Tumeacha kuheshimu sheria, tumekwisha

Na Deodatus Balile, Johannesburg

 

 

 

Wiki hii nimekuwa hapa jijini Johannesburg. Nimekuja hapa Afrika Kusini kwa nia ya kumuona Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, aliyetekwa, akapigwa, akaumizwa, akatobolewa jicho, akang’olewa meno na kucha. Ametiwa ulemavu wa kudumu. Ni masikitiko makubwa.

Nafahamu si siri tena, Watanzania mnafahamu kuwa Jukwaa la Wahariri liliniteua kuongoza kazi ya uchunguzi juu ya Kibanda kuumizwa. Jumatano ya Machi 17, 2013 gazeti la Mtanzania ambalo hadi Oktoba 2011 nilikuwa Mhariri Mtendaji wake, limetangaza kuwa mimi nikishirikiana na Denis Msacky, Ansbert Ngurumo na Mwigulu Nchemba, tulisuka mpango wa kumteka na kumuumiza Kibanda.

 

 

Sitanii, nimeipokea habari hii kwa masikitiko makubwa. Mhariri wa gazeti hili, Charles Mulinda, ninayemfahamu vyema kwa ubini na matendo yake tangu azaliwe, ameamua kunihusisha na kadhia hii. Sijitetei, na wala sina sababu ya kufanya hivyo. Nimepokea barua pepe, ujumbe mfupi na simu nyingi.

Wengi mnataka kufahamu ni hatua zipi nachukua dhidi ya Mhariri huyu, Gazeti la Mtanzania na Kampuni ya New Habari. Nimeona si vyema mimi kudharau juhudi zinazofanywa na TEF kuhusiana na suala hili. Zipo taratibu za kiutawala kupitia TEF na za kisheria kupitia kwa mwanasheria wangu zinazoendelea sanjari.

Nawaomba nyote mlioguswa tuwe watulivu, ukweli wote utafahamika juu ya kadhia hii na nasema bila kificho, kuwa ikithibitika nilimteka Kibanda, basi vyombo vya dola viniadhibu bila chembe ya huruma, lakini pia ikithibitika kuna japo chembe ya uongo, basi aliyenisingizia ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Baada ya utangulizi huu, niliodhani bila kuligusia suala hili, msomaji wangu ningekuacha katika mashaka makubwa, iwapo unasoma mawazo ya mtu sahihi au la, nirejee katika hoja ya msingi. Kichwa cha makala haya kinasema “Tumeacha kuheshimu sheria, tumekwisha”.  

Nikiwa katikati ya Jiji la Johannesburg Machi 15, 2013 nilishuhudia kitu ambacho Watanzania wengi wanaweza kudhani ni ndoto. Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, akiwa na msafara wake, alikuwa amesimamisha gari kwenye mataa akisubiri iwake taa ya kijani.

Namfahamu vyema Zuma maana wakati Mzee Nelson Mandela anasuluhisha mgogoro wa Rwanda pale Arusha, nilikuwa naripoti mara kwa mara habari hizo, na Zuma alikuwa akimwakilisha Mandela mara kadhaa. Kwa mantiki hiyo, si tu namfahamu Zuma kwa kumuona kwenye picha, bali kwa kiwango cha kupeana mikono.  

Mara kadhaa akija hapa nchini, nimeshiriki kumuuliza maswali akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na moja ya maswali ninayojivunia kumuuliza ni lile la Afrika Kusini kututaka Watanzania tuingie nchini kwao, kwa kupata viza wakati nchi kama Kenya hawadaiwi viza.

Swali hili, hatimaye lilizaa hatua ya kufutiwa viza na hata juzi nilipofika Oliver Tambo International Airport (zamani Johannesburg), niligongewa muhuri wa viza kama vile natoka Kipawa kwenda Mwanza. Nilifarijika kuona ndugu zetu hawa tuliowakomboa, hatimaye wametuheshimu na kutufutia viza.

Nilipouliza kwa mwanasheria mmoja mwenyeji wa Afrika Kusini, kuwa hili ni kawaida alinijibu hivi: “Wala hili si la kushangaza. Sheria inamzuia Rais wa nchi hii kujitenga na watu wake. Kama ni foleni inabidi asimame ajue uhalisia wa maisha ya watu wake.

“Kama ana haraka, sheria inamtaka atumie helikopta. Akijifanya kukimbia zaidi ya spidi 120 iliyoruhusiwa kisheria, magari yote ya msafara yanatozwa faini. Hata polisi, hawaruhusiwi kwenda zaidi ya spidi 120, wakifanya hivyo polisi mwenyewe anayeendesha gari anapigwa fani na kuilipa kwa fedha zake.

“Kama inatokea kuna ulazima kwa kwenda haraka, magari ya msafara yote yanalipishwa faini au wanapeleka utetezi kwenye Halmashauri ya Jiji mara tu baada ya msafara kufika uendako, na kueleza sababu za kwenda kasi au kupita kwenye taa nyekundu.”

 Sitanii, maelezo haya, yaliniacha hoi. Na kweli baada ya taa za kijani kuwaka msafara wa Zuma ulisonga mbele sanjari na magari yetu sisi walalahoi. Hawa wamejiwekea utaratibu na sheria na wanaziheshimu sheria hizi. Je, hapa kwetu linawezekana hili? Msafara au polisi wanaweza kupita kwenye taa nyekundu wakapigwa faini? Tuwasiliane.

 Tanbihi: Makala haya yalichapishwa Aprili 21, 2013