanyiwa kazi na mamlaka husika.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Hasanoo amesema timu za taifa za vijana hapa nchini na Afrika kwa ujumla zimekuwa na tabia za kufika mbali katika michuano mikubwa duniani.

Amesema kibaya ni kuwa wamekuwa wakipotea kwa kushindwa kupata nafasi katika timu wakubwa na kukosa mwendelezo mzuri wa kuendeleza vipaji vyao jambo ambalo limekosa tiba kwa kipindi cha miaka mingi.

Amesema mfano, Nigeria mwaka 1996 ilifanya vyema na kikosi chake cha U23 katika michuano ya Olympic kwa kuibuka na medali ya dhahabu ikiwafumua vigogo wa soka duniani, Brazil na Argentina.

Amesema hata kikosi cha U17 cha Timu ya Taifa ya Ghana maarufu kama ‘Starlets’ waliibuka mabingwa katika michuano ya kombe la Dunia mwaka 1991 na  1995, pia wakiingia hatua ya fainali 1993 na 1997.

Hasanoo amesema pamoja na timu hizo za vijana  kufanya vyema, lakini vyama vya michezo vimeshindwa kuwa na mwendelezo mzuri wa kuvilinda vipaji hivyo kwa manufaa ya timu za wakubwa.

Amesema pamoja na mafanikio hayo ya timu za vijana ndani ya bara hili lakini hali imekuwa ni tofauti kwa kaka zao kwa miaka mingi na rekodi pekee ni ile ya timu ya taifa ya Cameroon kufikia hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la dunia mwaka 1990 na Senegal 2002.

Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismail Rage amesema vijana wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonyesha jitihada kubwa na wanastahili pongezi lakini cha kujiuliza ni juu ya hatima yao baada ya michuano hiyo.

Amesema Tanzania imekuwa na bahati ya kuwa na vijana wenye vipaji na uwezo wa kuzisaidia timu za taifa, lakini wamekuwa hawapati nafasi katika vilabu na hata timu za taifa za wakubwa na kuishia mitaani.

Amesema mara nyingi nguvu kubwa imekuwa ikitumika wakati wa kuwatafuta wachezaji wa timu za vijana wenye umri wa miaka 17 hadi 20, lakini baada ya mashindano vijana hao hutelekezwa na kuishia kusikojulikana.

Kocha Mkuu wa Norongoro Heroes, Ammy Ninje amesema kupotea kwa vijana wenye vipaji mara baada ya michuano ya kimataifa inachangiwa na vitu vingi sana vinavyohitaji kufanyiwa kazi na wadau wote.

Amesema kwa mtazamo wa haraka haraka watu wengi wamekuwa wakiilaumu TFF lakini wanashindwa kuelewa kuwa shirikisho hilo halina klabu ya kuweza kuwasajili wachezaji hao, kinachotakiwa ni vilabu kuanza kuwamulika vijana hawa.

Amesema nchi zilizoendelea zina utamaduni mzuri wa kulea vipaji kwenye akademi kama kuingia mikataba na vijana hao wakiwa bado wadogo kitu kinachowafanya kusimamia maendeleo yao na mwisho wa siku kupata timu bora za wakubwa.

Ngorongoro Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Afrika za Vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger, Novemba mwaka huu baada ya ushindi wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90.

Nayo timu ya taifa ya Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi na kuendeleza furaha ya Watanzania  na wapenzi wa soka.

1037 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!