Mwezi huu, Novemba 5, 2018 Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli ilitimiza miaka mitatu madarakani. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Sam Kamanga, amesema Rais Magufuli amesaidia kufufua shirika hilo.

Katika mahojiano na JAMHURI, Kamanga ameeleza kuwa Rais Magufuli amesaidia Watanzania wamekuwa wazalendo, hivyo kuweza kuongeza wateja wa shirika.

Kamanga anasema kwamba rais amesaidia shirika hilo limeweza kushika nafasi ya tano miongoni mwa mashirika ya bima yaliyopo nchini.

“Sasa tuna biashara nyingi kubwa. Tumelikamata soko tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma kwani shirika lilikuwa kama linakufa. Kwa sasa tuna mradi wa bomba la mafuta, ndege yetu – Dreamliner na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa. Haya si mambo madogo,” amesema Kamanga.

Amebainisha kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu NIC imeongeza makusanyo ya ada kutokana na ongezeko la wateja.

“Sasa tunataka kuwa kiongozi wa soko la bima nchini na kuwa kampuni inayotoa suluhisho kwenye sekta ya bima nchini.

Nachukua nafasi hii kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa sababu ya NIC kufanya vizuri ni kutokana na kuwa ni shirika la Kitanzania kwa asilimia 100.

Kabla ya Awamu ya Tano tulikuwa tumedumaa, sasa shirika limechukua zaidi ya asilimia 100 ya wateja waliokuwa wamepotea sasa wamerudi.

Hivyo, nieleze tu kwamba NIC ni shirika la bima la kwanza nchini na hivi karibuni tumetimiza miaka 55 katika soko, jambo ambalo si dogo.

Tutaendelea kuwa viongozi katika sekta ya bima, tunamshukuru msimamizi (regulator) kuanzisha mfumo wa TIRA MIS.

Mfumo wa TIRA umekuja kusaidia zaidi sekta ya bima. Umesaidia kuondokana na udanganyifu uliokuwepo, uliokuwa umekithiri kwenye soko la bima.

Mteja wetu akipata tatizo atafidiwa katika kipindi kifupi baada ya kufuata taratibu zote. Ndani ya siku 45 anakuwa amepata haki yake.

Lengo kubwa tulilonalo ni kuwa shirika/kampuni kinara ya bima ndani na nje ya nchi. Tukishafika namba moja nchini, tunaanza mkakati wa kufungua ofisi nje ya nchi.

Nchi kama Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Rwanda na Kenya ni nchi ambazo tuna mkakati wa kufungua ofisi.

Shirika kwa sasa linaendeshwa kibiashara, mfano, kwa sasa tunaiangalia nchi ya Comoro kwa jicho la uwekezaji mkubwa hapo baadaye.

Tunatambua nia njema ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza uchumi wa nchi na kulinda rasilimali za nchi, hivyo tutahakikisha tunaongeza pato la taifa kutokana na nia hii.

Kutokana na nia hii njema ya serikali, tutakapofikia tunapohitaji kabla ya 2020 tutaweza kuongeza matawi katika nchi jirani, hivyo kutimiza lengo.

Nchi yetu ina jumla ya kampuni 32 za bima, lakini ni kampuni tatu tu ndizo zinamilikiwa na Watanzania. 29 zote ni kampuni za kigeni.

Tanzania imebarikiwa kufanya biashara na nchi zote zilizoizunguka, hivyo ni lazima kujitafakari kibiashara ili kuongeza mapato kama ambavyo nchi hizo zimekuwa zikifanya.

Nchi kuwa na kampuni tatu tu za wazawa si jambo la kusherehekea wala kufurahia, hivyo mkakati wetu ni kurudisha Shirika letu la NIC kuwa namba moja na lenye tija kwa Watanzania,” amesema Kamanga.

Akizungumzia changamoto zinazolikabili shirika hilo, amesema kwamba kuwepo kwa mzunguko mdogo wa fedha ni moja ya changamoto zilizomo katika taasisi.

“Pia watendaji wasio tayari kubadilika na kuendana na kukua kwa sayansi na teknolojia ni moja ya changamoto katika utendaji wa kila siku.

Watumishi wengi wamezoea kufanya kazi kwa mazoea, tunakutana na changamoto kwenye kuwabadilisha ili kuendana na hali halisi ya ukuaji wa biashara na teknolojia.

Kwa mara ya kwanza NIC imeongoza kwenye Maonyesho ya Saba Saba. Tumebadilika na tunaendelea kubadilika taratibu tofauti na hali ilivyokuwa.

Pamoja na changamoto tunazokuwa nazo, tunatumia teknolojia kuboresha shirika na kuwafikia wateja. Tumeweza kuongeza ajira kwa vijana kwa kutumia kaulimbiu ya ‘Changes begin with us’.

Tunazungumza na tunaendelea kuzungumza na vijana kuwapa uwezo na kuelewa kuwa hii taasisi ni yao, hivyo ni jukumu lao kuona inakua.

Ulimwengu wa bima unabadilika, hivyo ni lazima kutumia kizazi cha sasa ndilo jambo tunalofanya. Tumejipanga kubadilika kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Kwa sasa tunaanzisha utaratibu mpya wa kujiunga na bima kwa kutumia simu ya mkononi. Mteja wetu ataweza kukata bima yeye mwenyewe kwa kutumia simu yake ya mkononi bila kufika kwenye ofisi ya bima.

Mpango huu wa kukata bima kwa kutumia simu utaokoa muda mwingi kusafiri umbali mrefu ili kufika ofisi za bima.

Kuanzia mwakani, NIC imejielekeza kutoa elimu kwa Watanzania na kuongeza uelewa wa bima za majengo. Bima hii gharama yake ni ndogo zaidi kuliko ambavyo inadhaniwa na baadhi ya watu.

Ni lazima Watanzania wabadilike na kukata bima kwa ajili ya majengo yao, kila mmoja wetu anao uwezo wa kukata bima hii.

Bima ya jengo ni rahisi na nafuu sana kuliko hata bima ya gari. Tutakata bima kwa Watanzania wengi baada ya kuanza zoezi hili mapema mwakani,” amsema Kamanga.

Shirika la Bima la Taifa lilianzishwa Oktoba 16, 1963 na Serikali ya Tanganyika ikiwa inamiliki asilimia 70 ya hisa zote, na asilimia 30 zilizobaki zikimilikiwa na makampuni binafsi.

Mwaka 1967 baada ya Azimio la Arusha, serikali ilichukua hisa zote chini ya Sheria ya ‘The Insurance (Vesting of Interest and Regulations) Act, 1967.’ Tangu wakati huo hadi sasa shirika linamilikiwa na serikali kwa asilimia 100.

By Jamhuri