Juni 5, 2021 Msemaji Mkuu wa Serikali, Geryson Msigwa, ametoa taarifa ya mwenendo wa kazi za serikali, utekelezaji wa ahadi zake na eneo muhimu la ukusanyaji mapato.

Msigwa ameonyesha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuongeza makusanyo hata baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzuia alizoziita ‘kodi za damu’ Aprili 6, 2021.

Rais Samia amefanya mabadiliko makubwa TRA kwa kumwondoa Kamishna Mkuu, Dk. Edwin Mhede, ambaye amepelekwa katika mradi wa Mabasi ya Mwendokasi (DART). Amewaondoa makamishna kadhaa, pia na kumteua Alphayo Kidata kuwa Kamishna Mkuu.

Katika taarifa yake, Msigwa amesema: “Ukusanyaji wa kodi unakwenda vizuri, na serikali inawapongeza Watanzania wote kwa kuitikia wito wa kulipa kodi. Kodi ni maendeleo.

“Mwezi Jan 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.68, makusanyo Tril. 1.34 sawa na asilimia 79.8; mwezi Feb 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.61, makusanyo Tril. 1.33 sawa na asilimia 82.9; mwezi Machi 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.99 makusanyo Tril. 1.67 sawa na asilimia 84.1; mwezi Aprili 2021: malengo yalikuwa Tril. 1.61 makusanyo Tril. 1.34 sawa na asilimia 83.2 na mwezi Mei 2021: Malengo Tril. 1.619 makusanyo yalikuwa Tril. 1.33 sawa na asilimia 82.

“Serikali inakusanya kodi kama kawaida kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na kutoa huduma kwa wananchi, ikiwamo kugharamia mishahara, kuhudumia deni la taifa, kugharamia miradi ya maendeleo.”

Sisi tumefarijika mno kwa takwimu zilizotolewa. Ukiangalia kwa takwimu za makusanyo, hata hofu aliyoionyesha Rais Samia kuwa pengine kwa kuwazuia TRA ‘wasikusanye kodi za damu’ makusanyo yangeshuka kidogo, hili halikutokea.

Kwa takwimu hizi, makusanyo yameendelea kuongezeka. Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, mwezi uliopita aliwaambia wahariri mjini Morogoro kuwa akaunti zote za wafanyabiashara zilizokuwa zimefungwa zimefunguliwa.

Mheshimiwa Rais Samia, tunaomba kukwambia kuwa sisi tunaishi mitaani. Hakika utakusanya kodi hadi ushangae. Watu wako tayari kulipa kodi, ila si kwa kuporwa kama walivyokuwa wanafanya TRA hadi Machi, mwaka huu.

Kwa taarifa yako, maduka yameanza kufunguliwa tena. Ujenzi umeanza kufanyika tena. Watu wanakarabati nyumba zao sasa au kujenga nyumba mpya na vibanda vya biashara. Haya ni masuala yaliyokuwa yamefutika.

Biashara ikifunguka katika sekta binafsi, tunaamini TRA watakusanya kodi hadi ushangae. Sisi tunasema ustaarabu huu unaoendelea sasa wa kukusanya kodi bila kutishia watu kupelekwa jela, uendelee na kazi iendelee.

Watanzania wanahitaji kuheshimiwa, kufurahia matunda ya uhuru, badala ya kuishi kwa hofu kama vile nchi ipo chini ya mkoloni. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri