Kama tunavyokumbuka Februari 5, 1977, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizinduliwa Zanzibar. Siku hiyo Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere, alitaja kazi mbili za chama hicho.

Mwalimu Nyerere alisema kwamba kazi ya kwanza ya CCM ni kujenga Ujamaa Tanzania. Kazi yake ya pili ni kulinda heshima ya Tanzania. Kadiri siku zinavyokwenda, inaonesha kwamba CCM imeshindwa kufanya kazi zote mbili.

Kwanza, imeshindwa kujenga Ujamaa Tanzania. Kwa vyovyote, bila Azimio la Arusha lililoweka misingi ya Ujamaa, Tanzania hakuna Ujamaa tena.

Kwa upande wa kazi yake ya pili — ya kulinda heshima ya Tanzania — tunaweza kukubaliana pia kwamba CCM imeshindwa pia kufanya kazi hiyo.

CCM ya leo inahubiri siasa zaidi kuliko masuala ya kujenga heshima ya Tanzania. Kinachoonekana ni ukweli kwamba CCM imeiachia Serikali yake ifanye kazi ya kulinda heshima ya Tanzania. Nayo pia imeshindwa kulinda heshima ya Tanzania.

Kwa hiyo, Tanzania ya leo haiheshimiki kama CCM ilivyoheshimika wakati inazaliwa mwaka 1977.

Tuchukue, kwa mfano, majuma machache yaliyopita, Waziri wa Uchukuzi,  Dk. Harrison Mwakyembe, alikuwa mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Lubumbashi ni jina jipya la mji huo ambao wakati wa Wabelgiji uliitwa Elizabethville, yaani “Mji wa Elizabeth.”

Dk. Mwakyembe alikwenda Lubumbashi kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Alipokuwa Lubumbashi, Dk. Mwakyembe alijionea madereva wa Tanzania wanaoendesha magari makubwa ya mizigo wanavyoidhalilisha Tanzania kutokana na kutokuwa watanashati. Ni wachafu kupindukia! Wameshindwa kulinda heshima ya Tanzania.

Dk. Mwakyembe alisema kwamba  madereva wa Tanzania hawawezi kulinganishwa na madereva kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe na Zambia. Wao ni wasafi na wanajipenda. Wanalinda heshima ya nchi zao.

Madereva wa Tanzania ni wachafu kimavazi. Hata pia wengi wao miili yao ni michafu!

Hapa tunalazimika kumpongeza Dk. Mwakyembe. Amekuwa kiongozi wa kwanza Tanzania kuona na kutambua kuwa  madereva wa Tanzania ni wachafu na wanachafua heshima ya Tanzania mbele ya mataifa mengine.

Lakini wakati huo huo, kitendo cha Dk. Mwakyembe kugundua nje ya nchi kwamba  madereva wa Tanzania ni wachafu kinadhihirisha kitu kimoja. Kinadhihirisha jinsi viongozi wa Tanzania wanavyopenda Tanzania iheshimiwe zaidi nje ya nchi kuliko ndani ya nchi.

Viongozi wa Tanzania hawajali hali mbaya ya mambo hapa nchini. Kwa sababu madereva wachafu ambao Dk. Mwakyembe aliwaona Lubumbashi ni sehemu ndogo tu ya madereva  wachafu waliozagaa Tanzania. Cha kushangaza; viongozi wetu hawajaona madereva hawa wachafu wanavyochafua heshima ya Tanzania hapa nchini!

Waangalie madereva na makondakta wa daladala, pia wale wa magari makubwa kote Tanzania. Miili yao ni michafu na mavazi yao ni machafu. Na Serikali haioni hilo. Kwa hiyo, imeshindwa kuwataka au kuwaamuru wamiliki wa daladala na wa magari makubwa kujali usafi wa madereva na makondakta wao.

Ni muhimu Serikali itambue kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kuchafuliwa kwa heshima ya Tanzania kunakoendelea kufanywa na madereva na makondakta wa daladala hapa nchini.

Si Watanzania tu wanaotumia daladala. Hata wageni wanatumia daladala. Hawa wanawaona madereva na makondakta walivyo wachafu. Wanavaa sare chafu na zilizopasuka. Wanavaa sare chafu na zilizochanika. Wanabadilishana sare hizo chafu ndani ya daladala mbele ya abiria. Wanavaa kandambili. Na wengi wao hawachani nywele zao.

Uchafu wa miili yao na mavazi yao haukuishia hapo. Pia ni wakorofi na wazoefu wa lugha chafu. Kwa kweli wameshindwa kulinda heshima ya Tanzania.

Sasa waangalie wale wanaoendesha bodaboda. Nao pia ni wachafu. Unaweza kumaliza siku bila kumuona mwendesha bodaboda aliyevaa vizuri. CCM haioni hilo. Nayo Serikali ya CCM haioni hilo. Tumeshindwa kulinda heshima ya Tanzania.

Vijana wa Tanzania nao pia ni wachafu sana ukiwaweka kando wale wanaofanya kazi ofisini na wanafunzi wa shule. Kwa kweli wanatia aibu mitaani. Ni wachafu si kwa sababu ni maskini sana, bali ni wachafu kwa sababu CCM na Serikali yake  imeshindwa kuwaelekeza na kuwaongoza vijana wa Tanzania. Imeshindwa kulinda heshima ya Tanzania.

Kwa upande wa Dar es Salaam,  manispaa zote zimefanikiwa kuondoa biashara zilizokuwa zikitandikwa chini. Lakini manispaa hizo hazichukui hatua ya kuondoa uchafu mitaani.

Nenda Kariakoo na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam. Utakuta malundo makubwa ya takataka yanayoachwa bila kuzolewa. Uchafu wa Dar es Salaam unatia aibu. Manispaa zimeshindwa kulinda heshima ya Tanzania.

Sasa angalia ombaomba mitaani. Tulilinda heshima ya Tanzania kwa kuwaondoa  ombaomba hawa mitaani  wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama. Kwa kuwa Rais Obama amekwenda zake basi ruska kuvunja heshima ya Tanzania!

Tumeidhalilisha sana Tanzania! Tanzania ni miongoni mwa vituo vya dawa za kulevya barani Afrika! Tanzania inaongoza barani Afrika kwa kuandikisha watoto  wanaoanza shule, lakini wanamaliza shule wakiwa hawajui kusoma na kuandika vizuri.

Tanzania ni ya tatu barani Afrika kwa unywaji wa pombe za mataputapu baada ya Niger na Uganda! Tanzania ni ya tisa barani Afrika kwa uwezo mdogo wa watu wake katika kufikiri!

Tazama! Leo Dar es Salaam umekuwa mji wa starehe ambao wakati wote unakuta baadhi ya watu wamekaa makundi makundi mitaani wakiongea. CCM na Serikali yake imeshindwa kuhimiza watu kufanya kazi.

Nimewaona Wachina wakishangaa  kuona kuwa Tanzania ni nchi ambayo  watu wake hawataki kufanya kazi. Hakika tumeshindwa kulinda heshima ya Tanzania. Tumeidhalilisha Tanzania kiasi cha kutosha.

 

926 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!