Kazi ya utekelezaji wa ujenzi wa Gati mpya kwa ajili ya kuhudumia Meli za magari (RoRo Berth) kwenye Bandari ya Dar es Salaam imefikia asilimia 50 na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2019.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema mbali na kukamilika kwa ujenzi wa Gati hiyo unaotarajiwa kukamilika katikati ya 2019, kazi ya kuboresha Gati namba 1 tayari ilishakamilishwa na Mkandarasi tangu tarehe 7 Disemba mwaka 2018.

“Mkandarasi alikamilisha kazi ya ujenzi wa Gati namba 1 ambayo ilihusisha kuongeza eneo la kupakia na kupakua mizigo pamoja na kuongeza kina cha maji mpaka mita 14.5 na kazi kama hiyo kwenye Gati Namba 2 mpaka 4 ambayo inatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa ifikapo mwezi Julai mwaka huu 2019,” amesema Kakoko.

Mkurugenzi Mkuu amebainisha kwamba kwa upande wa ujenzi kwenye Gati namba 5 mpaka 7 kwa sasa Mkandarasi anaendelea na usanifu wa kina (detailed design) ambapo kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza mwezi Novemba 2019.

Mradi wa uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) unatekelezwa kwa awamu mbili ili kutoathiri uendeshaji wa shughuli za Bandari (port operations) wakati wa utekelezaji wake. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mradi inahusisha maboresho ya Gati namba 1-7 pamoja na Gati mpya kwa ajili ya Meli za magari.

Gati hiyo mpya inajengwa kwenye eneo la Gerezani Creek ambapo TPA ilisaini mkataba na Mkandarasi M/s China Habour Engineering Company Limited kutoka nchini China tarehe 10 Juni 2017 kwa kipindi cha miaka mitatu huku gharama za Mradi zikikadiriwa kuwa ni Shilingi Bilioni 330.

Awamu ya pili ya ujenzi wa Mradi itahusisha kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia na kugeuzia meli kitaalamu ikifahamika kama “deepening and widening of entrance channel and turning basin”.

Mpaka sasa Mamlaka ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi ambapo zabuni ya awali (expression of interest) kwa ajili ya kupata wakandarasi wachache watakaofuzu kushindanishwa ili kumpata Mkandarasi wa kazi husika ambapo uthamini wake umeshakamilika kwa ajili ya kuwashindanisha washindi wa awali.

Hatua ya pili ya zabuni itakuwa ni “Request For Proposal (RFP)” ambayo itafanyika mara baada ya kukamilika kwa tafiti na usanifu wa Mradi (engineering surveys, environmental and social assessment and detailed design).

Kazi kwa ajili ya kufanya usanifu Study and Design) inatarajiwa kukamilika Mei 2019 ambapo Mtaalamu Mwelekezi (Consultant M/s Technical) kutoka Italia anayeangalia namna bora ya kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli na kutengeneza nyaraka (tender document) anaendelea na kazi.

Kwa upande wa kazi ya kufanya uthamini wa athari za kijamii na kimazingira (environment and social impact assessment) inafanywa na Mtaalamu Mwelekezi Kampuni ya M/s Asian Consulting Enterprise ambaye anaendelea na kazi hiyo na anatarajia kuikamilisha ifikapo mwezi Mei 2019.

Aidha hatua ya pili baada ya tafiti na usanifu (study and design) kukamilika ni zabuni kutolewa kwa makampuni yaliyoshinda katika awamu ya kwanza (pre-qualifification) kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa kazi ya kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli na sehemu ya kugeuzia meli kazi ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2019.

Kwa kutambua ukweli kwamba usafirishaji mizigo unategemea kwa kiasi kikubwa usafiri wa njia ya reli, kazi ya uboreshaji wa mtandao wa reli ndani ya Bandari ya Dar es Salaam nayo itakuwa ni sehemu ya tatu ya maboresho katika awamu ya kwanza ya Mradi huu wa DMGP.

Aidha, Mtaalamu Mwelekezi (M/s Gauff) anaendelea na kazi ya usanifu (detailed design) kupitia Mradi wa “Tanzania Intermodal Transport Program (TIRP)” unaosimamiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kugharamiwa na Benki ya Dunia. Kazi ya kuboresha mtandao huo wa reli inatarajiwa kuanza mara tu Mtaalamu atakapokamilisha usanifu.

Sehemu ya nne ya awamu ya kwanza ya Mradi huu pia itahusisha kuimarisha na kuongeza kina katika Gati Na. 8-11 ili ziweze kuhudumia meli kubwa na za kisasa. Katika kutekeleza sehemu ya Mradi huu TPA imeandaa hadidu za rejea (Terms Of Reference) kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu (feasibility study and detailed engineering design) wa Mradi.

Zabuni hii inatarajiwa kutangazwa mwezi Mei 2019 na kazi ya upembuzi yakinifu itaanza mwezi Oktoba 2019 ambapo kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza mwaka 2021 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Gati namba 1-7.

Kuhusiana na ujenzi wa Gati 12-14 katika Bandari ya Dar es Salaam, Mhandisi Kakoko amebainisha kwamba mara baada ya kushauriana na wafadhili wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ambao ni pamoja na Benki ya Dunia, DFID na TradeMark East Africa (TMEA) imekubalika kwamba ili kuboresha Bandari kwa ujumla Gati zote za Bandari, Gati namba 12 (kwa sasa KOJ) hadi namba 15 zitajumuishwe kwenye Mradi wa DMGP.

Kwa kuzingatia majadiliano yaliyofanyanyika na ushauri uliotolewa, ujenzi wa Gati hizo umependekezwa uingie katika awamu ya pili (phase II) mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Mradi wa DMGP.

Mara baada ya kukamilika kwa awamu zote za Mradi wa DMGP, Bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia meli kubwa zaidi na za kisasa. Inatarajiwa kwamba Bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu (length overall) wa mita mia tatu na tano (305) zenye uwezo wa kubeba kontena (TEUs) kati ya 7,000 mpaka 8,000.

Bandari ya Dar es Salaam pia itaongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa zaidi ya mizigo kutoka uwezo wa sasa wa kuhudumia tani milioni 16 hadi kufikia tani milioni 28 hadi tani 30 kwa mwaka. Hali hii inatarajiwa pia kuongeza mapato ya TPA na Taifa kwa ujumla kutokana na uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia shehena kubwa zaidi.

Mpango wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam uliibuliwa kutoka katika Mpango Kabambe (Port Master Plan) wa Mamlaka wa miaka 20 (2009-2028) ambapo mwaka 2013 TPA ilikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu wa kuboresha Gati namba 1-7.

Kazi hiyo ya upembuzi yakinifu ilihusisha kuona namna bora ya kuongeza kina na kuimarisha Gati namba 1-7, kuongeza kina cha lango la kuingilia meli (entrance channel) na eneo la kugeuzia meli (turning basin) pamoja na ujenzi wa Gati mpya ya kuhudumia magari.

Katika upembuzi huo ambao uligawanyika mara mbili, sehemu ya pili ilihusisha kuangalia njia bora ya kuhudumia shehena mbalimbali na uboreshaji wa mindombinu ndani ya Bandari ya Dar es Salaam kwa ujumla ikiwa ni pamoja na mpangilio wa Bandari (improvement of port layout).

Kazi hizo pia ni pamoja na ujenzi wa Gati jipya, barabara ziingiazo na kutoka Bandarini, reli, uhamishaji na ujenzi wa maghala, ujenzi wa maeneo ya uendeshaji (operational yards) na ufungaji wa mfumo (conveyor systeam) wa kuhudumia shehena ya kichele (nafaka, mbolea, saruji na clinker).

Mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu kukamilika zilianza juhudi za kutekeleza Mradi ambapo Septemba 2014, ujumbe wa pamoja wa Wadau wa Maendeleo ukiwahusisha TradeMark East Africa, Department of International Development (DFID) na Benki ya Dunia ulifika Tanzania kwa ajili ya kuthamini Mradi wa uboreshaji  wa Bandari ya Dar es Salaam na kuingia makubaliano ya awali (MoU) na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi husika.

Mara baada ya MoU kusainiwa, uthamini wa utekelezaji wa Mradi na shughuli mbalimbali za Mradi ziliendelea na maandalizi ya tathimini ya Mradi (project appraisal document – PAD) yalikamilika mwezi Mei 2017 ambapo makubaliano baina ya Serikali na Benki ya Dunia ya mkopo wa Dola za Marekani Milioni 345 kwa ajili ya uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam-DMGP yalisainiwa mwezi Oktoba 2017.

Aidha uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam pia utawezesha kuiongezea ufanisi wa utendaji na ushindani baina yake na Bandari nyingine za ukanda wa Bahari ya Hindi kama vile Mombasa, Maputo, Beira, Nacala na Durban.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA anahitimisha kwa kusema kwamba TPA inatambua na kuthamini ushirikiano inaoupata kutoka Serikalini, Bunge, Wadau wote wa Sekta ya uchukuzi pamoja na wahisani wa maendeleo kama vile Benki ya Dunia.

1014 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!