Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wamefanya mazungumzo Ikulu ya Dar es Salaam na kufikia makubaliano kadhaa muhimu kwa wananchi wa mataifa haya jirani.

Mazungumzo yao yalikamilika kwa kutiliana saini mikataba minane katika nyanja tofauti, huku pia viongozi hao wakuu wakibadilishana zawadi kama ishara ya udugu kati ya mataifa wanayoyaongoza.

Kwa pamoja wakuu hawa wa nchi wamekubaliana kuondoa mara moja vikwazo 46 vya kibiashara vilivyokuwa vikionekana kuwa kero kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili. 

Ni kweli kwamba mataifa haya yana historia ndefu ya ujirani, yakiwa na jamii kadhaa zenye uhusiano wa kitamaduni kama Wajaluo, Wamasai, Wakurya na Wadigo, hivyo ni muhimu kuishi kwa upendo, uelewano na ushirikiano.

Kwa kutambua hayo, marais Samia na Uhuru wamekubaliana kuimarisha biashara kati ya mataifa haya ikiwamo ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa na barabara ya pwani kutoka Bagamoyo hadi Malinyi.

Baadhi ya mikataba mingine iliyosainiwa ni ya kisheria, kubadilishana wafungwa, uhamiaji, afya ya wanyama, uwekezaji na maendeleo ya miji na makazi; yote haya yakilenga kujenga uhusiano mwema.

Lakini kwa upande mwingine, uhusiano kati ya Tanzania na Kenya huwa ni wa shaka na wa kutoaminiana, ingawa hakujazuka ugomvi mkubwa wa kuhatarisha amani kwa pande hizi mbili.

Kwamba, mataifa haya yanategemeana, ni suala lisilokuwa na ubishi na ndiyo maana tunaunga mkono jitihada za viongozi wa sasa na waliopita za kuhakikisha kunakuwa na upendo na utulivu miongoni mwa wananchi wa pande zote mbili.

Kwamba, mataifa haya yanategemeana sana katika ikolojia ya utalii na kwamba ni muhimu kwa kila upande kulinda na kuhifadhi mazingira ni masuala yasiyoweza kupingwa.

Lakini ni lazima tukubaliane na ukweli kuwa kila taifa linahitaji kunufaika na maliasili liliyopewa na Mwenyezi Mungu; miongoni mwa maliasili hizo ni vivutio vya utalii.

Hatuna shaka kuwa Rais Samia yupo madarakani chini ya kiapo cha kulinda na kusimamia masilahi ya taifa letu, hivyo kila anachokifanya kinaendana na kiapo chake.

Kwa maana hiyo, pamoja na nia njema ya kushirikiana na Kenya katika biashara, utalii na masuala mengine ya kiuchumi, tunaamini wenzetu hawa hawatarejesha ile nia yao ya muda mrefu ya kufungua mpaka wa Gologonja unaotenganisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na ile ya Maasai Mara ya Kenya.

By Jamhuri