Kwa muda sasa Watanzania wameshuhudia wimbi kubwa la madiwani na wabunge wanaovihama vyama vyao. Walianza madiwani watano wa Arumeru Mashariki, wakafuata wenzao mkoani Kilimanjaro, kisha ikawa zamu ya wengine watatu wa Manispaa ya Iringa. Hawa wote walikuwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Baada ya hapo wimbi la madiwani kuvihama vyama vyao limeendelea, na kabla halijatulia, ikawa zamu ya wabunge. Lazaro Nyalandu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), akavijua uanachama na kupokewa Chadema.

Mbunge wa Kinondoni, Maulidi Mtulia (CUF) na Dk. Godwin Mollel (Chadema) nao wakavikimbia vyama vyao na kujiunga CCM. Si hivyo tu, bali wanachama kadhaa mashuhuri wa vyama vya Chadema na ATC-Wazalendo, nao wakaviacha vyama vyao na kurejea CCM. Wote hao, sababu wanazotoa kama chanzo cha wao kurejea CCM karibu zinafanana. Wanasema wanaridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli, hasa katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Tunatambua na kuheshimu uhuru wa mtu kuhama chama kimoja na kujiunga katika chama kingine. Ni haki ya kila mtu kikatiba. Lakini shaka yetu inakolezwa na madai ya kwamba haya yanayoendelea yanatokana na ushawishi wa kifedha. Pande zote zinatuhumiana, lakini upande mmoja umeenda mbali zaidi kwa kutoa ‘ushahidi’ wa rushwa inayodaiwa kutolewa na upande mwingine. Takukuru bado hawajajitokeza kueleza ukweli, au uongo wa madai hayo.

Pamoja na ukweli kuwa ni haki ya mtu kujiunga katika chama anachopenda, bado tunashawishika kuamini kuwa mpango wowote – uwe wa hiari au wa makusudi – wa kuthubutu kudumaza au kuua Upinzani katika Taifa letu, hauna budi kulaaniwa kwa nguvu zote. Upinzani si uadui. Mfano mzuri ni upinzani wa timu za Simba na Yanga. Upinzani wa timu hizo umesaidia kuleta hamasa ya ushindani ingawa nje ya mipaka tumekuwa wasindikizaji.

Upinzani umeisaidia sana nchi hii tangu Katiba ilipoutambua mwaka 1992. Upinzani umeibua mambo makubwa na mazito ndani na nje ya Bunge. Kashfa nyingi zilizotikisa nchi hii zimejulikana kwa msaada mkubwa wa Upinzani.

Upinzani unasaidia kukiamsha chama tawala. Wapinzani wanakuwa huru kuikosoa Serikali, tofauti kabisa na wanachama wa chama tawala peke yao. Tunapaswa kuwa na upinzani ulio imara ambao kazi yake, ukiacha ile dhamira ya kushika dola, ni kuionesha Serikali iliyo madarakani wapi inapopaswa kuparekebisha.

Kuna fununu kuwa wabunge wengine wako njiani kuvihama vyama vyao na kujiunga CCM. Tunaomba watambue kuwa licha ya kudumaza maendeleo, wanasababisha gharama kubwa kwa uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi zao. Tunatambua kazi kubwa na njema zinazofanywa na Rais Magufuli. Tunaamini kuwa zipo njia mbadala za kumuunga mkono badala ya hii ya kuvihama vyama.

By Jamhuri