Nichukue fursa hii kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa Ruge Mutahaba, pamoja na Watanzania wote walionufaishwa na kipawa cha mzalendo huyu.

Umati wa watu waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kumlilia Ruge unadhihirisha wazi aina au muundo wa kibinadamu wa Ruge. Kama asingekuwa mtu mwema, kwa hakika asingeliliwa kwa namna tuliyoiona.

Tunaweza kusema mambo mengi, lakini lililo muhimu kutoka kwa Ruge ni namna binadamu tunavyopaswa kuishi na wanadamu wenzetu. Ruge hakuwa malaika, lakini wingi wa waliomlilia unathibitisha pasi na shaka kwamba alikuwa mtu wa watu.

Kuna maneno ya ‘kimombo’ mimi hupenda kuyatumia mara kwa mara. Living for Others is the Rule of Nature. Ruge aliishi kwa ajili ya wengine. Alitumia kipawa chake kuwasaidia wenye mahitaji. Ametekeleza wajibu wake. Ameimaliza safari ya duniani, lakini nyayo za kazi zake zitaendelea kudumu.

Jambo jingine kubwa lililotokea wiki iliyopita ni la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uamuzi wake umepokewa kwa mitazamo tofauti. Wapo waliofurahi, lakini wapo pia walioumizwa kwa uamuzi wake huo. Sisi ni nani hata tumhukumu? Ametekeleza lile aliloona lina manufaa kwake binafsi, na bila shaka kwa taifa lake.

Pamoja na furaha waliyonayo Wana CCM ya kumpokea Komredi Lowassa, bado tunapaswa kuwa na hadhari yenye kutuongoza katika kuhakikisha kuwa vyama vya upinzani havitoweki nchini mwetu.

Natoa hadhari hii kwa sababu kuna kila dalili zinazoonyesha wazi kuwa lipo kundi jingine kubwa la watu wazito walio katika vyama vya upinzani kuhamia CCM. Naomba nieleweke vizuri hapa. Haki ya kujiunga au kuhama chama ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa.

Pamoja na ukweli huo, tusichukulie kwa namna yoyote ile ya kudhoofu kwa vyama vya upinzani kama ni dalili njema kwa ustawi wa demokrasia nchini mwetu. Mara zote nimeviona vyama vya upinzani kama kioo kwa serikali iliyo madarakani. Wengi wetu tunatambua na kuheshimu kazi kubwa ya kutukuka iliyofanywa na baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani katika taifa letu. Tunatambua kashfa kubwa zilizoibuliwa na vyama vya upinzani na hatimaye kulitikisa taifa letu.

Tunatambua ukosoaji mkubwa uliofanywa kwa miaka mingi na vyama hivi na hata kuisaidia serikali kufumbua macho na masikio. Juzi tu, tumeona kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na mbunge wa upinzani kwenye suala la kikokotoo.

Mambo mazito ya aina hii ni mara chache kuibuliwa na watu walio katika chama kimoja, japo huko nyuma yapo matukio kadhaa yaliyoibuliwa na wabunge wa CCM. Lakini kwa sababu ya ile desturi ya uwajibikaji wa pamoja, imekuwa vigumu kuwapata wanachama wenye vifua imara vyenye kuwawezesha kuibua ‘madudu’ ndani ya serikali inayotokana na chama chao.

Kuna ushahidi usiotiliwa shaka, kuna mengi yaliyoibuliwa na wapinzani yalitoka CCM, yakasogezwa kwa wafuasi wa upinzani na huko yakapata mwanya wa kusemwa hadharani. Kwa maneno mengine upinzani umekuwa ni kama spika inayotumika kusambaza muziki!

Neno au jina ‘upinzani’ linaweza kuwa na ukakasi, na huenda ikatupasa huko tuendako tupate neno zuri zaidi. Tukipata neno mbadala huenda hata msigano ndani ya vyama vya siasa tukauona ni jambo lenye kuleta manufaa kwa vyama vyenyewe na hata kwa nchi.

Vyama vya siasa imara, vyenye viongozi wenye weledi na wanaokosoa kwa staha, ni chachu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. Tutafanya makosa makubwa kuamini kuwa chama kilicho madarakani kinaweza kuwa chama imara au bora bila kuwa na upinzani, ama wa kutoka nje, au wa ndani.

Tuwapongeze wanaotumia haki zao za kuvihama vyama vya siasa, lakini wakati huo huo tuweke hadhari kuhakikisha kuwa vyama hivyo havigeuki na kuwa kama ‘viumbe walio hatarini kutoweka’.

Wazee wetu waliobariki uwepo wa mfumo wa siasa wa vyama vingi hawakufanya hivyo kwa bahati mbaya. Walifanya kwa kuamini kuwa wakati ulikuwa sahihi, pia walitambua umuhimu wa kuwa na whistleblowers katika suala zima la ujenzi wa taifa letu.

Tunapojiandaa kuona mtikisiko mwingine mkubwa wa vigogo kuvihama vyama vyao na kurejea CCM, tusipuuze wala kufuta ukweli kwamba uwepo wa vyama vya upinzani imara, vinavyowajibika kistaarabu ni suala zuri sana kwa ustawi wa taifa letu. Yeyote anayeitakia mema Tanzania hatafurahia kifo cha upinzani – iwe ndani ya chama tawala chenyewe au kwa vyama vingine. Tusifanye kosa hilo. Kuua upinzani ni kuvunja kioo kinachokisaidia chama tawala kujitazama na kujitakasa.

603 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!