Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ametoa kauli ya kijasiri kuhusu ushindi wa chama hicho, akitoa mfano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambao ni asilimia 42 pekee ya waliojiandikisha kupiga kura ndio waliojitokeza.
Nampongeza kwa dhati Komredi Bashiru kwa kuisimamia imani ile ya Mwana CCM ya “Nitasema Kweli Daima, Fitina Kwangu Mwiko.”
Nampongeza kwa sababu watu wenye uthubutu na wakweli kama Dk. Bashiru wanapungua kila uchao. Unaweza kusema kada hiyo ni sawa na ‘viumbe walio hatarini kutoweka.’

Ndani ya CCM kuna mahafidhina wanaodhani kusifu tu ndiyo njia inayoweza kukisaidia chama, serikali na viongozi wetu wakuu. Mara kadhaa tumeshauri na kuonya kuwa kujazana sifa na matumaini hewa si jambo la manufaa kwa CCM na kwa taifa.
Dk. Bashiru anashangazwa na uchache wa watu wanaojitokeza kupiga kura! Majibu anayo. Haya mambo tumeyasema, lakini kwa kuwa anayehoji na kutoa mapendekezo ya maana anaonekana ‘si mzalendo’, wengi wameogopa kuyasema.
Nampongeza Dk. Bashiru kwa sababu amesaidia kuwajibu wanafiki ambao kazi yao kuu ni kusifu na kuwavika wakubwa vilemba vya ukoka ilhali wakijua sifa na mapambio yao ni mauti ya chama.

Bila unafiki, leo kwenye jimbo langu naweza kujitokeza kupiga kura kama nafasi ya mbunge au diwani wangu imekuwa wazi kwa sababu za msingi au za asili.
Siwezi kujitokeza kwenda kupiga kura kujaza nafasi ya diwani au mbunge aliyehama chama, na mbaya zaidi, kumpigia kura yule yule aliyetoka chama kile halafu akapewa heshima ya kugombea nafasi ile ile katika chama hiki. Siwezi. Kwanini nishiriki dhambi ya kupoteza fedha za umma?

Wananchi si mazuzu, hata wanaohama hivi vyama si wajinga. Wana akili timamu. Wanajua wanachokifanya. Dosari ipo kwa hawa wanaowapokea na kuwapa heshima kubwa sana ya kugombea nafasi zile zile walizoziacha kule walikokimbia.
Moja ya matokeo chanya ya ‘shule za kata’ ni haya anayoyasema Dk. Bashiru, yaani watu kususa uchaguzi!  Shule hizi, pamoja na kasoro za kukosa walimu, vitabu, vyumba vya madarasa na mabweni; zimesaidia mno kuwafumbua macho Watanzania. Elimu wanayopata imesaidia mno kupembua mambo, hasa haya yanayogusa maisha yao ya kawaida ya kila siku.

Wanajadili aina ya mazingira walimosomea na kubaini kuwa yalisababishwa na ukosefu wa fedha. Wanajua fedha zinazotumika kwenye uchaguzi huu wa mazingaombwe kama zikipelekwa kwenye madawati au nyumba za walimu, zitawakomboa wengi. Haya mambo wanayaona. Wanayajua. Wanayajadili na kuyahoji, na yanawaumiza. Hitimisho lao ni kudharau mchakato mzima wa uchaguzi. Kwao, uchaguzi hauna maana! Ndivyo wanavyosema.
Watanzania wanaona nguvu kubwa, hila, dhuluma, vitisho na uonevu kwenye uchaguzi.

Watanzania hawa hawa wanaomwona mkuu wa mkoa akisherehekea na polisi kwa kula na kunywa baada ya ushindi wa chama tawala, hawawezi kuwa punguani hata wajitokeze tena kushiriki uchaguzi wa aina hiyo hiyo katika kata au jimbo jingine.
Wapiga kura wanaona namna masanduku ya kura yanavyojazwa kura zilizopigwa nje ya vituo vya kura. Wanaona namna mawakala wa upinzani wanavyobaguliwa na kuswekwa rumande ili kutoa mwanya kwa wagombea fulani fulani kushinda kiulaini. Wanawaona polisi wanavyokuwa ni polisi wa chama tawala badala ya kuwa polisi wa Watanzania. Mwaka 2012, katika Mkutano Mkuu wa 8 wa CCM, Mwenyekiti Jakaya Kikwete aliwambia Wana CCM: “Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu tutakwisha na tutakwisha kweli.”

Kwa maneno mengine, Kikwete alitaka CCM wakabiliane na mambo kwa hoja na kwa haki badala ya kutegemea maguvu ya polisi. Je, busara hii imetekelezwa? Hakuna.
Wapiga kura wanajua hata wapige kura wakiwa wanamwaga machozi, mshindi ni yule anayetangazwa na msimamizi wa uchaguzi anayelindwa na polisi.
Watanzania wasiojitokeza kupiga kura ni wale wanaoamini kuwa wapige au wasipige kura, mshindi anajulikana! Kituo kina wapiga kura 50, lakini matokeo ya mwisho yanaonyesha waliopiga kura ni 400. Tunamdanganya nani? Kama hivyo ndivyo, kwanini watu wahangaike kupanga foleni?

Dk. Bashiru bila shaka anakumbuka zamani zile ambazo mgombea aliposhinda uchaguzi hali ilikuwaje. Kwa hakika ilikuwa shangwe na vigelegele kwa kambi iliyoshinda. Leo hali ya mshindi na aliyeshindwa zinafanana! Aliyeshindwa hanung’uniki, maana alishajua matokeo mabaya kabla ya upigaji kura; na aliyeshinda hasherehekei kwa sababu nafsi inamsuta! Anajua ushindi wake ni wa dhuluma. Hata darasani anayeshangilia ushindi ni yule aliyeshinda kwa haki, si aliyepewa majibu ya mitihani.
Mwisho, nirejee kumpongeza Dk. Bashiru kwa kuwa mkweli. Kauli yake ifungue ukurasa wa mjadala ili tupate majawabu kwa haya yanayomuumiza kichwa. Tiba ya haya ni kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki utakaomfanya kila mpiga kura aone thamani ya kura yake. Lakini kama ni uchaguzi ambao mshindi anajulikana kabla ya kupigwa kura, naamini kwa dhati kabisa idadi ya wapiga kura itazidi kuporomoka kila uchaguzi. Hongera Dk. Bashiru kwa kuwa mkweli japo kauli yako itasababisha uchukiwe na mahafidhina ndani ya CCM.

Please follow and like us:
Pin Share