Familia ya Mohamed Msabaha (95) ya jijini Dar es Salaam inadai `kutapeliwa’ nyumba ya mzazi wao huyo kwa madai kuwa mnunuzi alimlaghai, hivyo wameiomba Serikali iwasaidie kuirejesha.

Nyumba hiyo inadaiwa kununuliwa na mtu anayetajwa majina ya Hussein Mkufya, kwa makubaliano na Msabaha ambaye kwa sasa anaishi wilayani Korogwe mkoa wa Tanga.

Msemaji wa familia hiyo, Hadija Msabaha (58) ameiambia JAMHURI kuwa baba yao mzazi, Msabaha alijenga nyumba hiyo iliyopo Kinondoni Shamba, yenye namba KIN/KNS/312 ilijengwa miaka mingi iliyopita,  lakini ikauzwa kupitia mbinu zinazoaminika kuwa na ulaghai.

Amesema, familia ya Msabaha ilipata taarifa ya mauzo ya nyumba hiyo mwaka jana, lakini hakuna mkataba wa mauzo ama ushiriki wa wanafamilia wakiwamo wanawake na watoto wa Msabaha.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha taarifa, mnunuzi huyo aliinunua nyumba hiyo kwa Shilingi milioni 30.

Hadija alikuwa kati ya watoto watatu wa Mzee Msabaha wakiwamo Fatuma (50) na Ramadhan (52) waliozungumza na JAMHURI wakisema mnunuzi huyo anaijua familia yao, hivyo isingewezekana kuinunua nyumba hiyo kwa nia njema pasipo kuwahusisha.

Watoto hao wanasema walitoa taarifa ya uuzaji nyumba hiyo kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kinondoni Shamba, Timbuka Chau.

JAMHURI ilipowasiliana na Mkufya kuhusu madai hayo amesema, ‘‘suala hilo siwezi kulizungumzia kwani lina shughulikiwa na vyombo vya sheria.’’

Akaongeza, ‘‘hao waliokuja kulalamika kwenye vyombo vya habari wajue hawawezi kupata haki kwa kukimbilia huko na kwa sababu hiyo nitawashtaki.’’

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kinondoni Shamba, Chau ameliambia JAMHURI kuwa familia hiyo iliwasilisha malalamiko ya kuuzwa nyumba yao katika mazingira yasiyofahamika.

Amesema malalamiko hayo yana mashiko kwa vile, hata ofisi yake haikushirikishwa kwa kupewa taarifa ama kushuhudia utiaji saini mkataba wa mauzo ya nyumba hiyo.

‘‘Sisi wa Serikali ya Mtaa hatukushirikishwa wala hatuelewi uhalali wa mkataba wa kuuziana nyumba hiyo,’’ amesema.

Hadija amesema hawaelewi utaratibu uliotumika kununua nyumba hiyo wakati familia wakiwemo wake wawili wa mzee huyo, Zaina Rashid na Amina Ally hawana taarifa.

Amesema badala yake, familia hiyo ilishtushwa na tangazo kuwa nyumba hiyo imenunuliwa na Mkufya.

“Tunachoelewa, mzee wetu katapeliwa nyumba kwa ujanja kwani hata hiyo fedha anazodai kulipwa (Shilingi milioni 30) hatuamini kama kweli,” amesema Hadija.

“Sisi kama watoto ambao tulikuwa tunaishi katika hii nyumba ya baba yetu mzazi tumemwomba Mkufya anayedai kuwa ameuziwa, aeleze ukweli ili ikibidi tumrudishie hela yake kama ana vilelezo, lakini amekataa,” ameongeza.

Mtoto mwingine, Fatuma Msabaha amesema kutokana na mauziano hayo kutiliwa shaka, ununuzi wa nyumba hiyo unapaswa kutangazwa kuwa batili.

 “Hatuwezi kudhulumiwa haki na kunyanyaswa namna hii kwenye nyumba ya baba yetu,”amesema.

Francis Massawe (29) ambaye ni mpangaji wa nyumba hiyo tangu Agosti mwaka huu, amethibitisha kupewa taarifa na mnunuzi huyo akitakiwa kuondoka.

Mpangaji mwingine, Jasmini Sadiki (28) amesema alianza kuishi katika nyumba hiyo mwaka 2009 akiwa na shangazi yake, hadi alipoolewa na kijana mmoja katika nyumba hiyo hiyo.

“Tulipangishwa katika nyumba hii na mzee Msabaha hadi mwaka 2015 tulipoitwa nyumbani kwa mjumbe wa mtaa kuchukua barua zilizotupa maelekezo wapangaji wote kuwa tutalipa kodi kwa Mkufya, mmiliki wa nyumba hiyo,” amesema.

Mpangaji mwingine, Frida Joseph (39) amesema taarifa ya nyumba hiyo kuanza kumilikiwa na Mkufya walijulishwa kwa mdomo.

Amesema Mkufya ameshawatangazia azma yake ya kuibomoa nyumba hiyo na kwamba wantakiwa kuhama ifikapo mwishoni mwa mwezi huu (Desemba).

Please follow and like us:
Pin Share