Tanzania ni kisiwa cha amani. Kauli hii imezungumzwa mara nyingi na kuwabwetesha Watanzania. Nchi kwa sasa ina mtihani mgumu. Kuna mtihani wa Uchaguzi Mkuu, unaopaswa kufanyika Oktoba, mwaka huu na Katiba Inayopendekezwa inayodhaniwa kuwa kura ya maoni itafanyika Julai, mwaka huu.
Tunadhani kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa itafanyika Julai kutokana na maelezo ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva. Kura hii ilikuwa ifanyike Aprili, lakini Mkoa mmoja wa Njombe ukachukua zaidi ya miezi miwili kuandikisha wapigakura katika daftari kwa kutumia mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR).


Hapa katikati imeibuka hofu kuwa kuna uwezekano wa kusogeza mbele Uchaguzi Mkuu kutokana na daftari la wapigakura kutokamilika. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameionya Serikali kuwa Uchaguzi Mkuu ukisogezwa mbele nchi ‘itapungua’.
Baada ya kauli hii ya Mbowe, Jaji Lubuva amejitokeza hadharani na kusema kuwa uchaguzi uko pale pale na akasema Kenya waliweza kujisajili wapigakura kwa siku 36 nchi nzima na Nigeria walitumia miezi miwili tu kusajili wapigakura milioni 70.


Tunachokiona Jaji Lubuva amesahau kuwa Kenya miaka yote wanavyo vitambulisho vya taifa. Nigeria nao wanavyo vitambulisho vya taifa. Hivyo kwa nchi hizo zilichofanya ni kuboresha takwimu ambazo tayari zipo. Hapa kwetu kuna kila dalili kuwa vitambulisho vya taifa vimekwama.
Hata waliojaza fomu za maombi siku nyingi hawajapewa. Hata matangazo ya mara kwa mara yaliyokuwa yanatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa sasa hayaonekani. Kilio kila kona ni ukata. Kila kona tunaelezwa kuwa Serikali haina fedha.


Tukirejea katika wazo la kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa, sisi tunaamini kwa sasa hili tungeliacha hata kulizungumzia. Tukubali kuwa hata Katiba Inayopendekezwa ikipigiwa kura tujue haitatumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mwezi Julai Bunge litakuwa tayari limevunjwa. Katiba haiwezi kufanya kazi bila kuwapo Bunge, likatunga sheria mbalimbali na kuhuisha sheria zilizopo baada ya Serikali kuandaa sera zikapitiwa na wadau, wakaweka mawazo yao na kuafikiana aina ya sheria waitakayo.


Serikali inaweza kutumia utaratibu wa kuitisha Bunge Maalum, kisha ikawasilisha miswada kadhaa chini ya hati ya dharura baada ya Katiba Inayopendekezwa kupitishwa, lakini ijue ikifanya hivyo itachochea vurugu katika Taifa hili. Itawafanya Watanzania watilie shaka zaidi nia ya Serikali katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.


Sisi tunasema pamoja na uzuri au ubaya wa Katiba Inayopendekezwa, muda si rafiki yetu. Tunachopaswa kufanya sasa ni kuweka mawazo pamoja kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaoanzia ndani ya vyama katika wiki sita zijazo, hadi kwenye Tume.
Tunahitaji muda wa kampeni kwa vyama kunadi sera na wananchi kuzitafakari. Hakika kama tunataka kuliepusha Taifa la Tanzania na vurugu, suala la Katiba Inayopendekezwa kwa sasa tuliweke kando. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri