MOJA ya mambo ambayo huwa nawapendea baadhi ya viongozi wa Marekani ni msimamo wao kwenye mambo ya msingi. Sisemi kwamba viongozi wetu hawana msimamo la hasha, chonde chonde msinihukumu hivyo, lakini tangu zamani, kama si nguvu ya Marekani na maswahiba wake, wengi wangekuwa wameshaumia.

Pamoja na uwezekano wa kuwepo uonevu kwenye operesheni zake mbalimbali, lakini ndugu zangu tukubali baniani mbaya kiatu chake dawa na mpe shetani haki yake. Nimeangalia picha za rafiki yetu Mwingereza aliyetoka Syria wiki moja iliyopita, kweli huwezi kuamini wala kula nyama kwa muda kama una roho nyepesi.


Watu wanachinjwa kama kuku wagonjwa nakwambia; ingekuwa wenye hatia kama inavyofanyika China nisingekuwa nalalamika sana. Lakini hapo Syria ni watu wasiojiweza kabisa kwa nguvu ya mwili – wanawake, watoto, wazee na watu waliopata njaa ya muda mrefu na kujifungia ndani ya nyumba zao kwa kuogopa mitutu ya majeshi ya serikali.

 

Kuna jamaa kwenye mitandao jamii niliwaona wanaguna waliposikia taarifa ya Uingereza kwenda lwake Syria kama Umoja wa Mataifa hautatoa uamuzi na maelekezo ya kueleweka. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague alisema zaidi ya mwezi sasa kwamba Uingereza inaweza kuchukua hatua zake kama diplomasia itashindwa.


Kweli kama binadamu wote ni sawa na Syria inao binadamu, basi hebu wote tuungane na Hague katika hili bila kumung’unya maneno wala kuogopa, tukawakomboe watu wa Syria. Nasema haya kwa uchungu kwa sababu kama daktari niliwahi kwenda kwenye maeneo yalipotokea mapigano kutibia watu, na najua madhara ya mashambulizi ya silaha dhidi ya watu ambao hawana silaha.


Potelea mbali kama vita haina macho, lakini dunia ya kistaarabu haiwezi kukaa kimya kuona masikini wa Syria wanauliwa na rais wao, Bashhar Assad, eti ili tu ang’ang’anie kwenye madaraka. Iko wapi sasa nguvu ya Umoja wa Mataifa na yale mataifa wakombozi wa wanaoonewa?

 

Urusi na China kweli zimekuwa na roho ya chuma mpaka zikaamua kukataa walau kupitisha tu azimio la kulaani na kuchukua hatua dhidi ya akina Assad? Biashara ya silaha na mafuta haitakuwa endelevu kiasi hicho, na Warusi wanatakiwa kujua mapema kabisa na kukaa upande wa wanyonge. Wamesahau jinsi Daudi alivyompiga Goliathi?


Hata kama wao hawataki kwenda kupigana pale, wawaachie Marekani na Uingereza najua wapo tayari kwenda au kutumia namna watakavyoona safi kuwakomboa watu ambao sasa wamewekwa kwenye sufuria la moto wanaungua wakiona. Najua mijadala inaendelea hapo 10 Downing Street na White House, hebu viongozi wetu vijana wa mataifa makubwa tumieni mbinu za medani muokoe watu wetu wa Syria.

 

Bila kumaliza tatizo la Syria hapatakalika Mashariki ya Kati, na sasa vita imelipuka mtindo mmoja, lazima wakubwa waingie pale watie adabu majambazi wanaoleta rabsha. Wanataka bei ya mafuta ije kutunyongea shilingi yetu? Tumechoka na chinja chinja inayoendelea, tunataka kuona mwisho wake, badala ya kila siku makanisani na misikitini sala za kuombea amani Syria bila hatua.

 

Imani bila matendo si tulishaambiwa imekufa? Sasa tunangoja nini? Hatuwezi kwenda kutibu marehemu, labda tukawatibu majeruhi sasa, inaumiza sana.

leejoseph2@yahoo.com


1241 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!