Umakini ni muhimu katika jambo lolote, lakini pia uharaka ni muhimu zaidi. Haina maana kwamba kitu chochote kinachofanyika kwa umakini ni lazima kiendeshwe kwa ugoigoi na kwa kupoteza muda.

Ila uharaka ndiyo unaoonesha umakini unaotakiwa. Mtu makini ni mwepesi wa kufikiri na kuamua, na yule goigoi ni mcheleweshaji, mzembe, asiyeweza kufanya uamuzi kwa wakati unaotakiwa.

Kwa kipindi kirefu nchi yetu imezoea kuendesha mambo kwa ugoigoi na ucheleweshaji, unaoyafanya mengine yakwame na kuwakoshesha wananchi walichokihitaji.

Nakumbuka wakati fulani huko nyuma, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kwamba Tanzania tunapaswa kukimbia wakati nchi nyingine zilizotutangulia kimaendeleo zikitembea.

Mwalimu aliuhitaji uharaka katika kuitafutia nchi maendeleo, au kulimaliza tatizo lililokuwa linajitokeza na kuweka kizingiti kwenye njia yetu ya maendeleo.

Siyo kwamba Mwalimu Nyerere alitaka nchi yetu isiwe na umakini, hapana, alitaka iwe na umakini lakini ulio katika mwendo kasi. Maana uharaka ni sehemu ya umakini.

Wakati fulani John Barongo aliwahi kunieleza kwamba wakati akiwa mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma, alipokea simu usiku wa saa 7 na akasikia sauti: “Julius hapa, nakutaka uje mara moja usiku huu hapa Ikulu.”

Kumbe ndipo Mwalimu alipokuwa amemteua kuwa mkuu wa Wilaya ya Bukoba wakati huo nchi ikiwa kwenye vita dhidi ya Idi Amin wa Uganda.

Hilo linaonesha kwamba pale hapakuwa na kulala, maana Barongo alisema kwamba aliendesha gari na kufika Ikulu alfajiri akamkuta Mwalimu anamsubiri.

Ninachotaka kuonesha hapa ni kwamba uharaka unaendana na umakini. Nyerere alikuwa makini na mtu wa kufanya uamuzi wa haraka.

Hivyo ndivyo inavyotakiwa hasa pale nchi kama yetu ambayo bado inasuasua kimaendeleo, inapotaka kuwa kwenye kasi ya maendeleo na kujaribu kupunguza pengo lililopo kati yake na nchi zile zilizoitangulia.

Kwa kipindi fulani, ambacho kimedumu kwa muda mrefu, kasi na umakini wa aina hiyo vimepotea. Lakini katika awamu hii ya tano ni kama vimeanza kurudi. Tumejionea jinsi Dk. Magufuli alivyoanza kuvirudisha tangu aingie madarakani.

Mara moja baada ya kukikalia kiti cha enzi, Magufuli hakutaka kufanya maandalizi, kitu ambacho wenzetu hukiita ‘picnic’ au mapumziko ya kujipongeza kwa namna ya kufanya starehe.

Yeye kama alivyoahidi wakati anausaka urais, alionesha kwamba hapa kazi tu, akiwa na maana ya kwamba urais ni nafasi yenye jukumu la kuwatumikia wananchi na siyo nafasi ya kustarehe na kula nchi.

Kwa maana hiyo ni kwamba Magufuli kaanza kukimbia katika kujaribu kuziba pengo kati ya Tanzania na wale walioitangulia kimaendeleo.

Hana muda wa kukaa na kuanza kukitafakari kitu kinachojionesha wazi. Akiona mahala kuna jipu hana muda wa kukaa na kuanza kujiuliza jipu hilo limekuwaje mahali lilipo, yeye anachofanya ni kuliona na kulitumbua mara moja, mambo ya limetoka wapi yatakuja baadaye kama upo ulazima wa kujua chanzo chake.

Majuzi, tumeona mabadiliko ya haraka yaliyofanyika kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii baada ya kuondoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa muda mrefu wa mfuko huo, Dk. Ramadhani Dau.

Baada ya kuondoka huko kwa Dk. Dau, aliteuliwa mtu wa kukaimu nafasi hiyo, Dk. Carina Wangwe, ambaye ndani ya saa tano naye akaondolewa na kuteuliwa mtu mwingine.

Kutokana na mabadiliko hayo ya harakaharaka wapo waliodai kwamba hiyo ni sehemu ya udhaifu, jambo ambalo naona linatokana na kutotafakari mambo kwa kina.

Lakini kwangu mimi hilo naliona kama jambo mojawapo linaloonesha kasi inayotumika katika awamu hii ya tano. Nalipongeza sana jambo hilo.

Inapotokea kwamba jambo fulani limeshtukiwa halipaswi kupewa nafasi ya kujaribiwa hata kwa dakika moja, jambo limeshtukiwa kuwa halifai papo kwa hapo lifanyiwe mabadiliko.

Mambo ya kutoa muda wa majaribio ndiyo yaliyoigharimu nchi. Jambo halifai, lakini linapewa muda wa kujaribiwa mpaka pale litakapoonesha kuwa halifai linakuwa limeshaleta madhara makubwa.

Madhara yanayokuwa yametokana na majaribio nayo yanakuwa mzigo mwingine unaohitaji kutengewa bajeti, ili kuurudisha katika hali yake ya kawaida.

Kwa hiyo, badala ya kukimbia kuwakaribia walio mbele yetu kimaendeleo, achilia mbali kutembea au kusimama kabisa, inatubidi kurudi nyuma kupasahihisha tulikopitia! Huo si uzembe bali ni kufuru.

Uamuzi wa kufanya mabadiliko makubwa kama hayo ndani ya muda mfupi hayana budi kupongezwa. Hiyo ni kasi ambayo kwa muda mrefu tuliisahau.

Ndiyo kama ile aliyoisema Barongo ya Nyerere kumwita usiku wa manane kutoka Mpwapwa kwenda Ikulu pasipo kusubiri kupambazuke.

Kusema ukweli maendeleo yoyote yawayo yanahitaji kasi ya aina hiyo ambayo kwenye usemi unaotumika kwa sasa ni ‘hakuna kulala mpaka kieleweke’.

Sielewi wanaosema kwamba huo ni udhaifu walitaka iweje, kwamba uteuzi wa kaimu ungeendelea ili tuone kama mambo yangeharibika ndipo mamlaka za uteuzi zishtuke na kuubadilisha?

Hivi, kweli wenye mawazo ya aina hiyo wanaweza kusema wanaitakia mema nchi yao, au niseme nchi yetu, kwa vile inawezekana wao wameishajitenga nayo?

Siwezi kusema kwamba Dk. Wangwe hafai, inawezekana anafaa ila siyo kwa pale. Kwa hiyo, kitendo cha kumwona anayefaa zaidi siwezi kukitilia shaka kama kile cha kufanya mambo kwa majaribio.

Nimalizie kwa kuipongeza kasi inayoonekana kwenye Serikali hii ya awamu ya tano, Serikali isiyotaka kufanya mambo kimajaribio, hiyo ndiyo tunayoweza kusema ni ‘hapa kazi tu’. Majaribio hayajawahi kuwa kazi, sana sana ni mafunzo.

1641 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!