Desemba 6, mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitangaza uamuzi wa Serikali wa kuundwa chombo maalumu ili kusimamia eneo la kilometa za mraba 1,500 katika Pori Tengefu la Loliondo.

Akasema: “Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum, kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo.”

Akaiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae muswada ili itungwe sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalumu au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia na kulinda mazingira na eneo hilo kwa jumla.

Ukiacha ushoroba na mazalia ya wanyamapori, eneo hilo ndilo chanzo cha asilimia 50 ya maji yote yanayoingia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti hii ina maana kufa kwa Loliondo ni kutoweka kwa Serengeti.

Akaitaka Wizara hiyo iandae waraka maalumu utakaowasilishwa serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Baada ya tamko hilo, mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari vikaandika “Waziri Mkuu amaliza mgogoro Loliondo”. Siku iliyofuata magazeti nayo yakaibuka na vichwa vya habari vyenye mwelekeo huo.

Nilikuwa miongoni mwa tuliotofautiana na aina hiyo ya vichwa vya habari. Nakumbuka niliandika makala ndefu nikionya kuwa mgogoro wa Loliondo upo na nikasema hauwezi kumalizwa kwa matamko, isipokuwa kwa hatua madhubuti. Wanaoifahamu vema Loliondo wanajua nisemacho.

Uamuzi wa Waziri Mkuu ulikuwa ni sehemu ya mlolongo wa tume zaidi ya saba zilizoundwa na kutoa na majibu yanayofanana. Hitimisho muhimu kwenye kamati zote hizo ni kutengwa kwa eneo la uhifadhi la Loliondo ili kulinda ikolojia ya Serengeti.

Nilisema kutulia kwa Loliondo maana ni kuyafanya mashirika yasiyo ya Serikali (NGOs) zaidi ya 30 yaliyoko katika eneo hilo, yafe. Kuna mama mmoja anasomesha watoto wake Arusha mjini ambako ada kwa mtoto mmoja kwa mwaka ni Sh milioni 52! Bila vurugu za Loliondo huyu atahimili ada hiyo kwa watoto watatu anaosomesha?

Nikasema wakati Waziri Mkuu akijiandaa kutoa tamko, tayari kuliwapo vikao mjini Arusha vyenye lengo la kupinga mpango huo.

Vinara wa mpango huo wapo ndani na nje ya nchi. Wanajulikana. Wengine wako ndani ya Baraza la Mawaziri. Wanajulikana, hata Waziri Mkuu anawajua. Upande mmoja wanaonekana ni watumishi wa Serikali, lakini upande wa pili ni mawakala wa NGOs na mabeberu. Mchana wanaonekana wako serikalini, usiku wako kwenye NGOs.

Wanaopinga mpango huu wengine ni wakuu wa mikoa. Wapo, na wanajulikana. Hawapingi mpango huu kwa sababu nyingine, isipokuwa kwa maslahi binafsi. Haiwezekani mambo haya yakawa yanajulikana kwa watu wa kawaida, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vikawa havijui. Huu ni woga au ni uzembe?

Mtu unaweza kujiuliza, kwanini kila mara wanaotangaza kunyang’anywa ardhi ni wananchi wa Loliondo pekee? Kwani nchi hii haina wafugaji katika maeneo mengine?

Miezi kadhaa iliyopita tulichapisha taarifa ndefu ya mamluki walioletwa nchini wakijifanya watalii, lakini wakiwa wamekuja kukusanya taarifa za uongo za kuichafua nchi. Tukawataja kwa majina, kazi zao na wanakotoka. Tukaandika hadi nyumba walizolala na watu walioshirikiana nao. Serikali, kama ilivyotarajiwa ikakaa kimya. Matokeo yake ni haya mashambulizi ya uongo yaliyochapishwa kwenye vyombo vya habari duniani kote kwamba Tanzania inawafukuza Wamasai kwenye ardhi yao.

Tumeshachapisha taarifa zote za siri kuhusu NGOs na wafadhili wao. Tumechapisha mtandao wao wote, lakini Serikali iko kimya kabisa. Kuna nini?

Wiki nne hivi zilizopita tulichapisha taarifa ya mpango mahsusi wa NGOs uliolenga kukwamisha agizo la Serikali la kugawa eneo la Pori Tengefu la Loliondo.

Hapa ikumbukwe kuwa Waziri Mkuu aliahidi kabla ya Machi mwaka huu chombo maalumu kingekuwa kimeshatangazwa ili kusimamia eneo hilo.

Wakati NGOs hizo zikijipanga, tukasema kumeibuka mvutano serikalini juu ya uanzishwaji wa chombo hicho, kiasi cha baadhi ya watendaji kunukuliwa wakisema hakitaundwa hadi Serikali ya Awamu ya Tano itakapokuwa imeondoka madarakani.

Tukasema mikakati hiyo inapata ufadhili wa baadhi ya mashirika ya kimataifa na NGOs, na kwamba wakati Serikali ikijiandaa kutangaza jina na aina ya chombo kitakachoundwa, wao wamekutana Arusha na kupendekeza chombo chao kiitwe Loliondo Area Management Authority (LAMA).

Kikao hicho kiliitishwa kwa ushirika wa asasi tatu za Pastoral Women’s Council (PWC), Ujamaa Community Resource Trust (U-CRT) na PINGO’S Forum. Kilifanyika katika hoteli ya Golden Rose jijini Arusha. Waziri Mkuu na Waziri wa Maliasili na Utalii tuliwahadharisha juu ya NGOs hizi na nyingine nyingi, sasa tunaona kazi zake! Nchi inachafuliwa. Waziri Mkuu alishaagiza zichunguzwe, lakini hatuoni kitu na kwa maana hiyo hazina kosa!

Wakati NGOs zikiunda LAMA, taarifa zinasema Serikali inakusudia kuunda chombo kitakachoitwa Loliondo Special Conservation Area (LSCA) na inapendekezwa kiwe chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA). Sasa nani mwenye mamlaka katika nchi hii ya kuamua na kutekeleza jambo? Iweje Serikali ikubali kichezewa namna hii?

Naomba viongozi watambue kuwa kinachoendelea Loliondo ni vita ya kiuchumi. Vita hii ni kubwa. Wasidhani ni ya ndani tu, bali ina nguvu kutoka hadi kwa majirani zetu. Bahati mbaya nchini mwetu intelejensia yetu imejiegemeza kwenye maandamano yasiyo na athari zozote, lakini hatuendi mbele kufanya intelejensia ya kiuchumi.

Tanzania inakua kiuchumi. Hilo majirani zetu wanalijua. Wanatambua kuwa hawana vivutio vya utalii kutuzidi. Ukitazama uongo uliochapishwa wiki iliyopita utaona unalenga kuua utalii wa Tanzania. Kama maelezo ni ya Loliondo, kwanini picha zinazopamba habari hiyo ziwe za Ngorongoro? Je, si kweli kuwa kwa kufanya hivyo wanalenga kuua utalii katika Serengeti na baadaye Ngorongoro?

Taarifa hiyo inayodaiwa kuwa ni ya uchunguzi imeandaliwa na taasisi za Marekani na Uingereza ambazo madalali wake hapa nchini ni kina PWC ambao licha ya matendo yao, wameendelea kukusanhya fedha kwa mgongo huu.

Hadi wiki iliyopita kulikuwa na maelfu kwa maelfu ya mifugo kutoka Kenya. Waziri Mkuu aliagiza ng’ombe wawekwe alama. Watanzania wamekubali. Wameweka. Loliondo kumejaa ng’ombe wasio na alama. Hawa wanatoka Kenya. Wanalisha Tanzania ili majani yaliyo upande wao yawafae wakati wa kiangazi. Amri za machifu wa Kenya zinafanya kazi ndani ya maeneo yao na kuvuka hadi Tanzania na ndio maana kuna kitu wanakiita ‘Maasai Land’. Mbona migogoro hii haiikubuki Monduli au Longido, au Maswa, au Tarime? Kwanini Loliondo tu? Ngorongoro ikitulia hawatakuwa na sehemu ya malisho.

Nionavyo mimi ni kuwa mgogoro wa Loliondo umedumu kwa sababu ya udhaifu wa baadhi ya watu wenye mamlaka ya kuumaliza. Tumekuwa na bahati mbaya, kama nchi, ya kusingiziwa maneno nasi tukakaa kimya.

Wenzetu wako makini. Wanatambua wakishaichafua Serikali ya Tanzania idadi ya watalii Serengeti na Ngorongoro itapungua maana hakuna mzungu angependa kwenda kustarehe eneo ambalo wananchi ‘wanateswa’. Bahati mbaya hata majibu ya Serikali yanayotolewa ni mepesi mno kana kwamba uongo na uzushi unaofanywa na wabaya wa nchi hii hauna athari kiuchumi.

Wakati umefika wa kuwa na intelejensia ya kiuchumi ili jambo lolote kabla ya kutokea na hata likishatokea, tujue namna ya kulikabili.

Muhimu ni kwa Serikali kufanyia kazi mambo tunayoyaweka kwenye vyombo vya habari. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kuzomoka kuandika kitu kisichokuwapo. Mambo yanayoandikwa na watu wengi kuhusu Lolindo yapo, na kwa maana hiyo ni wajibu wa vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana na watu hao ili kupata taarifa na kuchukua hatua. Muda ni huu.

Napenda kureja kama nilivyowahi kusema mara kwa mara huko nyuma kwamba haya tunayafanya ili kutimiza wajibu wetu Kikatiba.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatutaka tulinde mali ya umma. Ibara ya 27.-(1) inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao.”

Ndivyo Katiba ya nchi yetu inavyotutaka.

Wanyamapori na misitu ya Ngorongoro na Serengeti ni mali ya Watanzania wote wa leo na wajao. Hatuwezi kukaa kimya tukishuhudia urithi huu ukitoweka.

Haya tunayasema mapema ili wenye kusikia, na wasikie; wenye mamlaka ya kuchukua hatua na wafanye hivyo. Sitakuwa sehemu ya lawama kwa vifo vya Serengeti na Ngorongoro kwa kuambiwa sikusema nilipotakiwa kusema, kuonya nilipostahili kuonya, kushauri nilipoona nina wajibu wa kushauri na kulinda rasilimali za nchi pale nilipojua huo ni wajibu wangu Kikatiba. Vita ya kiuchumi yatupasa sote tuishiriki kwa moyo wa uzalendo.

1457 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!