Hayo ndiyo yaliyoongolewa pale Dodoma na mengi mengineyo ndiyo yalitokea wakati ule hali ya hewa ilipochafuka huko Visiwani. Hali ile ilisababisha Mzee wetu Jumbe ajiuzulu uongozi; akaacha Urais wa Zanzibar, akaacha umakamu wa Rais wa Jamhuri na akaacha umakamu wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

 Mwalimu alisema “mpaka leo kuna vitisho Zanzibar”. Ni kweli tunaona kama kule Visiwani watu baada ya uchaguzi ule wa marudiano wa tarehe 20/03/2016 bado kuna hali ya vitisho. Makundi ya watu bado wanaulizwa “mbona mnaacha msimamo? hamjui mambo ya hapa?” Maneno yale ya Mwalimu kuwa mpaka leo kuna vitisho Zanzibar, mimi nayakubali. Inaonekana wenzetu kule visiwani bado wamewagawanyika makundi mawili.

 Wale waliopiga kura ya marudiano tarehe 20 Machi, 2016 na wale wasiopiga kura na wanaosema waziwazi hawaitambui Serikali iliyoko madarakani hivi sasa. Je, hapo pana utulivu na amani miongoni mwa wananchi?

 Imani ya dini yetu sisi wakristo inatupa mwongozo namna hii “kila mtu na atii mamlaka iliyo kuu kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, na ile iliyopo imeamriwa na Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu, nao washindanao watajipatia hukumu. Kwa maana, watawala hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi wataka usimuogope mwenye mamlaka? Fanya mema nawe utapata sifa kwake” (Warumi 13:1 – 3) .

 Mwongozo huu ninauona kama ni sheria ya kuishi kwa amani chini ya Serikali yoyote ile. Lakini kama nilivyotanguliza kusema kwa imani yangu ya Kikristo. Sijui imani za dini nyingine zinasemaje. Ila hakuna mahali tabia ya kisasi ikakubalika kiimani yoyote ile.

Kisasi kinatokea kwa kutunza moyoni maudhi na mabaya, unayotendewa. Hivyo fukuto lake hutokea katika kujiridhisha kisilika. Hapo ndipo mwanadamu anatenda matendo ya kinyama – hivyo kisasi ni “unyama”.

Penye kisasi hakuna msalie mtume. Linatendwa lolote na kwa yeyote hata kiumbe asiyehusika na kukuudhi au kukudhulumu wewe binafsi, hasira za kisasi zitamfikia na kumdhuru tu.

 Watanzania, hasa huko visiwani kwa nini tujiingize katika vurugu namna hiyo? Inajulikana kuwa enzi za utawala wa Sultan (waarabu) wananchi wa asili (watu weusi), wakiitwa “magozi” walidhulumiwa haki zao kama si wananchi. Baada ya mapinduzi sasa inaonekana waarabu wanadhulumiwa haki zao kama si wananchi.  Wanafikia hata wananyimwa haki zao za msingi kama wazanzibari. Huu ndio umekuwa chanzo na asili ya wazanzibar kuwa na hali ya kutoaminiana miongoni mwao.

 Nini basi kifanyike kuondoa kabisa hali hizo za kutokuaminiana? Wazanzibari wakitaka wasitake, wajue wazi kuwa wote Visiwa vile ni vyao. Wote wana haki sawa. Kusema nchi haitolewi kwa vikaratasi au nchi haitolewii mwenye masanduku ni dhana na mawazo yaliyopitwa na wakati, ni mawazo potofu wala hayajengi nchi. Nchi ile wapo wazanzibari wa aina mbili.

 Wapo wazanzibari wale waliozaliwa kabla ya Mapinduzi matukufu ya Januari 1964. Hao ndio wazee waliokuwa katika makundi ya Waarabu, Wahindi, Magoa, Wazungu na watu weusi (Waafrika).

 Wazanzibari hawa mpaka sensa ile ya 2012 idadi yao ilikuwa ni watu 58,331 tu na mpaka leo hii wapo waliotangulia mbele ya haki kwa muumba wao. Basi idadi hiyo sasa imepungua kidogo! Humo wamo akina Maalim Seif, akina Dr. Shein akina Nasoro Moyo akina Brigadia Ramadhani Haki Faki akina Rashid Salim na niseme kwa ujumla wamo karibu wanasiasa wote mpaka kakina mzee Pandu Ali Kificho. Wazee wote wa Zanzibari visiwani idadi yao ndiyo hiyo haizidi watu 58,331. Na haswa imeshapungua kutokana na vifo. Wazee hawa wana umri kuanzia miaka 53 – 100, mimi nawaita wazanzibari asilimia.

Sasa wazee hawa ndio wanaojua machungu yote ya misuguano kati ya makundi makubwa ya wakazi wa kule Visiwani Zanzibar.  Lakini siku zao zinazidi kuyoyoma. Kwa nini wang’ang’anie siasa za malumbano na kuharibu maisha ya vizazi vya leo ambao mimi nawaita ndio Watanzania pyua?

Hawa ndio wale wote waliozaliwa tangu tarehe 26 April 1964 ambao mpaka leo umri wao unakomea miaka 52 tu na kuteremka nchini mpaka aliyezaliwa Aprili mwaka huu. Jamani, Watanzania hawa wako wengi kweli huko Zanzibar.

Kwa mujibu wa sensa ile ya 2012 ilyotolewa rasmi katika buku la sensa “The United Republic of Tanzania, Polulation Distribution by Age and Sex; Volume II, ukurasa 69 – 70, toleo la 2013 kuna hesabu hizi.

Jumla ya wakazi wote Zanzibar ni watu 1,303,569 (mpaka siku ya sensa 2012) mpaka leo hesabu itakuwa imeongezeka). Tuchukulie ile ya sense tu. Wazee wale wa umri kuanzia miaka 53 mpaka 100 idadi yao katika buku lile ilifikia wazee 58, 331 tu. Nguvu kazi ya Taifa, yaani kuanzia wenye umri wa miaka 15 mpaka 52 hawa wako 690,929 na ndio tunawaita wazalishaji uchumi wote wa Taifa lile za Zanzibar. Wapo watoto ambao ni tegemezi tangu aliyezaliwa April ya 2016 hii mpaka yule aliyezaliwa 2004 baada ya tarehe 26 Aprili ndiye ana umri usiozidi wa miaka 14 leo hii na bado tegemezi anasoma skuli (stil under parental care).

Tukijumlisha makundi matatu hayo, wazee akina zilipendwa wapo 58,331. Nguvu kazi ya Taifa Visiwani wapo 690,929. Na watoto tegemezi wapo 554,349. Ndipo tunapata wakazi wa kule visiwani kuwa 1,303,609. Nasema leo imepitwa idadi hiyo. Wako Zaidi maana huu ni mwaka 4 tangu sensa ilew ya mwaka 2012 ifanyike. Huenda leo hii wazanzibar si ajabu wakazidi 1,500,000 hivi.

Swali langu sasa kwa wazee wanasiasa visiwani ni haki kwenu kuwaamulia hatima ya kisiasa hao wakazi 1,245,278? Nani amewapa madaraka hayo? (that mandate)?  Inafaa, tuwape nguvu kazi nafasi wajiamulie mambo yao. Tusiwapakie kasumba za  Uafro  na Uhizbu hao. Wao kwa kweli hawahusiki na mitafaruku ya mipasho katika maisha ya huko Visiwani.

Nimesoma makala ya “Sekeseke za kifo cha Karume” na humo mwandishi Ezekiel Kimwaga, ametoa mwanga kidogo pale alipoandika “Tangu kifo cha Karume maisha ya Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu na Kiasia kwa ujumla yamekuwa mabaya zaidi.

Mahusiano yaliharibika kabisa na hadi leo kuna hali ya kutokuaminiana. Hicho nakiona ni kipengele muhimu sana kwa hali ya Zanzibar kuleta utulivu. Kumbe mtu aliyekuwa wa karibu sana na Mzee Karume, Mzee Rashid Salim angali hai na ndiye aliyeyasimulia hayo, kwa nini Serikali ya Muungano katika kumaliza hali ya kutoaminiana kule visiwani wasimtumie mzee huyu kupata suluhu ya hali ya huko visiwani?

Moja ya matamshi ya Mzee Rashid Salim ni hili, “kati ya makosa yaliyowahi kufanyika Zanzibar, mojawapo lilikuwa ni la kumuua mzee Karume. Athari zake zimekuwa kubwa na watu wengi wasio na hatia wameuliwa”. Hilo sasa lifanyiwe kazi (Sekeseke za Kifo cha Karume; Tazama Raia Mwema Toleo No. 453 la Jumatano Aprili 13 – 19 uk. 13). Wananchi wale 690,929 kweli wanajua hayo? Tusiwasizingie Wazanzibari hawa. Tusiwatilie maneno yetu vinywani mwao. Wao ni wasafi kimawazo.

 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri