Wiki iliyopita Taifa la Uingereza limepiga kura ya kujiondoa kwenye Umoja wa Jumuiya ya Ulaya (EU). Hoja zilizotumiwa na wahafidhina kufikia uamuzi huo ni kwamba wageni wengi wanaingia nchini Uingereza na hivyo kuchukua nafasi zao za ajira. Suala jingine wanasema wanakosa uhuru wa kufanya biashara na nchi zilizoko nje ya EU hadi waombe kibali.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ameamua kujiuzulu wadhifa huo ndani ya miezi 3 akisema yeye alitaka Uingereza iendelee kubaki ndani ya EU kwa sababu za kiusalama, biashara na mahusiano ya jamii. Aliamini na baadhi ya Waingereza waliopiga kura ya kubaki EU baada ya kuwapo kwa miaka 43 waliamini kuwa kujiondoa ni kujitengenezea ukiwa.

Kati ya hoja walizojenga waliotaka Uingereza ibaki, ni pamoja na watoto wao kupata fursa ya kusafiri, kusoma na kufanya kazi katika mataifa ya Ulaya, hali inayoweza kuwaongezea weledi na kuifanya dunia kuwa salama zaidi. Wakati huo huo, Scotland, ambayo ni sehemu ya Uingereza sasa inasema haioni sababu ya kubaki kama sehemu ya Uingereza.

Nchi hiyo inasema haiwezi kuamuliwa na wahafidhina wa Wales wenye chuki dhidi ya raia wa nchi nyingine duniani, ambao wanadhani kujitenga ndiyo msingi wa maendeleo, hivyo nao sasa wametangaza nia ya kuitisha upya kura ya maoni kwa nia ya kujiondoa katika Muungano wa Uingereza. Washirika wengine katika muungano huo ni Ireland na England.

Mwaka 2014 Scotland walitaka kujitoa katika Muungano wa Uingereza, ila wakabaki baada ya kupewa ahadi kuwa Uingereza haiwezi kujitoa kwenye EU. Sasa ukweli kwamba Uingereza imejitoa EU unaweza kuwa mwanzo wa taifa hilo kubwa kiuchumi kusambaratika. Ikiwa Scotland itaitisha kura ya maoni kwa sasa ni wazi watajiondoa, na washirika wengine wanaweza kuwaiga.

Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, amewapongeza Waingereza kwa kusema uamuzi wa kujitoa EU umewapa uhuru wa kweli. Ni wazi kuwa Trump anaamini katika siasa za ubaguzi. Boris Johnson aliyeendesha kampeni ya Uingereza kujitoa EU ndiye anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza. Naye, ana vimelea vya ubauguzi.

Dunia ya sasa inajielekeza zaidi katika kuungana. Ni jambo la aibu kuona mataifa hayo makubwa, yanakaribia kupata viongozi wanaoamini katika utengano. Kujitoa kwa Uingereza madhara yake tayari yameonekana. Sarafu ya Uingereza; Paundi imeshuka thamani. Wawekezaji wameanza kuhamisha mitaji yao. Uingereza na Marekani zinapaswa kuwatathimini viongozi hawa na kujitathimini pia, vinginevyo wataiingiza dunia katika matatizo makubwa si muda mrefu wasipowadhibiti.

1302 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!