DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Dunia imekumbwa na janga la ugonjwa wa corona (Uviko -19).Ugonjwa huu wa homa kali ya mapafu uligundulika kwa mara ya kwanza Desemba 2019 katika Jiji la Wuhan, China.

Ukaanza kusambaa kwa kasi katika mataifa ya Marekani, Uingereza, Ufaransa na barani Afrika. Kusambaa haraka kwa ugonjwa husababishwa na mwingiliano wa watu duniani.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna taifa linaloweza kujiendesha bila kutegemea taifa jingine.

Kadiri siku zilivyosonga mbele ugonjwa ulizidi kusambaa na kuwa tishio la dunia. Afrika haikubaki nyuma katika mapambano dhidi ya corona.

Pamoja na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya na wanasayansi, kuna nchi zilijikita katika tiba za asili, maombi na baadhi kujifungia ndani kwa siku kadhaa na kufunga mipaka.

Katika hatua nyingine ya mapambano dhidi ya uviko -19 wanasayansi katika mataifa mbalimbali walifanya tafiti mbalimbali na baadhi wakafanikiwa kupata chanjo na kuisambaza dunia nzima.

Yapo mataifa ya Afrika yaliyotilia shaka chanjo hizo na kutaka kufanyika kwa utafiti na uchunguzi wa kina kwa kutumia wataalamu wa ndani kabla ya kuanza kutumia.

Januari 27, mwaka huu, aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, aliwataka Watanzania kuwa makini wanapoamua kufuata chanjo ya corona nje ya nchi, akiwasihi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kumwomba Mungu.

Katika kujiridhisha na aina ya chanjo zinazoingizwa nchini kwa ajili ya corona, Aprili 6, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda kamati maalumu ya kufanya tathmini ya hali ya ugonjwa nchini na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kukabiliana nao.

Mei 17, mwaka huu kamati, chini ya uenyekiti wa Profesa Said Abood, ilikabidhi ripoti ikipendekeza njia ya kupata unafuu kama serikali itajiunga na mpango wa kupata chanjo unaofahamika kama Covax Facility kwa kuwasilisha andiko.

Juni mwaka huu, Rais Samia alisema Tanzania imeandaa andiko kwa ajili ya kuomba chanjo ya Uviko-19 kupitia mpango wa Covax Facility.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na corona nchini, hatimaye Tanzania ilipokea awamu ya kwanza ya msaada wa dozi 1,058,400 za chanjo huku Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, akiwahakikishia Watanzania usalama wake.

Akipokea msaada huo, Julai 24, mwaka huu kutoka Ubalozi wa Marekani, Dk. Gwajima alifafanua makundi yanayopewa kipaumbele kuwa ni watu wenye umri kuanzia miaka 50, wenye magonjwa sugu na watumishi wa afya.

Tanzania pia imepokea chanjo kutoka China na sasa chanjo ya corona hutolewa katika vituo mbalimbali kwa watu wote.

Hamasa ya kuchanja iliongezeka baada ya Rais Samia na viongozi wa kitaifa kujitokeza na kuchanja hadharani na kuwatoa hofu wananchi juu ya usalama wa chanjo hiyo na kwa kusema chanjo hiyo ni salama, imethibitishwa na wataalamu wetu na hutolewa bure.

Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupata chanjo. Viongozi wa ngazi mbalimbali wamekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, taasisi za dini na viongozi wastaafu wa kimataifa wanaunga mkono juhudi za mapambano hayo.

Novemba 29, mwaka huu, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete aliwataka wahitimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa (Iringa) kuwa mabalozi wazuri katika vita ya kupambana na corona.

“Tunategemea muwe mabalozi wazuri wa kwenda kuwahimiza wananchi kupata chanjo ya Uviko–19 kila mtu akichanja dunia yote itakuwa salama, tumuunge mkono Rais Samia katika mapambano haya,” amesema Kikwete.

Wakati dunia ikiendelea na mapambano dhidi ya corona, kuna taarifa za kuhuzunisha za kutokea kwa wimbi la nne la ugonjwa huo ambalo limeelezwa kuwa ni hatari zaidi. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya na kueleza kuwa aina mpya ya kirusi cha corona, Omicron, ni hatari na kinaweza kusababisha maambukizi kuongezeka kote ulimwenguni.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, alitoa wito kushinikiza jumuiya ya kimataifa kutoa chanjo kwa mataifa maskini kuwanusuru watu katika mataifa hayo.

Kirusi cha Omicron kiligunduliwa Afrika Kusini mwezi uliopita, ushahidi wa awali ukionyesha kuwa kirusi hicho kina hatari kubwa ya maambukizo. Afrika Kusini imesifiwa kwa kuripoti haraka taarifa hizo.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetangaza kuibuka kwa wimbi la nne la maambukizo ya Uviko–19. Taarifa ya wizara iliyotolewa Novemba 27 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe, imeeleza kuwa tishio la kuwapo kwa wimbi la nne la corona nchini linalotokana na viashiria mbalimbali na kwamba wizara ipo makini kudhibiti hali hiyo.

Hivi sasa jitihada kubwa zinaendelea za kupambana na corona huku ugonjwa wa ukimwi ukionekana kusahaulika kidogo, tofauti na miaka ya nyuma.

Desemba 1 ya kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani ambayo inaadhimishwa kama siku maalumu ya kukuza ufahamu kuhusu athari zinazotokana na ugonjwa huo. 

Tofauti na huko nyuma, kwa sasa ukimwi hauzungumziwi sana pamoja na ukweli kwamba maambukizi bado yako juu. Serikali na Wizara ya Afya zimefanya jitihada mbalimbali kuhusu ukimwi lakini katika ngazi za chini na mtu mmoja mmoja katika baadhi ya maeneo elimu hiyo bado haijafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Akimwakilisha Rais Samia katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa wanaobainika kuwanyanyapaa na kuwatenga watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

“Kumekuwa na madai kuwa watumishi wa afya wana tabia za unyanyapaa na kuvujisha siri za wagonjwa wanapotoa huduma katika vituo vyetu vya tiba na matunzo kwa wagonjwa hao. Vitendo na tabia hizi viripotiwe mara moja pindi vitakapotokea,” ameonya Majaliwa.

Kwa upande wake, Dk. Hassan Sembogo wa Morogoro, amesema pamoja na maambukizo kitaifa kuonekana katika kiwango cha chini lakini kuna baadhi ya mikoa kama Njombe na Iringa maambukizo ni zaidi ya asilimia 10.

“Baadhi ya maeneo hapa nchini watu wengi wanaogopa kupima afya zao kwa kuhofia unyanyapaa endapo watagundulika wameathirika. Hii ni kutokana na manyanyaso wanayopata wale wanaobainika kuathirika katika jamii. Elimu zaidi ya afya inahitajika ili kukabiliana na janga hilo hasa vijijini,” anasema Dk. Sembogo.

0755 985 966

By Jamhuri