Uamuzi wa Busara (11)

Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara tulisoma jinsi Katiba ya TANU inavyoelekeza kuwa raia wote watamiliki utajiri wa asili wa Tanzania kama ahadi na dhamana kwa vizazi vijavyo. Wiki hii ni mwendelezo wa tulipoishia. Endelea…

Makabila, kisha na baada ya Uhuru, walikuwa polepole wanajinyakulia ardhi na bila kuitumia au kuifanyia mabadiliko yoyote yenye kuwa dhalimu, waliwauzia wanyonge au makabaila wenzao.

Kwa ghafla tuligundua ardhi yote iliyo nzuri katika sehemu fulani imetwaliwa. Baya zaidi ni kwamba waliwafanyisha kazi

wanyonge na maskini ndugu hawa na pato la kazi hiyo ngumu ilimfaidia mtu mmoja, au kikundi fulani zaidi.

Mwaka hata mwaka hali ya Maganga ilizidi kudidimia. Hivyo mabepari na makabaila wanapoona kuwa sasa wananchi

wanatekeleza matakwa yao kama yalivyo katika katiba yao wakaanza kuwavuruga wananchi hao kwa njia nyingi.

Wangependa walione Azimio la Arusha linakufa, kusahauliwa na kutokomezwa. Wangefurahi kuona chama na serikali yake vinaunga mkono unyonyaji na kuutungia sheria za kuulinda. Katu, haitawezekana. Anayewaza hivi atakuwa anaota ndoto.

Maelezo haya yalikuwa msingi wa kwanza wa Azimio la Arusha. Wengine wangependa labda wajiulize, kama iwapo msingi mkubwa wa Azimio la Arusha ni Katiba ya TANU, kwa nini katiba hii haikutekelezwa tangu mwaka 1961 tulipopata Uhuru na kuongoza hadi mwaka 1967?

Ukweli ni kwamba si kama haikuwa inatekelezwa katiba yote ila zilikuwepo sehemu mbalimbali zinatekelezwa. Mara tu

baada ya Uhuru mishahara ya viongozi wa siasa serikalini ilipunguzwa. Mshahara ambao mawaziri wa kikoloni walikuwa

wanapata si sawa na huo ambao mawaziri wetu wanaupata.

Hizi zilikuwa baadhi ya hatua za mwanzo za kujali hali ya mtu wa kawaida. Hatua hii ni ya maana sana kwani tangu awali

viongozi wetu walitambua ni watu wa namna gani walikuwa wanatuongoza.

Katika kijitabu TANU na RAIA uk. 5 tunasoma hivi: “Leo tumeanza baragumu la pili. Baragumu hili ni la kuongeza utajiri wa nchi yetu. Mwanzo tuliomba kila mwananchi ashirikiane na wenzake ili kumwondoa mkoloni na kuondoa umaskini.”

Usemi huo ulitolewa mapema kabla ya kupata Uhuru na ilipofika mwezi Aprili, 1962 ndipo TANU ikaanza kuitekeleza

katiba yake. Ili wananchi tujione kweli tuko huru, maadui wetu watatu tuliwatangaza hadharani; UMASKINI, UJINGA na MAGONJWA na kuanza mara moja kuwapiga vita.

Mambo ilibidi yaende hatua, kwani Uhuru tulikuwa tumepata lakini kazi kubwa mbele yetu ilikuwa kuuimarisha Uhuru wetu.

Kazi hii haikuwa rahisi. Mkoloni alipoona bendera yake imeng’oka naye akakata shauri aondoke. Je, nani ashike nafasi yake? Ni wazi Maganga, wananchi walikuwa wanataka kuona kuwa kweli serikali ilikuwa yao. Wakati huo hatukuwa na watu wa kutosha wenye ujuzi kama Smith.

Pengine ilitubidi tuazime walewale ili watusaidie, kitu ambacho yeyote aliye huru asingependa aone ofisi zake zimekaliwa na walewale ambao matendo yao yaliudhi hivi kwamba tukakata shauri tuwaondoe.

Kazi hii na nyingine nyingi zilituchukua muda ingawaje si mrefu mno ukilinganisha na hali ambayo Mwingereza alituacha.

Wakati uimarishaji huo unaendelea na mipango kadha wa kadha ya maendeleo inapangwa, mambo mapya ambayo kabisa

yalikuwa yanapingana na lengo letu yakaanza kuzuka kwa wingi. Maganga si tu amechukua kiti cha mkoloni, bali pia amerithi mshahara ambao mkoloni alikuwa anaupata na hali kadhalika nyumba na mengine mengi. 

Mkoloni hakuwa anakaa na Waafrika kule Uswahilini, kama watu walivyokuwa wamezoea kukuita. Maganga pia ilimlazimu akae kule, kwani nyumba iko kule. Si Maganga peke yake bali pia Kaberege, Mwanjela, Luwatu na hata Kihenga akawemo katika kundi hilo la kuchukua vyeo vya wakoloni. Jambo hilo lilikuwa la lazima ili kukamilisha Uhuru wetu tuliorudishiwa.

Lakini wengine kati ya ndugu zetu akina Kaberege, Maganga na Kihenga kwa kupata nafasi hiyo, wakasahau kabisa kule

walikotoka. Badala ya kukaa chini katika viti hivyo ili kutengeneza mipango ya kuinua hali za wananchi na kuwafanya

wapone vidonda vya dhuluma za unyonyaji, wakaingiwa tamaa zilezile za wakoloni.

Kwanza, walijiona kuwa wao si sawa na wenzao waliobaki nyuma na wakaanza nao kuotesha mirija yao na kuanza hali ile

ile ya unyonyaji kama walivyokuwa watawala wale. Mikopo kadhaa ikachukuliwa na kujenga majumba makubwa na mengi na kuwapangisha wenzao ilhali wao wanazo nyumba za kulala walizopewa na serikali kwa malipo hafifu na pengine bila

malipo.

Wengine wakaanza kujipatia magari ya kifahari na kunywa pombe za bei ya juu, hivyo kustarehe vya kutosha.

Wengine wakawa wanaotesha mirija huko vijijini na kuwafanya ndugu hao wa huko wawafanyie kazi na kupata faida kubwa kwa jasho la ndugu hao vijijini.

Kibaya zaidi ni kwamba wengine walijiona kuwa sasa wao si sawa na Waafrika wenzao na kudiriki hata kuwadharau wale

ambao ndio waliokuwa askari hodari katika vita ya kuleta Uhuru. Ndugu hao (wengi kati yao), licha tu ya kuanza unyonyaji wakawa kabisa watu wengine. Mwendo ulianza kubadilika ili kufanana na Smith, Kiswahili kabisa kilidharauliwa na kulikuwa na sauti ya Kiingereza na fikira zao ni kama zinaelekea kule kule.

Hata waliokuwa chini yao wakawa wanapewa mfano ule kuwa: “Na mimi siku moja nitakuwa kama Maganga.” Wananchi

waliyaona yote hayo na kuyaangalia kwa makini sana. Wengine wakawa wanadai kuwa mishahara ambayo walikuwa wanaitumia kwa kuwakoga ndugu zao, haitoshi ili iwawezeshe kuendelea na mtindo huo.

Hapa ndipo pakaanza kuwa na majina ya ‘NAIZESHENI AU NAIZA’. Maana yake ni kwamba aliyefaidi uhuru; na

‘KABWELA’ yaani yule ambaye hajaona faida ya Uhuru.

Tukaanza kugawanyika katika makundi mawili. Chuki ikazuka. Mwafrika na zaidi Mtanzania mwenye moyo wa kusaidia na katika kila aina ya dhiki, tukawa tunapoteza moyo huo. Wengine kati ya ndugu hao waliwahi kufukuzwa kwenye

mabasi ya hapa mjini na kuambiwa walikuwa wanawabana bure.

Walikuwa wanawaonyesha kule ambako wenzao walikuwa wanapita – Kwa wenye magari ya binafsi. Si hayo tu, pengine

ndugu hao wenye magari walipatwa na maafa ya kugongana na mti au wao kwa wao. Badala ya kumsaidia haraka kama ilivyo kawaida yetu, kabwela alifurahi na kusema: “Naiza kapatikana.” Haya ni mambo ya hatari kwa taifa.

Huko vijijini kelele zikaanza kusikika. Ndugu wanajiuliza kama kulikuwa na tofauti yoyote baina ya kipindi hiki cha Uhuru na wakati wa mkoloni. Swali hili linaulizwa kwa sababu hapakuwa na mipango safi na wazi au jitihada ya kujaribu

kumwongoza ndugu wa kijijini ili naye atumie juhudi yake na ainuke kiuchumi, hivyo apate maendeleo.