Kuna njama za kuhujumu utu wa mtu na uchumi wa Mkoa wa Morogoro. Njama ambazo zinatekelezwa usiku na mchana na baadhi ya watumishi wa umma wakishirikiana na vibeberu uchwara waliomo mkoani humo. 

Mkoa wa Morogoro una ardhi ya rutuba kwa kilimo na ufugaji na Hifadhi ya Wanyama ya Mikumi ambayo ni kivutio kwa watalii. Vipo viwanda kwa wafanyakazi na vyuo vya elimu ya juu kwa wasomi na wataalamu. Wafanyabiashara na wakazi wananufaika na mazingira ya mkoa kutokana na shughuli mbalimbali za uchumi.  

Sifa hizi na nyinginezo kama vile misitu ya kijani kibichi, hewa safi na majira ya kipupwe, baridi, masika na kiangazi huwavutia na kuwapendeza wasafiri wapitao na wageni waingiao Morogoro kwa mapumziko mafupi. Burudani ya kuangalia maji yakitiririka milimani inakonga mioyo ya watu wa Morogoro. Hakika Morogoro yapendeza. 

Morogoro hii ya wahenga na mashujaa kina Kingalu, Rukwele, Kingo, Hega na wengine imetiwa nuksani na baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu. Kwa vile kila jambo au kitu kina ncha au namna mbili, mkoa huu umejikuta katika sampuli hiyo. Nzuri na mbaya, tamu na chungu, chanya na hasi na kadhalika. 

Namna kama hizi zinatokana na tabia ya mabadiliko ya nchi na mwenendo wa watu na viumbe vilivyomo katika sehemu husika. Hali kama hiyo ikitokea hushitusha, hushangaza na huhuzunisha watu waliomo katika eneo hilo. 

Mwezi uliopita Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, alifanya ziara katka Mkoa wa Morogoro kukagua na kuangalia shughuli za maendeleo zinavyotekelezwa na wananchi na kusimamiwa na serikali, ambayo yeye ndiye msimamizi mkuu. 

Ziara hiyo imetoa picha mbili. Mosi, wananchi wamekutwa katika kutekeleza majukumu ya ujenzi wa taifa lao. Pili, kuibuliwa njama za kuhujumu uchumi na utu wa wakazi wa mkoa huo. Njama hizo zinatekelezwa na watumishi wa umma wachache walioaminiwa, kumbe hawana punje ya wema na uaminifu.  

Haikuwa furaha ila huzuni kwa Waziri Mkuu, Majaliwa. Kwa masikitiko makubwa akasema, ninanukuu: “Mkoa huu tuna shida ya makusanyo ya fedha na namna zinavyotembea kwenda kwa matumizi ya wananchi. Halmashauri zinashindwa kutekeleza si kwamba hampati fedha, mnapata fedha. Lakini fedha zenu haziendi kwa wananchi. 

“…kule vijijini mnakusanya bilioni 3. Mniambie kama mna mradi wowote wa milioni 200 wa pamoja. Hamna!  Hamna! Halmashauri zinakusanya bilioni 3, bilioni 4 na nyingine bilioni 12, lakini hakuna kituo cha afya hata kimoja. Fedha zinakwenda wapi? Kula! Hatuwezi kukubaliana nayo.” Mwisho wa kunukuu. 

Lahaula! Kumbe bado wapo Watanzania wenzetu wanatamani kuhujumu uchumi na kupinga kuwako maendeleo kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro. Watumishi saba wanatuhumiwa kuchota fedha ya umma kiasi cha Sh bilioni 1.3 bila idhini ya serikali na kutumia kwa mambo yao binafsi. Wanatakiwa kuzirejesha fedha haraka iwezekanavyo. 

Hii si taarifa njema kwa serikali, wakazi wa Morogoro na hata kwa Watanzania wema. Wanalaani matendo haya. Nichukue nafasi hii kwa niaba ya Watanzania kutoa pole, heko na kongole kwa Ofisa wa IT mkoani humo, kijana John Mvanga, kwa kufichua njama hizi. Serikali imemrudisha kazini Mvanga kwa kusimamishwa kazi na wakubwa wake kazini, eti kufichua njama zao. Lo, salalaa!  Hawana haya wala hawajui kuwa ni vibaya. Makubwa! 

Taarifa hii inauma na ni nzito kubebwa na moyo wa mzalendo yeyote, kwani ina sumu ya kuua nguvu na kasi ya kujenga uchumi na kutoa huduma za afya, elimu, maji na barabara kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro. 

Mkoa wa Morogoro umetuonyesha na kutukumbusha kwamba wahujumu utu na uchumi pamoja na kupinga maendeleo ya jamii bado wapo nchini. Ni vema tukaangalia na mikoa mingine. Mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam imeonyesha dalili. Macho yaelekezwe huko na katika mikoa mingine nchini. 

Kabla ya kupata uhuru mwaka 1961, tulikuwa na sababu za kuhujumu uchumi wa wakoloni wanyonyaji, si uchumi wetu. Baada ya uhuru hatukuwa na sababu, uchumi ni wetu. Kwa kupuuza saburi na baadhi ya Watanzania kulaghaiwa na mabeberu tukajisaliti na kujihujumu.  Cha moto tumekipata. 

Hivi sasa tunavyojikosoa, tunavyojitambua na tunavyojali saburi, kweli tunatamani kuhujumu uchumi wetu, kulikoni? Hiki tulichonacho kibindoni tusikichezee. Kikitutoka tutalia na kusaga meno. Tukumbuke: “Msiba wa kujitakia hauna kilio.”

5448 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons