Tutetea urithi wa lugha zetu

Miezi kadhaa iliyopita nilimsikia jirani yangu Mkurya akitoa somo la nyota kwa wageni Wafaransa. Alitaja tafsiri, kwa Kikurya, ya nyota, mwezi, jua, na hata ya sayari Zuhura.

Lugha mama yangu ni Kiswahili, siyo Kizanaki, kwa hiyo hufurahia sana kusikia Mtanzania, tena kijana, akiwa na uwezo mzuri wa kuzungumza lugha yake asilia. Iilikuwa kielelezo cha uwepo wa urithi mkubwa wa tamaduni zetu.

Lakini nilitoka kufurahia kulindwa kwa lugha zetu asilia na kutambua pia kuwa bado ipo kazi kubwa ya kulinda kikamilifu matumizi ya lugha zetu, hasa Kiswahili. Bado tunatukuza lugha za kigeni kwa kiwango kikubwa na hatuoni umuhimu wa kuweka jitihada za dhati za kulinda na kukuza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.

 

Tunayo safari ndefu, lakini haielekei kama ni safari ambayo tutaikamilisha ikizingatiwa kuwa vipo vikwazo vikubwa mbele yetu.

Mfano mmoja unadhihirisha baadhi ya hizi changamoto. Nimekuwa naona picha ya aina mbili ya swala: mmoja anaitwa Thomson, na mwingine anaitwa Grant’s. Hawa swala wanapatikana Afrika peke yake na nimejiuliza sababu nzuri ya swala Waafrika kupewa majina ya Kizungu, na sipati jibu la kuridhisha.

 

Zipo sababu za historia ya ukoloni na hata ya utumwa ambazo zinaendelea kuathiri matumizi yetu ya majina na matumizi mengine ya lugha. Ukoloni ulijengwa juu ya msingi wa tabaka na hayo matabaka yalipewa hadhi tofauti na huduma za jamii ambazo ziliambatana na ubaguzi huo. Mpaka leo matumizi ya lugha ya Kiswahili yanabainisha historia hiyo na utasikia mijini kuna maeneo ya uzunguni, na ya uswahilini.

Hali halisi ya maisha iliyokuwa bora kwa Mzungu wakati wa ukoloni na ya dhiki kwa Mswahili imebaki kama mawazo ya kudumu kwenye fikra zetu hata baada ya kupatikana kwa Uhuru na ndiyo chimbuko la kutukuza vya wageni na kudharau asili yetu. Kila kitu cha Mzungu ni kizuri: yeye, majina yake, desturi zake, na hata mbwa wake.

 

Ukoloni wa mawazo ambao tumeshindwa kuupiga vita kikamilifu umechukua nafasi ya ukoloni tulioutimua Desemba 9, 1961. Matokeo yake ni kuwa hali ambayo si ya kawaida imeendelea kuonekana kuwa ni ya kawaida.

Swala aina ya Grant alipewa jina la mvumbuzi wa Uskoti aliyeishi kwenye karne ya 19, wakati swala aina ya Thomson ni jina la mvumbuzi mwingine wa Uskoti, Joseph Thomson. Hii ni hali ya kawaida kabisa kwa jamii ambayo haijivunii urithi wake.

 

Inawezekana kabisa kuwa tofauti za maendeleo ya jamii juu ya sayansi ya viumbe ndiyo chimbuko la awali la kuwepo majina tofauti kwa aina tofauti ya swala, pamoja na wanyama wengine. Lakini pia ukweli ni kuwa tumefumbwa na kukandamizwa mawazo na ukoloni na utandawazi kiasi kwamba hatuoni tena kuwa ndani ya lugha zetu za asili tunayo majina mbadala ya viumbe ambavyo tumeridhika kuviita kwa majina ya asili ya kigeni.

Lakini hata tukikubali ukweli kuwa si viumbe au vitu vyote vinaweza kuwa na majina mbadala ya lugha zetu asilia au Kiswahili, historia hiyo haizuii sasa kupatikana kwa majina ambayo yanaakisi mila, historia, na tamaduni zetu. Tusisahau kuwa si muda mrefu uliopita Zimbabwe ilikuwa inaitwa Southern Rhodesia, Zambia iliitwa Northern Rhodesia, na Burkina Faso ilikuwa inaitwa Upper Volta.

 

Muongoza wageni mmoja kanifahamisha kuwa tafsiri ya Kiswahili ya swala anayejulikana kama Thomson kwa Kiingereza ni Swala Tomi. Nimeona pia maelezo kuwa Grant’s anaitwa Swala Granti. Kwa jamii ambayo ina urithi mkubwa wa utamaduni mimi naona kama kutumia haya majina ni dalili ya uvivu mkubwa miongoni mwetu, na labda ishara ya kujidharau pia.

Wakati tunang’ang’ania majina ya Kiswahili yenye uhalisia wa kigeni, tunaacha majina mbadala yanayotokana na jamii zetu. Kwenye jamii ya Wangoreme wa Mkoa wa Mara, yapo majina tofauti kwa aina tofauti ya Swala, na hali itakuwa hivyo kwa majina ya viumbe miongoni mwa jamii ambazo zipo kwenye mazingira ya wanyamapori.

 

Ukombozi wa fikra unahitajika pia kwa wataalamu wetu wa lugha ya Kiswahili ambao wameacha majina yenye asili ya kigeni kushamiri na kuacha kutumia kikamilifu lugha zetu za asili kubuni majina mapya. Utafiti wa kina wa majina ya wanyama yanayotumika kwenye makabila yetu ungesaidia kuepuka kubandika jina Granti na Tomi kwa swala Mwafrika.

Tumetoka kuadhimisha mlolongo wa sherehe za kudumisha mila na tamaduni zetu. Lugha ni nguzo kuu ya utamaduni, na jitihada za kulinda matumizi ya lugha yanayozingatia urithi wetu ni njia muhimu ya kuanza kujikomboa kutoka kwenye utawala wa fikra unaotuelekeza kukuza ya wengine, na kupuuza ya kwetu.