Kati ya viongozi waliowahi kuiongoza nchi yetu na nitakaoendelea kuwaheshimu sana na kuwapenda ni Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Rais Mkapa aliwahi kuwaomba Watanzania wajifunze kuwa na tabia ya kutokuwa na uvivu wa kufikiri. Mara baada ya Mheshimiwa Rais kutoa kauli hiyo alishambuliwa na watu wengi kwamba alikuwa ametukana. Leo hii miaka 10 tangu alipotoa hiyo kauli, naona kwamba kumbe kweli alikuwa yuko sahihi na kwamba moja ya sababu kubwa za matatizo yetu tuliyonayo hayasababishwi na kitu kingine ila sababu kubwa ni uvivu wetu wa kutotaka kufikiri sana.

 

Mara baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda; Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitamka rasmi kung’atuka nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano na kubaki na nafasi ya Mwenyekiti wa CCM. Nchi yetu iliporidhia mfumo wa vyama vingi Mwalimu alitangaza pia kung’atuka uenyekiti wa CCM.

 

Baada ya kutangaza kung’atuka uenyekiti wa CCM akiwa katika kikao cha waandishi wa habari, mwandishi mmoja, Stanley Kamana (marehemu), alimuuliza Mwalimu kama ifuatavyo, “Mwalimu mara baada ya kumalizika Vita ya Kagera ulitangaza kung’atuka urais, sasa hivi nchi yetu imeridhia kuingia katika vyama vingi, unatangaza kung’atuka uenyekiti wa CCM. Je, tukikutafsiri kuwa unaanzisha matatizo na matatizo hayo yanapotokea unakimbia tutakuwa tumekosea?”

 

Majibu ya Mwalimu kwa mwandishi huyo yalikuwa kama ifuatavyo: “Mwenyezi Mungu alikuwa ni mkarimu sana na moja ya mambo aliyothamini sana ni uumbaji wa binadamu, na ndiyo sababu uumbaji wake  aliufanya kwa namna ya pekee tena wa mwisho na siku hiyo ya uumbaji Mungu alitayarisha chombo kilichokuwa na ubongo, na kwa masharti yake kila mmoja alitakiwa achukue ubongo mara moja tu bila kurudia. Basi, na aliyechota kidogo ubongo wake pia ni kidogo hivyo hata uwezo wake wa kutafsiri mambo ni kidogo kwani kila binadamu hutafsiri mambo kulingana na ukubwa wa ubongo wake.”

 

Katika siku za karibuni nchi yetu imekuwa inashuhudia mgogoro kati ya madaktari na Serikali, mgogoro kati ya Chama Cha Walimu na Serikali, mgogoro kati ya wafanyakazi wa migodini na Serikali, na kadhalika.

 

Kwa namna ambavyo kila mmoja amekuwa anachangia mawazo yake wakati wa migogoro hii, mtu utaweza kubaini wazi uwezo wetu wa kuangalia mambo ulivyo. Ukiangalia sana migogoro hii utabaini jinsi nchi hii hapa tulipofikia kuwa ni pabaya sana na itabidi tukae tujiangalie tunakoenda. Ukiona hasa makundi yanayopiga kelele utabaini kuwa ni makundi hasa yaliyopo kwenye sekta ya huduma za jamii ambayo kwa mazingira ya kazi zao hayana mwanya wa kupokea rushwa na hata kama yakilazimisha, basi hiyo rushwa yataipokea kwa tabu sana.

 

Mimi ni mtumishi wa umma kwa miaka 30 sasa, hivyo najua wazi kuwa ni kweli mishahara ya watumishi wa umma inapishana kutoka kada moja hadi nyingine, lakini haipishani katika kiwango cha kutisha sana. Tofauti hii inakuja kuwa kubwa kwa sababu ya rushwa. Sisemi kuwa watumishi wote wa kada zisizolalamika wanakula rushwa la hasha! Wengi wao wana nafuu kwa sababu angalau “one day yes” ipo siku kwani wanaweza kupata mahala pa kupenyea.

 

Nchi yenye rushwa iliyokithiri ina mambo ya ajabu. Hapo DRC enzi za Mobutu Sese Seko ikiitwa Zaire nchi ilifilisika kabisa, lakini askari waliendelea kuwa watiifu kwa Mobutu na hata serikali ilipofikia mahala kwamba haiwezi kuwalipa askari wake kabisa, Mobutu alitaka apunguze jeshi lake ili aweze kuwa na jeshi analoweza kulilipa. Maaskari walimwambia, “Usipunguze ukubwa wa jeshi, wala usitulipe mishahara kabisa, ila tuachie bunduki kila mmoja atajua namna ya kujilipa.”

 

Hapa kwetu tunaelekea huko huko. Mtu atakuwa tayari kufanya kazi yoyote yenye mianya ya rushwa hata kama atalipwa fedha kidogo kabisa au hatalipwa kabisa. Kwa hiyo lazima kwanza tukiri kwamba tunayo matatizo; na kama tunayo matatizo sasa tuambizane  wazi kuwa binadamu hutakiwa kufikiri zaidi wakati wa matatizo ili uamuzi atakaoutumia kutatua tatizo hilo uwe na busara na hekima.

 

Namshukuru Mheshimwa Mbunge wa Kisarawe kwa namna alivyotumia busara kuwasilisha hoja binafsi, ambayo kwa kweli ilijaa busara na namna wa kuishauri serikali kuhusu sheria ya mafao ambayo ilikuwa inatamka wazi kuwa endapo mtumishi ataacha kazi kabla ya miaka 55 au 60, hatarejeshewa michango yake aliyokwishachanga katika mfuko wa jamii anayohusika nayo.

Kwa kuwa alijenga hoja nzuri kabisa Serikali ikamsikiliza na Bunge likaridhia sheria hiyo ipitiwe upya katika kikao cha Bunge cha Oktoba, mwaka huu.  Mbunge mzuri ni anayekuwa daraja kati ya Serikali na vyombo au taasisi mbalimbali kama vile wapigakura na vyama vya kijamii, na kamwe asiyekuwa ukuta.

 

Kadri miaka inavyokwenda sote tunashuhudia machafuko yanavyotokea katika Bara letu la Afrika. Nchi zilizokuwa kisima cha amani sasa zinatisha. Tazama pale Sierra Leone, Liberia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kila mahali panapogunduliwa mafuta, madini balaa tayari, kisa ni nini? Kutogawanya vizuri pato la taifa.

 

Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE  alisema,  “Wengine humwona mwenzao anafanya kosa, badala ya kumwabia pale pale kijamaa kwamba atendalo ni kosa, watanyamaza kimya. Lakini hawanyamazi kabisa! Watakwenda kumteta katika vikundi vya siri siri. Mateto haya si ya kumsaidia mwenzao, ni ya kumdhuru.

 

Hii ni aina mojawapo ya fitina. Wengine hugawa watu katika mafungu. ‘Fulani’ japo akifanya kosa kubwa sana hasemwi. Lakini ‘fulani’ wa pili akifanya kosa japo dogo, kosa lile hukuzwa likawa kama Mlima Kilimanjaro.

 

Hawa hutafuta sababu za kumtetea ‘fulani’ wa kwanza au za kumlaumu “fulani” wa pili ambazo hazifanani kabisa na ukweli. Kwa watu wa aina hii, ukweli ni jambo ambalo hutegemea mtu – si kitu kinachojitegemea chenyewe bila kujali mtu. ‘Fulani’ wa kwanza akisema katika majadiliano kuwa mbili na mbili ni tano, wao watakubali.

 

Lakini ‘fulani’ wa pili akisema sivyo, mbili na mbili nne watamwona ni mtu mbaya kabisa ambaye hastahili hata kusikilizwa. Hawa hawajali ukweli, hujali nafsi tu. Kwao, ukweli ni maono yao na matakwa yao. Hatuna budi, hasa katika majadiliano na mazungumzo yanayohusu jumuiya, tujifunze kusikiliza hoja zenyewe zinazotolewa na wenzetu, na kuijibu zile hoja kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali kama aliyezitoa ni rafiki au si rafiki. Pia wanaopingwa hawana budi wakubali kuwa kinachopingwa ni zile hoja zao, siyo wao wenyewe.

 

Bila mazoea haya, mazungumzo hayana maana; yanakuwa ni kupoteza wakati maana huwa tumekwisha kuzihukumu hoja za mtu hata kabla hajazitamka! Kadhalika, hoja zetu zikijibiwa kwa kupingwa halafu tukawakasirikia waliozipinga tunafanya mazungumzo yasiwe na maana, kwa sababu tunapenda hoja zetu zikubaliwe tu hata kama si hoja safi.”

 

Nimetumia maneno haya ya Mwalimu ili kuelezea dhana potofu inayojengeka katika jamii yetu.

 

Nimesikia wakati wa mgomo wa madaktari baadhi ya watu wanasema madaktari ni halali kugoma na watu ni halali kufa. Masuala ya kufa yanaelezwa hata katika Katiba ya nchi yetu kuwa haki ya kwanza ya binadamu ni kuishi. Hata katika vitabu vitakatifu imeandikwa suala la kutamatisha uhai wa binadamu na alifanye Mungu peke yake. Wakati tunalaani katika  kitendo cha mtu kuua au  au kusabababisha kifo, anaamka mtu mzima kabisa mwenye umri kama wangu anasema, “Kupigwa kwa Dk. Ulimboka ni halali hata kama angelikufa.”

 

Katika hali kama hii ya mgogoro huyo ndiye tunayemtarajia awe daraja kati ya serikali na madaktari. Wapo watu kwa kauli zao na matendo yao wanatia kichefuchefu. Serikali katika dunia yoyote ile huwa inakuwa na umbo au sura ya baba au mzazi.

 

Wakerewe wanao msemo unaosema “mtoto akinyea nguo kinachotupwa ni kinyesi na wala siyo mtoto”. Nashukuru vyombo vya habari kila mara vilitafuta suluhu katika kadhia ya madaktari na Serikali wala havikuwa na chembechembe ya kutaka kutafuta mkosaji ni nani na mshindi ni nani? Wakati tunalaani mgomo wa madaktari hao hao wanafurahia kama kiongozi wao angelikufa. Hawa wakipata madaraka ya kuweza kuua wataua sana.

 

Nikiwa bado nashangaa na kutafakari sakata la madaktari na Serikali ghafla likaja sakata la Serikali na Chama cha Walimu. Waingereza wanao msemo unaosema, “Misfortunes never come singly, they always come in a battalion.”

 

Kwangu nilitarajia tena maelewano na suluhu vitawale. Hilo halikuwezekana. Baadhi ya walimu wakaitikia wito wa chama cha walimu wa kugoma, Serikali ikatumia busara ikaenda mahakamani ikajenga hoja na Mahakama ikaamuru mgomo usitishwe na Chama cha Walimu kikatii.

 

Kwa watu wanaotumia busara na ambao si wavivu wa kufikiri, sasa wangelianza kutuliza munkari wa pande zote mbili kati ya Chama cha Walimu na Serikali. Kwa mara nyingine nishukuru hotuba ya kamati ya Mwalimu Margaret Sitta kwa maneno mazuri aliyoyasoma wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Hawa walikuwa wapatanishi wasiotafuta umaarufu kupitia mgogoro huu.

 

Lakini naomba tena nieleze masikitiko yangu kwa maneno ya mheshimiwa mbunge mmoja aliyesema, “Katiba ya CWT inazungumzia haki na wajibu.” Je, lini alikwishasikia CWT ikawatetea walimu walioshiriki kutoa taarifa potofu hadi wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wakachaguliwa kuingia kidato cha kwanza?

 

Aliwahi kusema mwanasiasa Njellu Kasaka, “Tatizo letu ni kulalamika, kiongozi analalamika, mhudumu analalamika.” Hivi hao walimu waliohusika na njama hizo hatua zipi zimechukuliwa? Hatutarajii viongozi waendelee kulalamika hadharani badala ya kuuambia umma hatua zilizochukuliwa dhidi ya walimu hao.

 

Ipo hadithi moja ya mtu mmoja ambaye alimruhusu jirani yake kuwa anakatisha nyumbani kwake mbali na kuwa lilikuwa ni kosa hakuwahi kulisema hilo kosa hadi siku ambayo jirani yake amemnyima mboga.

 

Hivi watu wa kawaida wangelimwona kuwa anamzuia jirani yake kutumia njia isiyo halali? Au alikuwa analipiza kisasi cha kunyimwa mboga? Sasa hivi tusuluhishe kwa amani mgogoro uliopo kwanza ili baadaye tuoane kama kuna upungufu katika sheria iliyoanzisha CWT ili tusionekane mambo mengine tunayazungumza kwa hila (malice).

 

Madaktari na walimu ni watoto wa Serikali hii hii hata kama wameinyea. Kinachostahili kutupwa ni kinyesi na wala si watoto, hata hao wanaoendelea kutoa uchonganishi wanalijua hili ila wanajitafutia umaarufu tu.

 

Mwalimu Nyerere alisema, “The district commissioner or the regional commissioner who responds to a problem by detaining people – even within his legal powers – is almost always demonstrating his own incapacity for leadership. For it is very rare indeed that a peasant, a small trader, teacher, doctor or craftsman, or a junior official is a danger to the security of the state or to our economic progress.

 

Naamini tatizo la madaktari hawa na walimu hawa ni njaa na watakuwa wanalalamikia tofauti kubwa ya walionacho na wasionacho, hivyo naisihi Serikali isitumie bunduki kuua nzi.

 

Mwandishi wa makala haya Muyemba wa Muyemba ni Mwalimu Mwandamizi aliyeko Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Ni msomaji mwasisi wa Gazeti la JAMHURI. Anapatikana kwa simu 0754 831257/0763 316420/0754 038501/0762 903133.

 

1463 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!