Kwa  maana yake halisi uchaguzi ni njia ya msingi ya jamii ya kujipatia viongozi kidemokrasia.

Sifa mojawapo ya uchaguzi wa kidemokrasia au wa huru na haki ni uchaguzi kufanyika kwa siri. Sifa nyingine ni uchaguzi kufanyika mara kwa mara katika vipindi vinavyoeleweka, uchaguzi kutoa fursa sawa kwa wagombea wote, na uchaguzi kuruhusu waangalizi wa ndani na wa nje kuwafuatilia.

Katika Afrika hakuna uchaguzi huru na wa haki. Kwa maneno mengine hakuna uchaguzi wa kidemokrasia; kwa jumla uchaguzi katika Afrika hugubikwa na ubinafsi, wizi wa kura, rushwa na udanganyifu.

Katika mazingira hayo ni wazi katika Afrika uchaguzi hauna maana. Ni kupoteza wakati na fedha kufanya uchaguzi barani Afrika.

Ukitaka kusema kweli, chaguzi za Bara la Afrika huvurugwa na vyama tawala. Utakuta, kwa mfano, kila unapofika uchaguzi chama tawala kinawaletea wapiga kura (wananchi) ilani (ahadi za utekelezaji) lakini ikishinda uchaguzi inatekeleza ahadi chache sana.

Kwa hiyo, unapofika uchaguzi mwingine chama tawala kinakuja tena na ahadi zile zile za kuwaletea wananchi maji, elimu bora, huduma bora za afya, barabara na kadhalika.

Katika mazingira hayo ya kurudiwarudiwa ahadi zile zile, wananchi hutambua kwamba chama tawala kinawadanganya na kinachezea akili zao. Kwa hiyo, hujipanga kukichagua chama cha upinzani.

Chama tawala kikitambua kuwa wananchi wamejiandaa kukitoa hutumia mizengwe, rushwa, na wizi wa kura kwa kutumia tume za uchaguzi. Mwisho wa siku wananchi wanatangaziwa ushindi wa chama tawala. Katika mazingira haya uchaguzi hauna maana barani Afrika.

Jambo jingine linalofanya uchaguzi uonekane hauna maana barani Afrika, ni matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi. Matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi yanaathiri vyama visivyo na uwezo mkubwa wa kifedha na wagombea wasio na uwezo mkubwa wa kifedha.

Hii ni kusema kwamba gharama kubwa za uchaguzi zinasababisha chama kilichotoa mgombea bora kushindwa kwenye uchaguzi, pia mgombea mwenyewe kushindwa uchaguzi.

Tunaambiwa kuwa kuna sheria iliyotungwa kwa lengo la kudhibiti matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi. Hata hivyo, ni sheria iliyoshindwa kufanya  kazi.

Halafu kuna suala la kutumia nguvu kubwa na Serikali kudhibiti wapinzani wasishinde uchaguzi. Utakuta Serikali ya chama tawala inatumia polisi kudhibiti wapinzani wasifanye mikutano, wasiandamane, na washinde kwa mbinde.

Utakuta kwamba katika maeneo mengi nchini Tanzania, wapinzani hutangazwa kushinda uchaguzi baada ya kutumia nguvu kubwa na na vurugu kudai matokeo ya uchaguzi.

Maeneo ambayo wapinzani wanakuwa wapole wanaporwa ushindi. Hapa tena, ni wazi katika Afrika uchaguzi hauna maana. Kinachotakiwa ni mgombea aliyeshinda kutangazwa mara moja kuwa ameshinda bila kusubiri zitokee vurugu.

Jambo jingine linalovuruga chaguzi barani Afrika, ni kunyanyaswa wapinzani kwa lengo la kuwakatisha tamaa ili wasigombee tena katika chaguzi.

Halafu kuna suala la kukiuka Katiba. Ni kitu kilichofanyika Zanzibar. Baada ya kuonekana Chama cha Wananchi ( CUF)  kimeshinda uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, peke yake alichukua uamuzi wa kufuta uchaguzi huo.

Hakuna sehemu yoyote ya Katiba ya Zanzibar inayomruhusu mtu mmoja kufuta matokeo ya uchaguzi. Na hapa tena kama unafuta uchaguzi baada ya kufahamika matokeo yake una maana gani?

Hakuna anayetaka mabaya Zanzibar, lakini ukweli ni kwamba kitendo hicho kimeathiri sana umoja na amani ya Zanzibar.

Wazanzibari wanaishi katika hali ya wasi wasi wakati wanasubiri kurudiwa uchaguzi Machi 20, mwaka huu, uchaguzi ambao CUF imesema haitoshiriki.

Lakini pia kuna hii Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa Zanzibar ambayo ilishirikisha CUF kwa lengo la kuimarisha amani na mshikamano  wa Wazanzibari. Itaendelea kuwapo baada ya uchaguzi ambao CUF haitoshiriki?

Tukiendelea kuzungumzia uchaguzi wa Zanzibar ulivyofutwa bila kuzingatia Katiba, tutaona kwamba katiba za nchi za Afrika zinachangia pia uchaguzi uonekane  hauna maana.

Angalau Katiba ya Uganda inaleta picha kwamba inaruhusu uchaguzi huru na wa haki.

Tazama, wakati Katiba ya Tanzania inapiga marufuku matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani, Katiba ya Uganda inaruhusu.

Jambo jingine linalovuruga uchaguzi barani Afrika hata unaonekana hauna maana, ni kitendo cha marais wanaomaliza muda wao wa kutawala kubadilisha katiba za nchi zao ili waendelee kutawala. Kwa kifupi, katiba za nchi zinachezewa kwa manufaa ya watu wachache.

Tazama, Rais Yoweri Museveni wa Uganda aligombea uchaguzi wa rais baada ya kuondoa vifungu vya katiba vilivyowekwa ukomo wa kuomba kuteuliwa kuwa mgombea urais!

Nako Burundi, Rais Piere Nkurunziza amecheza na tafsiri ya katiba ya nchi yake na makubaliano ya amani ya Arusha.

 Naye Paul Kagame wa Rwanda, na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaendelea kucheza na katiba za nchi zao waendelee kutawala.

Hapana shaka marais wanaojiongezea muda wa kutawala wanatengeneza mazingira yanayowahakikishia ushindi. Hakika katika Afrika uchaguzi hauna maana.

By Jamhuri