Katika makala iliyopita kwenye safu hii, tuliandika kwa makosa kuwa makala ile ingekuwa hitimisho. Tena kukawa na kosa lililoonyesha kuwa ilikuwa sehemu ya tano. Usahihi ni kwamba hii ndiyo sehemu ya tano na ya mwisho katika mfululilo wa makala hii ya “Udini sasa Nongwa.

Mhariri

Upo usemi wa mwanafalsafa mmoja wa Kiingereza, Fransis Bacom, usemao “Reading Makes a full man” na “Writing makes an exact man”. Usemi huu wa kale unamaanisha mtu akisomasoma vitabu/makala au anapevuka kiakili.


Aidha, akiandika hapo mtu anakuwa mkweli maana kwenye kuandika hakuna ubabaishaji, unaandika unachotaka kiandikwe na si vinginevyo.


Tabia yangu ya kujisomea imenipanua sana uwezo kifikra na tabia ya kuandika inaonyesha kile kinachodhamiriwa. Hivi karibuni nimepata kusoma kitabu kiitwacho “HOLY WAR IN ISLAM” kilichoandikwa na Bwana ABD AL-MASIH, nikaona katika kurasa 55-56 wazo kuu la harakati za uislamu. Yeye ameandika wazi kabisa hatua mbalimbali za jihad katika uislamu.


Labda nimnukuu kidogo hapa, “In countries where Islamic state has not yet been formed an Islamic reformation may occur, aiming to root out all reminders of Christianity and western colonialism from the laws of the land. Indeed there is potential for a revolution to over through the existing government with one that will implement the shariah. Countries like Lebanon, Malaysia, Nigeria and Tanzania are examples showing the long-term political strife and trials involved in farming Islamic States”.


Kwa tafsiri yangu, maana yake nchi zile zisizokuwa na serikali rasmi za kiislamu, marekebisho ya mfumo wa utawala wa kiislamu yaweza kutokea kulenga kung’oa mabaki yote ya ukristu na mabaki yote ya ukoloni katika sheria ya nchi kama hiyo.


Upo uwezekano wa mapinduzi kutokea katika serikali za aina hiyo kwa kuleta utawala wa sheria. Nchi kama Lebanon, Malaysia, Nigeria na Tanzania ni mifano ya kuonyesha migongano ya majaribio ya muda yenye kuhusisha uanzishwaji wa Taifa la Kiislamu.



Bwana Abd Al- Masih katika kitabu chake hicho anaendelea kuandika maneno haya, namnukuu tena, “The majority of the populations in these countries are NOT Muslims. Despite this ratio, Christian leaders are removed from their position of influence, one by one and news papers and other media increasingly, transmit Islamic propaganda. The atmosphere in these countries is often tense and explosive”.


Kwa tafsiri yangu ni kwamba wakazi wengi katika nchi hizo siyo waislamu.


Licha ya uwiano huu, viongozi ambao ni wakristo huondolewa mmoja mmoja  kutoka kwenye vyeo vyao vyenye ushawishi. Magezeti na vyombo vingine vya habari kutangaza propaganda za uislamu. Mazingira katika nchi hizi mara kwa mara huwa ni yenye kujawa na wasiwasi na yenye jazba.


Baadhi ya vyombo vya habari vya kiislamu vya hapa Tanzania kama vile Al-Nuur, Al-Huda, Radio Imani na jarida la kila mwezi la KHILAFAH vimekuwa mstari wa mbele katika kuzingatia habari zenye kulilaumu Kanisa na Serikali ya kidemokrasia iliyopo kuwa havitaki utawala wa kiislamu.


Je, maandishi namna hii kutoka kwa wasomi kama huyu mwandishi wa kitabu hicho cha Holy War in Islam uk. 56 ni mawazo endelevu ya kuleta au kujenga Amani na Umoja wa Kitaifa hapa Tanzania? SIDHANI! Kwanza tujiulize, huyu Abd Al- Masih ni mzalendo wa nchi hii? Mimi sijui. Ila maandiko yake haya niliyoyanukuu hapa yanaonyesha ni mpenda shari na amejaa chuki.


Lakini sisi watanzania  kwa kusikiliza mahubiri ya Sheikh Mkuu Shaaban Bin Simba au Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa tunatambua wazi tofauti kubwa ya moyo wa viongozi hawa na ule wa huyo Abd Al- Masih. Viongozi wetu wakuu kama Mufti au Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam daima wanahubiri ushirikiano, mshikamano kwa Watanzania wote. Ni moyo wa uzalendo kwa Taifa lao na nchi yao ya Tanzania.


Kumbe maandishi katika kitabu cha Bwana Abd Al- Masih ni tofauti kabisa. Inatokeaje hali hiyo? Msimamo upi ndiyo endelevu? DINI ISITUGAWE WANANCHI WAZALENDO WA TANZANIA. Mamluki wa nje wana nia zao na kamwe hawana uchungu wa Taifa hili. TANZANIA IJENGWE NA WENYE MOYO- wazalendo.


Kinachoandikwa ndicho kiwe cha kweli na kilichodhamiriwa. Hivyo naelekea kuamini kwamba Bwana Abd Al-Masih amedhamiria kutuvuruga kama inavyovurugwa nchi ya Mali. Viongozi wetu wa dini na sisi waumini letu liwe moja lile lile la UMOJA NA AMANI katika nchi yetu. “ALUTA CONTINUA”

Brigedia Jenrali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806 758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


By Jamhuri