NA MICHAEL SARUNGI
Uwezekano wa kupata medali katika mashindano yajayo ya Jumuiya ya Madola yanayotarajiwa kuanza Aprili 4
hadi 15 mwaka huu katika mji wa Gold Coast nchini Australia, utakuwa mkubwa endapo kila mmoja atatekeleza
jukumu lake ipasavyo.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti juu ya maandalizi ya timu ya Tanzania inayotarajiwa kushiriki
katika mashindano hayo, wanariadha wakongwe na wadau wengine wa michezo wamesema vijana wanapaswa
kupewa maandalizi ya kisayansi kulingana na hali iliyopo.
Filbert Bayi, aliyeweka rekodi ya dunia katika mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 1974 katika mbio za
mita 1,500 huko Christchurch, New Zealand, amesema hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio ila kinachotakiwa ni
maandalizi na wachezaji wenyewe kujitambua.
Amesema licha ya mamlaka husika kuwa na jukumu la kutoa huduma stahiki kwa wachezaji kambini, lakini
kikubwa ni mchezaji mwenyewe kutambua nini anachohitaji kuelekea katika mashindano hayo yenye hadhi kubwa
duniani.
Amesema kwa miaka mingi wanariadha wa Tanzania wameshindwa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali
kutokana na maandalizi duni pamoja na wanariadha wenyewe kushindwa kujitambua na kujua nini wanataka.
Amesema kuna sababu nyingi zinazochangia michezo nchini kuzorota, lakini kubwa ni wanamichezo wenyewe
kushindwa kuelewa kuwa michezo kwa sasa ni ajira kubwa inayoweza kumwingizia mtu fedha nyingi tofauti na
miaka ya nyuma.
Mwanariadha mwingine mkongwe aliyetamba katika michuano ya Olimpiki mwaka 1984 nchini Marekani, kwa
kushika nafasi ya sita kwa kutumia saa 2:11:10 na ile ya mwaka 1988 huko Soul, Korea Kusini, Juma
Ikangaa amesema wawakilishi hao wanapaswa kuelewa umuhimu wao kwa Taifa kabla ya yote.
Amesema licha ya kambi zao za mazoezi kukabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini pia wanapaswa kuwa na
jitihada binafsi ya kuelewa kuwa Watanzania zaidi ya milioni 55 wapo nyuma yao wakitarajia kuwakilishwa vyema.
Anasema ili kufanikisha hilo, kila mdau anapaswa kutimiza wajibu wake kuanzia kwa Serikali na mamlaka zake
zote bila ya kuingiza siasa katika maandalizi haya, na pia wajengwe kisaikolojia wawe tayari kwa kushindana.
Kocha mkuu wa timu ya riadha ya Tanzania inayojiandaa na mashindano hayo, Zakaria Barie, amesema vijana
wapo vizuri na wanaendelea na mazoezi licha ya changamoto ndogo ndogo za kibinadamu ambazo zinafanyiwa
kazi.
Amesema mamlaka husika tayari zimekamilisha majukumu ya kuiweka timu kambini na kutoa huduma stahiki
kilichobaki ni kwa wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha wanatoa uwakilishi wenye tija kwa Taifa la Tanzania.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilipata medali katika mashindano hayo mwaka 1970 wakati Titus Simba alipotwaa
medali ya fedha katika michezo, iliyofanyikia huko Edinburg, Scotland.
Amesema Tanzania ina medali 21 tangu imeanza kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1966, ikiwa ni
miaka 52 tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza, hali ambayo imeendelea kufedhehesha.
Tanzania ilipata medali nyingine za ndondi kupitia kwa Willy Isangura aliyepata medali ya shaba michezo hiyo
ilipofanyikia Brisbane, Australia mwaka 1982, na michezo iliyofuata iliyofanyika mwaka 1990 Auckland, New
Zealand; Haji Ally pamoja na Bakari Mwambeya walipata medali za fedha na shaba katika uzito tofauti.
Mwaka 1994 michezo hiyo ilifanyikia Vancouver, Canada, na bondia Hassan Matumla alitwaa medali ya fedha
katika michezo hiyo.
Tanzania ilitwaa medali yake ya kwanza ya dhahabu katika ndondi pale bondia Yombayomba alipotwaa medali
katika michezo ya 1998 ilipofanyikia Kuala Lumpur, Malaysia.
Mchezo wa riadha ndiyo unaoongoza kuiletea Tanzania medali nyingi baada ya kukomba jumla ya medali 15 za
aina tofauti tofauti, huku ndondi ikitwaa medali 6 kutoka katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola na mingine kwa
nyakati tofauti.

Huo ndiyo uliokuwa mwisho wa mabondia wa Tanzania kutwaa medali katika michezo hiyo ambapo miaka ya
2006, 2010 na 2014 hakuna bondia aliyerudi na medali yoyote.

1287 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!