DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita serikali imetangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo mbalimbali, kilichowashtua wengi ni namna uchaguzi huo ulivyofanywa. 

Wazazi wengi wanalia; hasa wale maskini ambao hawana uwezo wa kuwapeleka watoto wao shule binafsi (private) kwa masomo ya kidato cha tano.

Kwa miaka mingi hata kabla ya uhuru, uchaguzi wa wanafunzi serikalini hutumia kitu kinachofahamika kama ‘sel-form’ ambazo hujazwa na wanafunzi wenyewe kabla au baada ya kumaliza kidato cha nne, kwa kuangalia mwenendo wa mitihani alivyofanya. 

Mara nyingi wanafunzi hujaza hizi fomu kwa ushauri wa wazazi, au walimu wao. 

Kwenye ‘sel-form’, mwanafunzi huchagua ‘tahasusi na vyuo anavyopenda yeye’ na wanaohusika katika kuwapanga au kuwachagua, hutumia machaguo ya mwanafunzi husika. 

Mwaka huu mambo hayakuwa hivyo. Mtoto amefaulu PCB au PCM vizuri tu, lakini anachaguliwa HKL; kweli hii ni sahihi?  (mtasema shule za sayansi ni chache).

Lakini haiji akilini mtu amefaulu Kemia katika daraja A, Jiografia daraja B na Baiolojia B lakini anapelekwa kusoma HKL alikopata C-C-C; au amefaulu vizuri HGL lakini anapelekwa kusoma Kompyuta, Fizikia na Hesabu. Je, aliomba kusoma masomo hayo?

Kituko kikubwa kilikuwa kwa wale waliofaulu kwa divisheni ‘one’ lakini wanapangiwa kusoma ‘Record Management’ na wala hawakuiomba. 

Yupo kijana ana ‘Division One’ ya alama 14, lakini anapangiwa kusoma Hotel Management huko Singida. 

Hivi kuna mzazi aliyekubaliana na wewe uliyeko ofisini hapo Dodoma kwamba anataka mwanaye asomee uhudumu wa hoteli?

Mwanafunzi mmoja ana ‘Division One’ ya alama 16, amepangiwa kusoma ‘Certificate in Community Development’ kule Tengeru. 

Ninyi maofisa Elimu Dodoma, mlizungumza  na mzazi wa huyu kijana akawaambia anataka mwanaye asomee maendeleo ya jamii?

Si kwamba ninabeza fani nyingine, la hasha! Bali kila mtu asomee anachokitaka! Mimi mwanangu ana kipaji cha kuchora, anataka awe msanii wa uchoraji kama Masoud Kipanya na nimejaza ‘sel-form’, wewe unamlazimisha akasome mifugo au utunzaji kumbukumbu! Kwa nini? 

Eti kwa sababu tu uko ofisini, unaamua. 

Nimesikitika kuona mwanafunzi mmoja amevaa mabango mengi mwilini akilia amepata ‘Division One’ ya alama 14, sasa amepangiwa kusoma Hotel Management wilayani Bagamoyo.

Ni nini kinachoonekana katika hali hii?

Kwanza, serikali imeona wanafunzi hawaendi kwenye vyuo vyao ambavyo hawatoi ajira na vyuo vingi vinakufa kwa kukosa wanafunzi. Sasa kilichopo ni kuwapeleka kwa nguvu.

Pili, ile tabia ya taasisi ya vyuo vikuu (TCU) kula na ‘wajanja’ wa vyuo vikuu, hasa vile vya binafsi kuwapangia wanafunzi, inahamia vyuo vya kati baada ya ‘Chuma’ kuondoka. 

Mwendazake alikataa hii tabia (ya rushwa), aliruhusu kila mwanafunzi asome chuo anachotaka na fani anayopenda! Sasa hivi tunalazimisha wanafunzi wakasomee Hotel Management!

Tatu, inaonekana vyuo vya kati vimeomba vipewe wanafunzi moja kwa moja kutoka wizarani bila kujali vipaji vyao, lengo lao ni kuwa na wanafunzi wengi ili wapate ‘capitation’. Wakufunzi wanajali pesa kwa kuua vipaji vya watoto wetu. Wizara nao wanajali pesa ya asante wanawateketeza watoto wetu.

Nne, hii ni mbinu chafu ya kuwatengenezea shule binafsi fedha. Tunalazimishwa kwa nguvu kuwapeleka watoto wetu shule binafsi kusoma kidato cha tano na cha sita. 

Kwa sababu haiwezekani mtoto amesota sana kusoma na kupata alama za juu kisha anaambiwa akasomee Ualimu wa Chekechea, Kasulu TC, eti kwa sababu tu mkuu wa chuo hicho amesoma na waziri fulani. 

Wazazi wasio na uwezo watawapeleka watoto wao kwenye shule gani binafsi mnazozitengenezea soko? 

Mzazi wa kutoka Machochwe, Buzilayombo au Kibanchabancha, atasomesha mwanaye kwenye shule zenu mlizojenga kama Feza, Mosabe au St. Francis? Angalizo langu na la Watanzania wenzangu ni kutaka kuwapo kwa ‘uhuru wa elimu’, kila mwanafunzi asome anachokitaka, akuze talanta yake aliyopewa na Mungu, si kulazimishwa kwenda kujaza vyuo.

Tunakuomba waziri mkuu; wewe ni mwalimu mwenzetu, hili lisikushinde. Tusaidie wazazi maskini tunaotaka watoto wasome wanachokitaka na kukipenda, si anachokitaka Mkuu wa Chuo cha Utalii Singida.

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, hizi ‘sel-form’ wanazojaza wanafunzi ni za nini? Kazi zake ni nini? Au mliiga kutoka kwa wakoloni bila kujua kuzitumia?

Mwandishi wa makala hii iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii amejitambulisha kama Mwalimu Matete, anapatikana kwa simu namba: +255 752 761 116

1393 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!