Nyerere: Huwezi Kuwadanganya Wote

“Unaweza kuwadanganya watu wote kwa muda fulani na baadhi ya watu wakati wote, ila hauwezi kuwadanganya watu wote kwa wakati wote.”

Haya ni maneno yaliyojaa hekima yaliyotolewa na Baba wa Taifa na Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alifariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza. Dunia haiwezi kumsahau kwa kusimamia haki, amani na kupambana na unyonyaji katika nchi zinazoendelea.

Mandela na Elimu

“Elimu ni silaha yenye nguvu yenye uwezo wa kuibadilisha dunia.”

Nukuu hii ni miongoni mwa maneno yaliyotolewa na Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini kuchaguliwa kidemokrasia, Nelson Rolihlahla Mandela. Alikuwa kiongozi wa chama cha siasa cha ANC na mpambanaji dhidi ubaguzi wa rangi uliokuwa umekithiri nchini humo. Alizaliwa Julai 18, 1918 na alifariki dunia Desemba 5, 2013.

John F. Kennedy na Ushindi

“Ushindi una baba wengi ila kushindwa ni yatima.”

Nukuu hiyo ni ya John Fitzgeraild Kennedy, Rais wa 35 wa Marekani aliyefahamika zaidi kwa kifupi cha majina yake JFK na wengine walimuita Jack. Alizaliwa Mei 29, 1917 na kuwa Rais wa taifa hilo kuanzia Januari 20, 1961 hadi alipouawa kwa kupigwa risasi Novemba 22, 1963.

Martin Luther: ukimya wa marafiki

 “Ukimya wa marafiki zetu unaumiza kuliko kelele za madui zetu.”

Haya ni maneno ya Martin Luther King Jr mmisionari wa Marekani aliyepigania haki za binadamu. (Januari 15, 1929 – Aprili 4, 1968).

Alipozaliwa aliitwa Michael Luther King, Jr baadaye alibadili jina na kuitwa Martin.