Tuwakubali Ili wakubalike

Vipaji vipo kila kona ya dunia, lakini ili kipaji kikue ni lazima kwanza kikubalike nyumbani kabla hakijakubaliwa ugenini. Kipaji hakipatikani shuleni, kipaji unazaliwa nacho na unakua na kutembea nacho, na ili kipaji kionekane na watu wengine unatakiwa ukioneshe.

Ukioneshe kwa kuthubutu kufanya kile unachokiona unakiweza, na baada ya kuonesha ndipo watu wanapoona kwamba kumbe unaweza.

 

Watanzania wengi wanaweza lakini hata pale wanapoonesha kwamba wanaweza mbele ya Watanzania wenzao, badala ya kuwakubali wameishia kubezwa na kupuuzwa na mwishowe wamejikuta kama kwamba wamefanya yale ambayo hayakubaliki katika jamii.

 

Hakuna kitu cha maana katika kujaribu kama

kukubalika (moral support). Ukikubalika unajijengea katabia fulani ka kujiamini ambako kanakuongoza uendelee kuthubutu na kufanya vizuri na vizuri zaidi. Huu ni utaratibu wa dunia ambao kila jamii inauabudu.

 

Miaka 50 hadi 70 pamoja na kwamba Wamarekani weusi walikuwa na vipaji vingi hasa vya michezo na kuimba, lakini walishindwa kuendeleza vipaji vyao kwa vile kulikuwa na siasa za ubaguzi zilizowatenga watu kulingana na rangi za ngozi zao. Hivyo watu weusi wenyewe walibaguana na wakashindwa kuvitambua vipaji vya weusi wenzao, kitu kilichowafanya wasikubalike kitaifa na hata kimataifa.

 

Ni miaka ya 1980 tu ambapo zilianza kampeni kabambe miongoni mwa mweusi kuwakubali weusi wenzao, kitu kilichosukuma hata wakakubalika kitaifa na kimataifa.

 

Nchi za kusini mwa Asia (Korea Kusini, Malaysia, Thailand, Singapore na Indonesia) kwenye miaka ya mwanzoni ya 1960 zilikuwa nyuma ya Tanzania kimaendeleo. Walianza kuiga, kubadili na kuboresha (coping, adapting and innovating) wakakubalika kwanza nyumbani na baadaye dunia ikawakubali, jambo ambalo hadi leo wamekuwa viongozi wa teknolojia mbalimbali duniani.

 

Nikirudi kwenye picha yetu hapo juu, ambayo inaonesha vijana wa Kitanzania wakiwa wamefanya utundu wa kuiga na kuboresha mashine ya kuchezea mchezo wa Billiard au kwa jina maarufu hapa nyumbani pool table (puli); mchezo huu unachezwa na watu matajiri katika nchi zilizoendelea, lakini hapa kwetu billiard anacheza kila mtu hata asiyeweza kumiliki dola moja kwa siku anacheza.

 

Kwanza ni jambo la busara kama tutaweza kuwapongeza vijana hawa, waliotumia ubunifu wa hali ya juu kwa kutengeneza mashine ya puli kwa kutumia malighafi ya udongo na miti ambayo ni sahihi kwa kupambana na uharibifu wa mazingira, vijana hawa wamekuwa wabunifu na wamejali mazingira kuliko hata Wazungu, ambao wamekuwa mawakili wa uharibifu wa mazingira kwa miaka mingi, lakini mashine zao zimekuwa zikitengenezwa kwa mbao na plastiki ambazo zinachafua mazingira.

 

Sina budi kusema kwamba tuwakubali vijana hawa ili waboreshe vipaji vyao kwa kutengeneza mashine billiard za udongo wa mfinyanzi ambao utachomwa na kuwa kama chungu, ili hata mvua ikinyesha isiharibike na iweze kudumu kwa muda mrefu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewafungulia njia ya kukubalika kitaifa na hata kimataifa.

 

Mwanasiasa anapokuwa jukwaani akihutubia, atashuka kutoka jukwaani mara moja na kuanza kukimbia kama kila atakalozungumza watu watamzomea, lakini kama atakuwa anashangiliwa kwa kupigiwa makofi ataendelea kuhutubia na huku akiendelea kuiboresha hotuba yake hapo hapo jukwaani.

 

Na sisi kama tunataka vijana hawa waendeleze vipaji vyao vya utundu wa kubuni na kuiga vitu ambavyo Wazungu wanatumia fedha nyingi na muda mwingi kuvitengeneza, basi nawaombeni tusiwabeze bali tuwakubali ili wakubalike, kitu ambacho kitawafanya waendelee kukuza na kuboresha vipaji vyao.

 

Mobile: 0782 000 131

Email: [email protected]