Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa Tanzania na Watanzania si maskini.

Na kwa sababu hiyo anawataka wananchi wasijione kuwa ni maskini, badala yake wajione kuwa ni matajiri kwa sababu wamejaliwa rasilimali zote.

Tunaungana na Rais Magufuli tukiamini kuwa umaskini mkubwa wa Watanzania umo kwenye fikra, na kamwe si kwa rasilimali.

Kwa muda mrefu nchi yetu imeibiwa rasilimali nyingi. Tangu zama za utumwa, ukoloni na hata baada ya uhuru, Tanzania na Afrika kwa jumla tumeendelea kuibiwa mali zetu.

Kuna sababu nyingi zilizosababisha hali hii. Miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa elimu na ujuzi wa kujikwamua kwenye lindi la umaskini, uonevu wa mataifa makubwa kwenye ulali wa kibiashara, ukosefu wa teknolojia na mitaji, siasa na uongozi mbovu wa baadhi ya watawala; na uwepo wa vibaraka wa ndani ya nchi wanaoshirikiana na wenzao wa kigeni katika kuhujumu rasilimali za Afrika.

Miaka takriban 60 baada ya kupata Uhuru hatuna sababu ya kuendelea kulalamika. Hatuwezi kuwa nchi ya watu wanaolalamikia wakoloni au mabereru. Tuna wazee na vijana walioelimika katika nyanja zote za kiuchumi.

Kinachotakiwa sasa ni kila mmoja wetu kuamka na kutumia vipawa alivyojaliwa katika kuongoza mapambano ya kujikomboa. Vita hii inakuwa nyepesi kama tunakuwa na viongozi kuanzia ngazi ya chini hadi taifa wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.

Mataifa yaliyoendelea hayakufika hapo kwa hisia, bali ni kwa kubuni na kuchapa kazi kadiri ilivyowezekana.

Kijiografia Tanzania ipo mahali pazuri mno. Hata hivyo, jiografia pekee si kigezo cha kuwa imara kiuchumi. Tunapaswa kutumia fursa hii kuzalisha na kuuza zaidi kwa mataifa yanayotuzunguka. Wananchi wahamasishwe ili washiriki uzalishaji mali na watafute masoko nje ya nchi.

Viongozi wetu waendelee kulinda rasilimali za nchi ili zisiendelee kuibwa au kutoroshwa kwa manufaa ya wachache. Tuhakikishe kabla ya kuomba tunatumia rasilimali zetu kwa kadiri inavyowezekana.

Mapambano haya yatakuwa rahisi endapo wananchi tutaunga mkono juhudi za serikali katika ujenzi wa uchumi wa kisasa ili hatimaye tuutokomeze umaskini nchini mwetu.

By Jamhuri