Waziri Mkuu (mstaafu), Edward Lowassa, mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya uamuzi mwingine mgumu katika maisha yake ya kisiasa. 

Kama ilivyo kawaida yake katika kufanya uamuzi mgumu kwenye maisha yake ya uongozi nchini, Lowassa alirejea katika Chama chake cha awali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitokea Chama kikuu cha upinzani – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). 

Uwepo wa Lowassa Chadema katika kipindi chake cha miaka mitatu umekuwa wa manufaa kwa chama hicho pengine na kwa taifa kwa ujumla. Vilevile uwepo wa Lowassa CCM kwa miaka mingi kabla ya kutimkia upinzani umekuwa wa manufaa kwa chama hicho pengine na taifa. 

Jambo moja la uhakika ni kwamba, uamuzi huo wa hivi karibuni wa mwanasiasa huyo umezingatia mengi, lakini kubwa zaidi miongoni mwa hayo ni kulenga kuunganisha maarifa na uzoefu wake katika kuitumikia nchi pamoja na viongozi wengine wa sasa serikalini, hasa Rais Dk. John Magufuli. 

JAMHURI tunaamini kwamba mchango wa Lowassa katika Serikali ya Awamu ya Tano ni muhimu katika kuinufaisha nchi, kwa hiyo tunazidi kutoa mwito kwa viongozi hawa wawili; Rais Magufuli na Edward Lowassa kuzidisha ukaribu wao na viongozi wengine nchini kwa manufaa ya taifa. 

Tunaamini uzoefu na maarifa ya Lowassa katika masuala ya uongozi, sambamba na uzoefu na maarifa ya wastaafu wengine katika awamu zote za uongozi wa taifa hili, ni muhimu katika kulisogeza mbele gurudumu la maendeleo, hasa katika nyakati hizi ambazo serikali inajitahidi kurekebisha makosa kadhaa ya kiutawala yaliyowahi kufanyika miaka ya nyuma, sambamba na kubuni njia bora zaidi zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla. 

Ni kweli Lowassa angeweza kutoa ushirikiano kwa Magufuli na serikali yake akiwa bado Chadema, hata hivyo ni kweli kwamba kwa mazingira ya sasa ufanisi unaotokana na ushirikiano wa Lowassa kwa Magufuli na serikali kwa ujumla unapata nguvu zaidi akiwa ndani ya CCM. Tunawatakia ushirikiano mwema kwa manufaa ya taifa. 

783 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!