Wiki iliyopita Waziri mwenye dhamana katika wizara ya kazi, ajira na maendeleo ya vijana aliwasilisha bajeti ya wizara yake.

Kubwa lililotawala katika hotuba yake ilikuwa ni suala la kutengeneza ajira kwa vijana. Waziri alisema kuwa wamejipanga kutengeneza ajira laki sita katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

 

Hili ni jambo la kupongezwa sana. Kinachonisukuma kuandika uchambuzi huu ni michango ya waheshimiwa wabunge iliyotokana na baada ya hotuba hiyo. Wengi walikuwa wakisisitiza vijana ama kujiajiri au kuwezeshwa kujiajiri.

 

Mara zote ninaposikia hamasa kutoka kwa viongozi kuhusu vijana (na Watanzania kwa ujumla) kujiajiri, huwa napata shida kuhusu mbinu zinazotumika kuhakikisha Watanzania wenye fikra za kuajiriwa wakigeukia kujiajiri. Kimsingi suala la Watanzania kujiajiri linaufumbuzi mkubwa katika kubadilisha fikra zao kushinda hata kuwapatia mitaji na vitendea kazi kama ambavyo wabunge wengi walivyokomalia!

 

Kutokana na suala la kujiajiri lilivyo na mizizi katika fikra, leo nataka kuchambua hali ya mabadiliko ya kidunia kiuchumi na namna inavyoathiri uchumi wa mataifa yetu machanga. Athari za uchumi huu pia zinachagizwa na fikra tulizonazo Watanzania wengi kuhusu maendeleo yetu kiuchumi, hali za viongozi kiuchumi na namna tunavyoburutwa na wenzetu huko duniani!

 

Niseme mapema kuwa msingi wa uchambuzi wangu huu ni kutaka kukuonesha picha halisi ya uchumi na maendeleo yaliyopo duniani kwa sasa; na kutoa hamasa ya kifikra kwa mtu mmoja mmoja. Ni ushahidi usio na chenga kuwa sehemu kubwa ya Watanzania tunafikra za kimasikini, tunaamini katika umasikini na tunabadilika pole pole mno ukilinganisha na mabadiliko ya dunia.

 

Ndio maana huwa nashangaa eti hadi leo hii kiongozi anaehesabika kuwa mwadilifu ni Yule masikini ama mwenye fedha kidogo katika akaunti zake za benki. Mimi ninaamini kuwa mshindi anaweza kuibua washindi wengine na kamwe aliyeshindwa hawezi kuibua mshindi.

 

Kiongozi ambaye amezoea radha ya umasikini katika maisha yake binafsi hana jeuri ya kuongoza wananchi wake kufanikiwa kuwa matajiri ama niseme kuwa na uchumi mzuri. Ninaona ni jambo la maana tena la kulitafuta; kuongozwa na viongozi “washindi”.

 

Najua kuna watu watadhani ninahamasisha viongozi wawe mafisadi, ‘la hasha!’. Tumejenga utamaduni mbaya wa kutegemea viongozi wa kisiasa kutokua matajiri na hadi sasa utamaduni huo unatuliza. Ni kutokana na utamaduni huu ndio maana hadi leo wanasiasa wengi wanaficha thamani ya mali walizo nazo.

 

Na hata wale wanaosema ukweli wanasema kwa shingo upande huku wakisubiri kukosolewa na wananchi waliojaa mitazamo ya kimasikini. Kadiri tunavyotamani viongozi wa kisiasa wawe masikini (ama maisha ya kawaida) ndivyo tunawajengea wigo wa kuchuma mali na kuzificha.

 

Fikra za Watanzania kwa viongozi wa kisiasa nazihusianisha na mfano wa watu waliopewa talanta, 5, 2 na 1. Waliopewa 5 na 2 walizifanyia biashara wakazalisha faida lakini aliyepewa moja aliifukia na baadae akatoa visingizio kibao.

 

Si jambo la ajabu kumkuta mwanasiasa ana mali na utajiri kwa sababu kanuni za kiuchumi zinanithibitishia kuwa mtu akipewa mshahara ama marupurupu na akaamua kuwekeza anaweza kuzalisha mara dufu.

 

Kwa mtazamo huu ni kipi cha ajabu tukisikia kuwa rais ambaye tunamlipa zaidi ya Sh milioni 10 kwa mwezi; anamiliki hoteli ya nyota tano? Utajiri ni mawazo na fedha unayoipata ni kama mbegu, unaweza kula mbegu ama unaweza kutafuta udongo mzuri ukapanda na kuvuna maradufu!

 

Tusipobadili fikra na kuendana na enzi mpya, tunaweza kuandamana tukapigana mabomu na vifaru na kisha baadaye tukawashinda watawala na ‘kuwakimbiza’ huku nchi yetu ikibakia magofu. Watakuja watawala wapya lakini matatizo ya msingi yatakua ni yale yale na bila shaka yatakua yameongezeka zaidi. Kama huelewi ninachokisema kaziangalie Misri, Libya, na Algeria kwa mtini ukajifunze!

 

Nafahamu ninapotaja Misri, Libya na Algeria kuna watu “wanaobubujika upako wa siasa” hao wanaweza kuniambia kuwa chama kilichopo madarakani Tanzania na viongozi wake ni lazima waondolewe ama wavuliwe magamba ili mambo yaende sawa. Pia wapo watakaosema nchi za Magharibi zilizifanyia hila nchi hizi; iwe ni hilo la kwanza ama la pili; sitaki kushughulika nayo.

 

Hapa ninaongelea uchumi, wenye siasa zenu nendeni kwenye miraba yenu ‘mkakomae’ na malalamiko yenu. Kwa sababu mnapopanda malalamiko mtavuna mbegu ya chuki ambayo sumu yake haitawaacha salama hata kama mtatwaa madaraka. (Asomaye na afahamu!)

 

Mambo ni tofauti katika ‘Information Age’ kwani kupata utajiri na mafanikio mengine inakuchukua muda mfupi sana. Inaweza kuchukua masaa 24 tu mtu kuwa milionea au hata bilionea kutokana na nguvu ya taarifa. Kwa kuwa nchi zilizoendelea ziliuona mwezi mapema mwezi wa ‘Information Age’ ndio maana tunashuhudia vijana wa umri mdogo mdogo wakiwa mamilionea kwa muda mfupi.

 

Hili tunajifunza kutoka kwa akina Bill Gates (Microsoft) (Marekani), Mark Zurkeberg (Facebook)-Marekani. Usifikiri ni Magharibi pekee, hata Tanzania tuna mifano ya vijana wanaotoka vyuoni na kuingia katika kujitegemea kwa mafanikio.

 

Vijana hawa wanatumia nguvu iliyopo kwenye ‘Information Age’ tunao mfano kama wa Raymond Maganga mwanzilishi na Mkurugenzi wa DesireMore, Ltd akiwa na miaka ishirini na kidogo anamiliki kampuni hiyo ya teknolojia ya kompyuta na kampuni yake inakua kwa kasi ya ajabu.

 

Leo hii tunavyozungumza kuna wawekezaji wenye mabilioni ya dola ambao wameziweka fedha zao kielektroniki. Wawekezaji hawa (Electronic herd) ambao idadi yao ni maelfu wana nguvu ya ushawishi duniani kuliko hata wanasiasa tunaowachagua.

 

Mathalani, wakiona kuwa nchi haiendeshi vema mwenendo wa sera kulinda fedha na maslahi yao wana uwezo wa kuhamisha fedha ama mitaji yao ndani ya sekunde chache kwa spidi ya mwanga kwa kubonyeza kitufe kimoja tu katika kompyuta zao!

 

Dhoruba kama hii iliwahi kuzikumba nchi za Malaysia, Thailand, Indonesia na Korea mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ukizingatia kuwa tuna wawekezaji wa kimataifa nchini mwetu katika sekta ya fedha na mitaji inayohamishika, jambo hili linaweza kutokea hata kwetu.

 

Kwa maana hii utaona kuwa, serikali zetu zilikua na nguvu ya kudhibiti mambo enzi hizo wakati wa zama za viwanda. Lakini katika enzi hizi mpya, nguvu ya fedha za kielektroniki katika ulimwengu ndio zinazihenyesha nchi zetu.

 

Mchambuzi mwingine anaeheshimika duniani George Soros katika kitabu chake kiitwacho, “The Crisis of Global Capitalism” amebainisha siri yenye kushtusha kidogo. Anasema, “Katika ulimwengu wa ubepari yametokea kampuni kubwa duniani ambazo thamani ya kampuni moja inazidi uchumi wa nchi nyingi za Magharibi.

 

Hii inamaana kuwa kuna kampuni ambazo zinaweza kuvuruga kabisa chumi za nchi kwa ajili ya kulinda maslahi ya kibiashara ama ya wanahisa wachache. Ndio maana hata tunapopigania haki zetu dhidi ya wawekezaji ni vema kama taifa tukawa makini sana. Ukweli ni kwamba kutokana na dunia ya uchumi ilivyo sasa; ukiwaudhi “wawekezaji” hawa wanaweza kuuadabisha uchumi wetu vibaya mno!

 

Ndio maana wakati mwingine kampuni kubwa zinapoingia nchini kufanya biashara ya rasilimali zetu zinakua na nguvu ya kuamua yanachokitaka kinacholeta faida kwao na hazina muda wa kuangalia kinachosemwa na wanasiasa ‘maslahi ya taifa na wananchi’.

 

Kutwa kucha tunalalamika mpaka jasho zinatutoka kukidhani kuwa watawala wetu wanafanya makusudi kuingia mikataba inayodhaniwa ni mibovu ama ya kifisadi. Na kwa sababu tunafikiria ‘ki-industrial age’ (sisi na viongozi wetu) ndio maana hatuishi kuhamasishana kugoma, kuandamana na kupambana na wawekezaji pasipo kufahamu nguvu waliyonayo katika enzi hizi mpya.

 

Simaanishi kuwa tuwaache watuibie, lakini ninaonesha upande mwingine wa sarafu ambao ikiwa tutabadilisha mitazamo na fikra zetu tuna nafasi kubwa ya kuwa washirika badala ya watumwa katika dunia mpya yenye uchumi mpya na mifumo mipya.

 

Nikisema hivi silengi kuwatetea viongozi uchwara, wala rushwa na wazembe (kama wapo nitafurahi hata wakipigwa mawe hadharani); lakini kiu yangu ni kuona mfumo wetu wa kufikiria (personal and national mindset) ukibadilika. Mafanikio ya taifa yatakuja kwa kuwa na mafanikio ya mtu mmoja mmoja na ili tufike hatua hiyo ni lazima mtu mmoja mmoja awe na fikra sahihi kuhusu yeye na taifa lake kiuchumi.

 

0719 127 901 stepwiseexpert@gmail.com

1154 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!